Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

DAR ES SALAAM

Na Pd. Audiphace Mujuni

Maana ya Msalaba
Msalaba wa Kristo ni Altare ya Agano Jipya linalotoa Sakramenti za Fumbo la Pasaka, Katekisimu ya Kanisa Katoliki (KKK) Na. 1182. Ni mahali Kristo alipojitoa sadaka kwa ukombozi wetu, hivyo Msalaba ni Altare ya Kwanza ambapo Kristo alijitoa sadaka.
Msalaba ni ishara ya utawala wa Kristo na kushindwa kwa shetani. Msalaba ni Ukombozi wa mwanadamu, Matayo 20:28, “kama vile mwana wa Adam asivyokuja kutumikiwa bali kutumika na kuitoa nafsi yake iwe fidia kwa wengi.” Hii ni Alama Kuu katika Ukristo
Aina Mbalimbali za Misalaba.
Kuna aina nyingi za misalaba kadri ya sehemu na tamaduni husika, lakini yote inamaanisha jambo moja kuu katika Ukristo, kusulibiwa kwa Kristo.
Msalaba wa Kilatini (Crucifix), ndio maarufu zaidi. Msalaba wa Ki-Keltiki (wa Scotland), una duara kuzunguka maunganio ya msalaba. Msalaba wa Kigiriki, una umbo la herufi X. Msalaba wa Yerusalem una umbo kubwa kama wa Kilatini, lakini una misalaba mingine midogo midogo, katika vile vipembe vinne.
Historia ya Msalaba
Msalaba kama alama ya mistari miwili inayokutana katikati, ilikuwapo na ilitumika kama ishara takatifu kwa baadhi ya dini au Imani mbalimbali, hata kabla ya kuzaliwa Kristo. Kadri ya mwana historia Tyack G. S., alama ya msalaba ilitumiwa kama ishara takatifu ya muungu Bacchus wa Kigiriki na muungu Bel wa Wakaldayo miaka mingi kabla ya kuzaliwa Kristo, na waliiweka katika sarafu za pesa zao.
Pia, mwana historia Cutner H. anasema kuwa alama ya msalaba wenye duara juu yake, ilitumika na Wamisri miaka mingi kabla ya kuzaliwa Kristo kama ishara ya muungu wao wa uzazi. Waliiweka kwenye paa za majengo yao na kwenye makaburi yao kama alama takatifu.
Lakini pia, historia inaonesha kuwa kuanzia karne ya 6 Kabla ya Kristo (KK) hadi karne ya 4 Baada ya Kristo (BK), alama ya msalaba ilitumika kama chombo cha utekelezaji wa hukumu ya kifo kwa watu waliohukumiwa kufa kifo kibaya na cha uchungu au maumivu makubwa.
Aliyehukumiwa alipigiliwa misumari kwenye mbao mbili zilizounganishwa kwa maumbo tofauti tofauti (kama + au X, n.k.), na kumuacha hapo juu afe taratibu. Hii ilifanyika sana nyakati za utawala wa Wagiriki na Warumi katika sehemu walizozitawala na Uyahudi ikiwemo. Hivyo kwa watu hawa, msalaba ilikuwa ishara ya kifo cha aibu, na ni kwa mtazamo huu Yesu pamoja na wafuasi wake wa mwanzo (hasa Mitume), waliuawa msalabani kama ishara ya kuwadhalilisha.
Utamaduni wa kutundika vitu kwenye miti maalum na kutumika kwa ibada, hasa za uponyaji, ulikuwepo pia kati ya Wayahudi tangu mapema. Tunasoma katika kitabu cha Hesabu, 21:4-9 kuwa baada ya manung’uniko na kutenda dhambi, Waisrael waliadhibiwa sana kwa kuletewa nyoka wenye sumu kali na kwasababishia vifo vingi huko jangwani, baadae Mungu akamuamuru Musa atengeneze Nyoka wa shaba na kumtundika juu ya mti ili kila atayemuangalia baada ya kugongwa na nyoka, atapona. Hili lilifanyika, na kweli watu wakapona.
UKUU WA MSALABA
Baada ya kuwa tumeona matumizi mbalimbali ya alama ya msalaba, sasa tuone, Utukufu wa Msalaba unatokea wapi?
“Maana kama vile Musa alivyomuinua yule nyoka jangwani, vivyo hivyo mwana wa Adam hana budi kuinuliwa, ili kila mtu aaminiye awe na uzima wa milele katika yeye,..maana Mungu hakumtuma mwanae ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye.” Yohana, 3: 16-17.
Kristo anapoamua kuutumia msalaba kama njia ya ukombozi wa ulimwengu, anaubadilishia maana kutoka kuwa alama ya aibu, uovu, udhaifu na kifo, na kuwa alama ya Ushindi kwa wale wanaomuamini Mungu na Kristo wake. HUU NDIO UKUU WA MSALABA. Msalaba unakuwa ndiyo njia ya kumwendea Mungu. Msalaba unakuwa in ALAMA YA UZIMA WA MILELE.
MAMBO YANAYOAMBATANA NA UKUU WA MSALABA
Msalaba ni hitaji la lazima la kumfuata Yesu.
Luka, 9:23-25, “akawaambia wote, mtu yeyote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate.” Bila Imani katika msalaba na kuwajibika kwa mahitaji ya msalaba, hatuwezi kumfuata Kristo, hatuwezi kumfikia Kristo, na hivyo hatuwezi kuokolewa na Kristo.
Msalaba ni Njia ya kueneza na kusimika Ufalme wa Mungu popote.
KKK, (Na. 550,853), “Ni kwa njia ya toba na kujifanya upya, na kwa kufuata njia nyembamba ya msalaba, ndipo taifa la Mungu linapoweza kueneza ufalme wa Mungu.”
Msalaba ni njia ya Utakatifu.
KKK (Na. 2015), “Njia ya ukamilifu hupitia kwa njia ya msalaba. Hakuna utakatifu bila majikatalio na bila vita ya kiroho.”
Msalaba ni mfano wa mshikamano na upendo wa Mungu kwa watu wake, na kati ya watu wenyewe, KKK (Na. 1939).
MSALABA NI ISHARA YA TOBA KAMILI.
Wagalatia, 2:19-21, “…, mimi nimekuwa pamoja na Kristo msalabani, na sasa naishi, lakini si mimi tena, bali Kristo anaishi ndani yangu. Maisha haya ninayoishi sasa, naishi kwa Imani, Imani katika mwana wa Mungu aliyenipenda hata akayatoa maisha yake kwa ajili yangu. Sipendi kuikataa neema ya Mungu,…”
Tukijifungamanisha na msalaba tunastahilishwa kuwa wenye haki, yaani watakatifu (Webrania, 5:9).
Tukifungamanisha na msalaba, tunakuwa huru dhidi ya dhambi, (Wagalatia, 5:1). Tunatakiwa kusimama imara ili tusinaswe tena chini ya konga la dhambi.
Kama tukiukubali Msalaba, unatupa nguvu ya kutubu dhambi, Luka, 23:39-43. Mwizi alikubali msalaba wake na kusamehewa dhambi zake.
“Kwa sababu neno la msalaba kwao wanaopotea ni upuuzi, lakini kwetu sisi tunaokolewa, na ni nguvu ya Mungu,.. kwa Wayahudi jambo hili ni kikwazo na kwa watu wa mataifa ni upumbavu, lakini kwa wale walioitwa Wayahudi kwa Wayunani (watu wa mataifa), Kristo ni nguvu ya Mungu na hekima ya Mungu. Maana kinachoonekana kuwa ni upumbavu wa Mungu, kina busara kuliko hekima ya binadamu; na kinachooneka kuwa ni udhaifu wa Mungu, kina nguvu kuliko nguvu za binadamu...” 1Kor. 1:18-32
Tupate nguvu ya kumshinda shetani kwa msalaba wa Kristo. Tupate hekima ya Kimungu kwa msalaba wa Kristo. Weka msalaba uliobarikiwa na Shemasi, Padri au Askofu nyumbani mwako, vaa msalaba huo shingoni, nk, kama ishara ya kuishi na nguvu ya Kristo na kuishi katika Nguvu ya Kristo, na kama ishara ya kuurithi uzima wa milele.
Silaha yetu iwe ni msalaba katika maisha yetu, tukaubebe kijasiri na kusonga mbele kuuelekea uzima wa milele. Msalaba ni alama ya kuzikataa anasa za kidunia. Msalaba ni alama ya kujitoa bila kujibakiza, na Msalaba ni ishara ya sala ya Mnyenyekevu.
Matayo, 12:20, Isaya, 42:1-4, “Tazama mtumishi wangu niliyemteua, mpendwa wangu anipendezaye moyoni. Nitaiweka roho yangu juu yake, naye atatangaza hukumu yangu kwa mataifa yote. Hatakuwa na ubishi wala kupiga kelele, wala sauti yake haitasikika barabarani. Mwanzi uliopondeka hatauvunja, wala utambi ufukao moshi hatauzima, mpaka atakapoifanya hukumu ya haki itawale. Kwake yeye mataifa yatakuwa na matumaini.”
HITIMISHO
“Kwa sababu neno la Msalaba kwao wanaopotea ni upuuzi, lakini kwetu sisi tunaookolewa, ni nguvu ya Mungu,.. kwa Wayahudi jambo hili ni kikwazo na kwa watu wa mataifa ni upumbavu, lakini kwa wale walioitwa, Wayahudi kwa Wayunani (watu wa mataifa), Kristo ni nguvu ya Mungu na hekima ya Mungu, maana kinachoonekana kuwa ni upumbavu wa Mungu, kina busara kuliko hekima ya binadamu; na kinachoonekana kuwa ni udhaifu wa Mungu, kina nguvu kuliko nguvu za binadamu...” 1Kor. 1:18-32
Tupate nguvu ya kumshinda shetani kwa msalaba wa Kristo. Tupate hekima ya Kimungu kwa msalaba wa Kristo. Weka msalaba uliobarikiwa na Shemasi, Padri au Askofu nyumbani mwako, vaa msalaba huo shingoni, n.k., kama ishara ya kuishi na nguvu ya Kristo na kuishi katika Nguvu ya Kristo, na kama ishara ya kuurithi uzima wa milele.
Silaha yetu iwe ni msalaba katika maisha yetu, tukaubebe kijasiri na kusonga mbele kuuelekea uzima wa milele.

Pd. Audiphace Mujuni
Jimbo Katoliki la Bunda.

Waamini wa Parokia ya Bikira Maria Mama wa Rozari Takatifu - Makongo Juu, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam wakiwa kanisani wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya Dominika ya Nne ya Kwaresma, iliyokwenda sanjari na kuweka jiwe la msingi la shule ya Parokia hiyo. (Picha na Mathayo Kijazi)

Msimamizi wa Kituo cha kulelea watoto (‘Children’s Home, Msimbazi’), Sista Stella Zavery akipokea misaada kutoka kwa Wazee na Wastaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam walipofranya matendo ya huruma katika kituo hicho kilichopo Parokia ya Msimbazi, jimboni humo.

Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Henry Mchamungu akibariki vipaji wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya Dominika ya Nne ya Kwaresma iliyoadhimishwa katika Kigango cha Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu, Parokia ya Mtakatifu Augustino, Salasala jimboni humo. Katikati ni Paroko wa Parokia hiyo, Padri Peter Assenga.

Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Henry Mchamungu (katikati), akiwa katika picha ya pamoja na Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) wa Parokia ya Mtakatifu Augustino, Salasala jimboni humo, baada ya Adhimisho la Misa Takatifu ya Dominika ya Nne ya Kwaresma iliyokwenda sanjari na Askofu kukagua ujenzi wa kanisa la Kigango cha Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu parokiani humo. Kulia ni Paroko wa Parokia hiyo, Padri Peter Assenga, na kushoto ni Dekano wa Dekania ya Mtakatifu Thomas More, Padri Romwald Mukandara.

MWANZA

Na Paul Mabuga

Biashara ya huduma ya usafiri wa pikipiki maarufu hapa Afrika Mashariki na hata katika miji na vijiji vyetu kama bodaboda, ni ajira ya uhai na kifo!
Ni kazi ya raha kwa kuwa inaiingiza  kipato, lakini pia ni ya karaha kutokana na wakati mwingine jamii inavyowatazama wanaoiendesha.
Pia, kazi hii imejaa mzuka wa kilele cha tijira kwa vijana wa fasheni, wanaopenda muziki ‘mnene’ na bomba la moshi linalobalaruka kwa sauti kubwa.
Kwao, hawa hii ni ruya ya kupaa hadi anga la saba na kujisikia katika ndoto ya kilele cha furaha, na hili ni zilizala katika ajira hii, ikisimuliwa kwa Tumaini Letu na waendesha bodaboda watatu kutoka katika Jiji la Mwanza.
Wa kwanza ni Emmanuel Kalima mwenye umri wa miaka 32 hivi sasa na mkazi wa Ilemela katika jiiji la Mwanza. Leo  analazimika kuendesha bajaji katika  kituo cha Sabasaba jijini humo baada ya kupata ulenavu uliotokana na kukatwa mguu wa kulia  kufuatia ajali aliyoipata miaka tisa iliyopita  wakati akiwa na kazi ya kuendesha bodaboda.
Kalima yupo katika kituo chake cha kazi akisubiri abiria, akiwa na Rozari yake shingoni, bila shaka ana matumaini kibao kwamba  maombi yake yatasikika, pengine leo kama jana atapata fedha ya kutosha kununua chakula kwa  familia yake ya  watoto wawili na mke, pia kumudu mahitaji ya shule kwa wanae wawili  wakubwa wanaosoma darasa la kwanza na la pili mtawalia. Lakini pia ana jukumu la kupeleka hesabu kwa mmiliki wa chombo hicho cha usafiri.
“Nipo naishi na mke wangu na watoto, na maisha ni ya furaha, hakuna unyanyapaa ndani ya familia yangu, na kuna mapenzi makubwa. Tunafurahia maisha kwa wakati huu,” anasema Kalima ambaye mara baada ya kumaliza elimu yake ya Kidato cha Nne  mwaka 2007, aliingia katika mapambano ya kutafuta naisha.
Wa pili ni Nhumba Mihaye ambaye pia aliacha kazi ya udereva wa bodada aliyokuwa akiifanya katika jiji la Mwanza na  kuamua kuedesha bajaji katika kituo cha Buswelu jijini humo.
Kwa sasa ana umri kama wa miaka 55 hivi na alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kuanza biashara hiyo ya huduma katika jiji hilo. Kama ilivyo kwa Kalima, Mihaye naye anatakiwa kukamilisha hesabu ya ‘bosi’ na nyingine ya kujikimu kwa familia yake.
“Boda hapa ziliingia mwaka 2008, na mie wakati huo niliingia kufanya kazi hiyo. Ili kumudu maisha na mipango yangu, nilikuwa nakesha na  kipindi hicho kupata hesabu ya shilingi 70,000/- hadi 80,000/- kwa siku, ilikuwa ni kawaida.
 Ingawa abiria walikuwa wachache, lakini na sisi watoa huduma tulikuwa wachache, na  kazi ilikuwa nzuri kwa kweli kulinganisha na sasa  hivi ambapo ushindani ni mkubwa, na watu wamepigika, hawana fedha hadi wengine wanatembea kwa miguu” anasema Mihaye.
Anashukur u kwa kazi hiyo kwa kuwa ameweza kujenga nyumba, na ana watoto ambao angalau wamesoma hadi chuo kikuu. Lakini changamoto alizokutana nazo wakati huo ndizo zilizomfanya aachane na udereva wa  bodaboda, hasa baada ya kuona kuwa anaweza kupoteza maisha.
Wa tatu ni Bahati Yohane, mkazi wa Kiseke Jijini humo, na  yeye anashukuru kwa kazi ya bodaboda kwa kuwa  ilimfanya akapata mke ambaye anaye hadi sasa. Anasema wakati huo anaendesha boda boda, mambo yalikuwa mazuri na hata alimudu kila mahitaji katika familia yake.
“Kutokana na kuwa na fedha nyingi, nilijikuta naongoza matumizi ambapo kila baada ya kazi kabla ya kurudi nyumbani, nilikuwa napita baa na kupata  [nakunywa bia] kidogo.  Ilifikia mahali, mke wangu alikuwa anagomba sana kuendesha piki piki nikiwa nimelewa, lakini sikukoma, hadi nilipokomeshwa, na ndiyo maana unaniona hivi, nachechemea,” anasema Yohane ambaye ana umri wa miaka 46, ambaye kwa sasa amehamia kwenye bajaji.
Yohane anasema kuwa nyakati hizo wandesha bodaboda walikuwa wakituhumiwa  kuwapa ujauzito mabinti wanafunzi, na anadai kwamba kwa siku hizi hilo limepungua  kwa kuwa wasichana wengi wamejitambua na hawadanganyiki na vitu vidogo vidogo kama ilivyokuwa zamani. Na pia wazazi wametambua majukumu yao ya kuwatimizia mahitaji mabinti zao.
Anasema pia ni kweli wapo waendesha boda boda  ambao hata wanafikia hatua ya  kufukuzwa kwenye vituo kutokana na tuhuma za unyanyasaji wa kingono kwa abiria wao, wakiwemo watoto na wanawake. Anaongeza kuwa licha ya tabia hizi mbaya  kupungua, lakini zimekuwa zikijenga taswira mbaya ya kazi hiyo machoni pa jamii.
“Ila kisa cha kuacha kazi ya bodaboda, ilikuwa ni siku moja pale Kiseke, nilikuwa nimekunywa pombe na naendesha, nikajikuta naingia  barabara kubwa bila tahadhari. Ilitoka huko, bodaboda kwenye barabara kuu ikiwa kasi na kunichota kama  mwewe anavyonyakua ikifaranga. Kutoka hapo sikujitambua hadi nilipojikuta  hospitalini natibiwa na hicho ndicho kisa cha huu ulemavu nilionao,” anasimulia Yohane.
Kwa upande wake Mihaye anasema kuwa kuna mtindo wa vijana, kupanua mabomba ya moshi ya pikipiki zao ili zitoe mlio mkubwa wakiendesha, wengine wanaweka muziki sauti ya juu kujifirahisha na hata kuzing’oa sight mirror  [vioo vye pembeni; na kuweka urembo mwingine kama fasheni.
“Ila wengi wanaong’oa vioo vya pembeni, huwa ni wahalifu, nia yao huwa ni kwamba wakimkwapua abiria wa pikipiki ya mbele yao au mtembea kwa miguu, wakimbie bila kikwazo cha kuona kuna mtu anawafuata, wanaamini kwamba, wakiwa wanaona wanafuatwa wataghafirika na kupunguza mwendo,” anasema Mihaye na kuongeza,
“Kuna siku nilikuwa na abiria mwanamke napita barabara ya hospitali ya mkoa  wa Mwanza, Sekou Toure. Vijana wanamna walikuwa nyuma yangu na pikipiki yao, wakakwapua mkoba wa abiria huyo. Niliamua kumshusha na kuanza kuwafukuza.
Walikuwa  wakikata mitaa ninao, huku ninapiga kelele  za mwizi, na walipoona ninawakaribia wakautupa chini mkoba, nikauchukua na kumrejeshea abiria kule  nilikomuacha baada ya kuachana na wezi hao.”
Na kuhusu kisa cha kuachana na udereva bodaboda, anasema kuwa, siku moja saa nane za usiku, alimpakia abiria mwanamke na hakujua kuwa yule alikuwa ni sehemu  ya majambazi, “ilikuwa ni ile njia ya kutoka Ilemela Mahakamani kuja njia  ya lami, tulipokaribia sehemu yenye miti isiyo na watu wengi, yule abiria alianza kujichezesha nyuma ili  nipunguze mwendo ama kuanguka, na kwa mbele nikaona kundi la vijana wakiwa na nondo na mapanga.
“Nilipoona hivyo, nikaendesha pikipiki kuwafuata waliko ili niwagonge, wakatawanyika na kujiweka mbali  walipoona hivyo, nikashuka na kumg’amg’amia yule mwanamke kwenye pikipiki,huku nikimpiga na kumgeuza kinga endapo wangenishambulia;
“Waligundua manbo ni magumu, wakakimbia na nikabaki na yule abiria feki, nikamwambia alete hela yangu, akabisha, nikamsachi na kumkuta ana shilingi 15,000/= nikamnyang’anya, nikamwambia ondoka naye akatimka kama hana akili sawa sawa.  Na huo ndio mwisho wangu na bodaboda,” anasimulia Mihaye.
Kalima yeye anasema kwamba kwa siku hizi mambo mengi yamebadilika, uhasama wa wenye magari au madereva wa daladala na waendesha bodaboda kitu ambacho kilikuwa chanzo cha ajali nyingi, umepungua baada ya kila upande kuuheshimu mwingine.  Pia uelewa wa sheria miongoni mwa madereva wa bodboda kumeondoa pia ile tabia ya wao kufukuzana na askari wa usalama barabarani.
“Nimeshuhudia vifo vya madereva boda boda sita ama saba hivi kutokana na ajali zilizo katika mazingira haya tangu nianze kuendesha bodaboda mwaka 2010,” anasimulia Kalima ambaye kabla ya kujinunulia pikipiki yake alifanya kazi ya ajira Halmashauri ya Jiji la Mwanza kama mhudumu, na baadaye hotelini, na hivyo kujipatia fedha kwa ajili hiyo.
“Hata hivyo siku moja mwaka 2015,  nikiwa naendesha pikipiki kuelekea mjini kutoka Airport na abiria wangu akiwa dereva bodaboda mwenzagu, na wakati trafiki wameyazuia magari ya  upande mmoja wa barabara, [wakati huo barabara ya Aiport haijawa na njia mbili] ili kuruhusu basi la timu ya Mbao iliyokuwa ikifanya mazoeazi katika viwanja vya DIT hapa Mwanza, kuingia barabara kuu ili waelekee upande wa kulia kwetu,  lilikuja gari moja likiwa na mwendo mkali.
Gari hilo ni kama lilikataa amri ya trafiki na kuingia upande wetu ulioruhusiwa,  na hivyo kukutana uso kwa uso na sisi  na kutugonga. Ilikuwa ajali mbaya sana. Tulipakiwa katika magari mawili tofauti, mwenzangu akapelekwa Sekou Toure na mimi nikapelekwa Bugando [hospuali] na huko, baada ya kulazwa kama mwezi mzima wakanikata mguu,” anasimulia Kalima, na kuongeza kuwa, “ Baada ya kukatwa mguu, nilikaa siku tatu bila fahamu, baadaye nilijitambua na kujiona mwenye afya na nikawa nakula chakula kama kawaida.
Nilishtuka  baada ya kuona kama kuna wepesi usio wa kawaida kwenye mguu wa kulia, na ndipo nilpotambua kuwa umekatwa. Nilisikitika sana, wakanipa moyo kuwa, utaota na kurejea hali ya kawaida, na nikayaamini haya maneno.”
Anasema aliielewa hali hiyo baadaye na kuendelea kuisha nayo.  Ila kwa sasa anawaomba wasamaria wema kama wanaweza kusaidia  fedha za kupata mguu bandia ili maisha yake yaendee kawaaida. Anapatikana kwa namba  0786858676, mwenye kuwiwa kumsaidia anaweza kuwasiliana nae. Kwa naelezo ya awali anadai mguu bandia  unaweza kugharimu kati ya shilingi milioni mbili hadi tatu.

DAR ES SALAAM

Na Arone Mpanduka

Dunia kwa sasa ipo kwenye kipindi cha mfungo kwa Dini zote mbili, ambapo Wakristu wapo kwenye Kwaresma, na Waislamu wapo kwenye Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.
Mfungo huo hasa kwa upande wa chakula, umekuwa na tofauti kwa Dini hizo ambapo Wakristu wanaweza kula kidogo mara tatu kwa siku bila kushiba, huku Waislamu wakila mara moja kwa kutwa hasa majira ya jioni. Kwa wanamichezo walio kwenye Ramadhan ufanisi wao uwajani ndiyo huwa na changamoto kidogo.
Wataalamu wa soka nchini Algeria waliwahi kufanya utafiti miaka 20 iliyopita, hasa kwa kuwatumia wachezaji waliofunga katika kipindi kama hiki.
Timu mbili za soka za kitaaluma za Algeria (wanaume 55) zilifanyiwa utafiti. Majaribio ya uwanjani ya uchezaji wa kimwili na soka yalikusanywa kabla ya mfungo wa Ramadhan, mwishoni wa mwezi wa Ramadhan na wiki mbilibaada ya Ramadhani. Wachezaji waliulizwa kuhusu tabia za kulala namtazamo binafsi wa mazoezi na uchezaji wa mechi.
Utendaji ulipungua kwa kiasi kikubwa kwa kasi yao uwanjani, wepesi, kukimbia na mpira, na nyingi zilibaki chini baada ya kumalizika kwa Ramadhani. Takriban 70% ya wachezaji walidhani kuwa mazoezi na uchezaji wao uliathiriwa vibaya wakati wa mfungo.
Mabadiliko ya awamu ya ulaji wa chakula na usumbufu wa mifumo ya kulala huathiri utendaji halisi wa kimwili na unaozingatiwa. Wachezajiwa Kiislamu wanahitaji kuchunguza mikakati ambayo itaongeza utendaji wakati wa Ramadhani.
Athari za kisaikolojia na kiafya za Ramadhani kwenye majibu ya homoni, kimetaboliki na tabia zimekuwa lengo la utafiti. Data chache kuhusu utendaji wa kimwili zinaonyesha kwamba vipengele vya chini zaidi (yaani mapigo ya moyo) huathirika kidogo ilhali kazi kubwa zaidi hupungua. Kwa sababu soka inashindaniwa kimataifa na mechi zinaendelea kupangwa wakati wa Ramadhani, lengo lilikuwa kujifunza jinsi Ramadhani inavyoathiri utendaji wa ushindani kwa wachezaji wa soka.
Utafiti huo ulifanyika Algeria mwaka 2004 wakati mwezi wa Ramadhani ulipoanza kati ya Oktoba 15 na Novemba 13 mwaka huo. Timu mbili za wataalamu zilikubali kushiriki katika mradi huo.Jumla ya wachezaji walioshiriki katika utafiti huo walikuwa 55.Kamati ya maadili ya jimbo la Algiers iliidhinisha itifaki hiyo. Wachezaji wote walitoa idhini yao iliyotiwa saini, iliyoarifiwa kabla ya kushiriki katika mradi.
Wachezajiwalijaribiwa  wiki mbili kabla ya kuanza kwa Ramadhani, katika wiki ya mwisho ya Ramadhani na wiki mbili baada ya kumalizika kwa Ramadhani. Wachezaji walihojiwa kila siku wakati wa mfungo na mmoja wa wataalamu wawili waliofunzwa kuhusu mambo ya kimwili na ya kihisia.
Data inayoendelea ilifupishwa kwa takwimu za kawaida za maelezo. Mabadiliko ya muda yalibainishwa na uchanganuzi wa kurudiarudiwa wa tofauti (marekebisho ya Geisser-Greenhouse) na utaratibu wa ufuatiliaji wa kutumia programu ya takwimu ya SAS JMP (Cary, North Carolina, Marekani). Data ya kawaida kutoka kwa mahojiano ilifupishwa kwa masafa.
Kati ya wachezaji 55 wa awali, kulikuwa na data kamili kuhusu watu 48 waliokuwa na majeraha au ugonjwa. Wachezaji walikuwa na wastani wa kilo 72.6, urefu wa futi 6.1  na walikuwa na umri wa miaka kati ya 17 hadi 34 . Uzito haukubadilika wakati wa mradi huo.
Katika wiki ya nne ya Ramadhani, ufaulu ulipunguzwa kwenye majaribio mbalimbali (kasi ya mita 20, uchezaji wa kasi, wepesi na ustahimilivu ) na ulikuwa chini ya viwango vya awali ulipojaribiwa wiki 2 baada ya kumalizika kwa kipindi cha mfungo.
Uwezo wa kustahimili ulipunguzwa kwa karibu 20% mwishoni mwa Ramadhani na karibu nusu ya punguzo lilipatikana tena katika wiki 2 baada ya mfungo. Viwango vya mapigo ya moyo vya mara baada ya kukimbia viliongezeka kwa karibu sambamba na kupunguzwa kwa uvumilivu, hata hivyo, ingawa umbali wa kukimbia uliongezeka katika wiki 2  baada ya mfungo, mapigo ya moyo baada ya kukimbia hayakubadilika sana.

DAR ES SALAAM

Na Arone Mpanduka

Bendi ya Urafiki ilianzishwa mwaka 1970 na kiwanda cha nguo cha Urafiki ambacho kilikuwa ni kiwanda cha Umma kwa wakati huo. Kiwanda kilijengwa kwa msaada wa watu wa Jamhuri ya China.
Azma ya kuanzishwa bendi katika kiwanda hicho ilitokana na umuhimu wa kutangaza bidhaa zake ambazo zilikuwa ni Khanga na Vitenge, na hasa ikizingatiwa ushindani uliokuwepo wakati huo Tanzania, kulikuwa na viwanda vingi vilivyotengeneza bidhaa hizo.
Meneja Mkuu wa kiwanda cha Nguo cha Urafiki kwa wakati huo, Joseph Rwegasira aliubariki mpango huo wa kuanzishwa bendi ya dansi ya kiwanda na hivyo aliidhinisha malipo ya hundi ya shilingi 50,000/=   kununulia seti ya vyombo vya muziki katika duka la Dar es Salaam Music House, mtaa wa Samora Avenue.
Ili kupata kundi lililo bora, Menejimenti ya kiwanda cha nguo cha Urafiki ilimuajiri Juma Mrisho Feruzi, maarufu kama Ngulimba Wa Ngulimba, na kumuagiza atafute wapigaji kutoka popote ili kuunda kundi imara. Katika kuhakikisha bendi hiyo mpya inasimama barabara, Ngulimba alichukua wapigaji watano kutoka Orchestre Qwillado, bendi ambayo aliipigia kabla ya kuanza Urafiki. Na hii ndio maana nyimbo za mwanzoni za bendi ya Urafiki zilionekana kama zina mahadhi ya Orch. Qwillado.
Wanamuziki aliowachukua Ngulimba kutoka Orch. Qwillado walikuwa ni Maiko Vincent Semgumi, mpiga gitaa la Solo, Ayoub Iddi Dhahabu ,Besi, Abassi Saidi Nyanga (Tenor Saxophone) na Fida Saidi(Alto Saxophone). Ngulimba yeye akiwa mwimbaji na pia kiongozi wa bendi ya Urafiki.
Wanamuziki wengine wa mwanzoni ambao waliungana na hao watano waliotoka Orch. Qwillado  ambao tayari walikwisha ajiriwa kiwandani Urafiki, walikuwa Juma Ramadhani Lidenge(Second Solo), Mohamed Bakari Chachil(gitaa la kati), Ezekiel Mazanda(rhythm), Abassi Lulela(Besi), Hamisi Nguru(Mwimbaji), Mussa Kitumbo(Mwimbaji), Cleaver Ulanda(Mwimbaji), Maarifa Ramadhani(Tumba), Juma Saidi (Manyanga) na Hamisi Mashala(Drummer Boy).
Mtindo walioanza nao Urafiki ulijulikana ‘Mchaka Mchaka’ na baadae ukabadilika na kuwa ‘Chaka Chua’ na hatimae mwisho bendi inaelekea ukingoni walipiga mtindo wa ‘Pasua’ na ‘Patashika’
Mwaka 1971 Gidion Banda, mwanamuziki kutoka bendi ya Morogoro Jazz alijiunga nabendi ya Urafiki, yeye alikuwa mpulizaji ala ya upepo, Saxophone.
Bendi ya Urafiki ikiwa katika hali yake ya uchanga mwaka 1970 ilipata ajali ya gari, iligonga mti maeneo kona ya Kigogo na Msimbazi Mission wakati dereva akiwa katika spidi  kali. Walikuwa wakitokea kwenye onyesho la usiku lililofanyika Ukumbi wa Chang’ombe, Temeke.
Baadhi ya wanamuziki waliumia sana na gari lao, ‘VW Comby’ ilikuwa halifai kabisa.
Wapigaji walioumia walikuwa ni Hamisi Mashala Drummer Boy alivunjika mguu, Mohamed Bakari Chachil aliumia kichwani na kupata ‘stich’ na pia Ayoub Iddi Dhahabu na Maarifa Ramadhani walipata maumivu makali kwa ndani mwilini.
Bendi ilisimamisha maonyesho yake kwa muda hadi wasanii wake walipopata nafuu na kuanza maonyesho tena. Hali ya ajali ile ilileta fikra mbaya kwa wasanii wa Urafiki na wapenzi wao na ilionekana kana kwamba kulikuwa na mkono wa mtu katika ajali ile ambapo hakuwatakia mema wanamuziki wa Urafiki. Juma Mrisho ‘Ngulimba’ alitunga wimbo ‘Nimekosa Nini Jama’, wimbo ulioelezea kadhia hiyo.
Aidha, Bendi ya Urafiki ilipitiwa na wanamuziki wengi, baadhi wakiwa ni Thobias Cosmas Chidumule na Frank Mahulu. Waimbaji waliotokea Western Jazz (Saboso) mwaka 1973 na kuongeza nguvu katika safu ya uimbaji.  Waimbaji hao walishiriki nyimbo nyingi baadhi zikiwa Tausi Karuka, Jembe na Panga (Geza Ulole), Kosa la Nani, Mauaji ya Soweto, Rukia Hukusikia, Maonyesho ya Mtu Mweusi n.k.
Pia katika safu ya upulizaji  na magitaa waliongezeka Mkali na Hidaya kutoka Morogoro wakipuliza matarumbeta. Hao walikuja mwaka 1973 na Ali Saidi aliyetokea Cuban Marimba akipiga gitaa la kati (rhythm) na baadae mwaka 1975, Mganga Hemedi kutoka Tanga, akitokea Atomic Jazz, nae alijiunga na kuwa upande wa solo na rhythm.
Bendi ya Urafiki imetunga nyimbo nyingi, zaidi ya mia tatu zinazoelekeza kwenye siasa, mapenzi, nasaha na mafundisho na pia kukosoa. Baadhi ya nyimbo zake za siasa zilizopata umaarufu ni kama zile Mwenyekiti Nyerere, Mauaji ya Soweto, Jembe na Panga n.k.
Tungo au nyimbo zao zimesaidia kuhamasisha  ukombozi  wa Bara la Afrika na kutoa muelekeo wa sera za nchi kama vile Kilimo cha kufa na kupona na uhamasishaji wa kuhamia vijijini. Nyimbo hizo zimetoa mchango mkubwa sana katika siasa za Tanzania.
Mwaka 1975 Bendi ya Urafiki ilishiriki katika mashindano ya bendi za muziki wa dansi yaliyofanyika Mnazi Mmoja Dar es Salaam na bendi ya Urafiki ilishika nafasi ya tatu na Mzee Ngulimba, kama kiongozi wa Bendi ya Urafiki aliiwakilisha Tanzania pamoja na bendi ya Afro 70 iliyopata nafasi ya kwanza na baadhi ya vikundi vya utamaduni kutoka Tanzania Bara na Zanzibar nchini Nigeria katika maonyesho ya mtu mweusi yaliyofanyika huko.
Kufikia katikati ya miaka ya 1980, bendi ya Urafiki ikawa inasuasua kutokana na uchakavu wa vyombo na Menejimenti iliyokuwepo wakati huo haikuwa tayari kutoa pesa kununulia vyombo vipya.Na huo ndiyo ukawa mwisho wake kwa kufa taratibu.

BUJUMBURA, Burundi
Ushiriki wa klabu ya Dynamo ya Burundi katika Ligi ya Mpira wa Kikapu Afrika, umefikia ukomo baada ya kukataa kuvaa jezi yenye nembo ya ‘Visit Rwanda’.
Timu hiyo ilifunika ujumbe huo katika mchezo wao wa ufunguzi katika Kongamano la Kalahari mjini Pretoria, lakini wakapoteza mechi zao mbili zilizofuata.
Hayo yanakuja huku kukiwa na mvutano wa kisiasa kati ya nchi hizo mbili.
Burundi ilifunga mipaka yake na Rwanda mwezi Januari baada ya kumtuhumu jirani yake kufadhili mashambulizi ya waasi.
Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye alidai serikali ya Rwanda inayoongozwa na Paul Kagame inaunga mkono kundi la waasi la Red Tabara baada ya shambulio la wanamgambo hao kuwaua watu 20 mwezi Disemba.
Rais Kagame anakanusha shtaka hilo, lakini serikali ya Burundi imemtaja kuwa “jirani mbaya”.
Rais wa Ligi ya Mpira wa Kikapu Afrika (BAL) Amadou Gallo Fall alisema kuwa ligi hiyo haikuwa na budi, ila kuifukuza klabu hiyo kwa kukataa kufuata kanuni za ligi hiyo zinazosimamia mahitaji ya jezi na sare.

DUBAI, Saudia
Mshauri wa timu ya mbio za magari ya Red Bull, Helmut Marko amesema kuwa atasalia na timu hiyo kufuatia mazungumzo na Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo Oliver Mintzlaff.
Marko alikabiliwa na uchunguzi wa ndani huku kukiwa na mzozo karibu na bosi wa timu Christian Horner.
Aliambia Sky Germany: “Tulikubaliana kwa pointi zote. Nitaendelea hapa.Mkataba wangu bado una miaka mitatu kumalizika.”
Marko alimshukuru Max Verstappen kwa msaada wake katika suala hilo.
Bingwa huyo mara tatu wa dunia alikuwa amesema siku ya Ijumaa baada ya kufuzu kwenye mashindano ya Saudi Arabian Grand Prix kwamba Marko “lazima abaki”.
Alikaribia kutishia kuondoka Red Bull ikiwa sivyo, akisema, “Ikiwa nguzo muhimu kama hiyo itaanguka, hiyo sio nzuri kwa hali yangu pia.”
“Uaminifu wangu kwa [Marko] ni mkubwa sana. Daima nimekuwa nikieleza hili kwa kila mtu ndani ya timu, kila mtu aliye juu, kwamba yeye ni sehemu muhimu katika kufanya maamuzi yangu kwa wakati wote katika siku zijazo pia ndani ya timu. “