Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

DUBAI, Saudia
Mshauri wa timu ya mbio za magari ya Red Bull, Helmut Marko amesema kuwa atasalia na timu hiyo kufuatia mazungumzo na Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo Oliver Mintzlaff.
Marko alikabiliwa na uchunguzi wa ndani huku kukiwa na mzozo karibu na bosi wa timu Christian Horner.
Aliambia Sky Germany: “Tulikubaliana kwa pointi zote. Nitaendelea hapa.Mkataba wangu bado una miaka mitatu kumalizika.”
Marko alimshukuru Max Verstappen kwa msaada wake katika suala hilo.
Bingwa huyo mara tatu wa dunia alikuwa amesema siku ya Ijumaa baada ya kufuzu kwenye mashindano ya Saudi Arabian Grand Prix kwamba Marko “lazima abaki”.
Alikaribia kutishia kuondoka Red Bull ikiwa sivyo, akisema, “Ikiwa nguzo muhimu kama hiyo itaanguka, hiyo sio nzuri kwa hali yangu pia.”
“Uaminifu wangu kwa [Marko] ni mkubwa sana. Daima nimekuwa nikieleza hili kwa kila mtu ndani ya timu, kila mtu aliye juu, kwamba yeye ni sehemu muhimu katika kufanya maamuzi yangu kwa wakati wote katika siku zijazo pia ndani ya timu. “

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Uwanja wa gofu uliopo Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, upo mbioni kukarabatiwa ili uwe na hadhi ya Kimataifa.
Akizungumza na Tumaini Letu, Afisa Michezo wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Charles Maguzu alisema kuwa mchakato huo umetokana na agizo lililotolewa na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Damas Ndumbaro aliyetaka uwanja huo kufanyiwa matengenezo.
Alisema kuwa agizo hilo linataka BMT kuhakikisha wanashirikiana na Chama cha Gofu nchini (TGU) katika kuhakikisha uwanja huo unafanyiwa maboresho na kuwa kwenye hadhi ya kimataifa.
Alisema kuwa Waziri Ndumbaro aliona kwamba uwanja huo umewaelemea TGU, hivyo wanahitaji msaada wa usimamizi ili uendelee kuwa bora na kuwasaidia watu wa ukanda huo kuutumia.

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Siku chache baadaya kuchezeshwa kwa droo ya Robo Fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, washabiki mbalimbali wa timu ya Yanga wameibukia kwenye mtandao wa kijamii wa klabu ya Mamelody Sundowns ya Afrika Kusini na kuipiga mikwara.
Machi 12 mwaka huu, Yanga ilipangwa kucheza na mabingwa hao wa Ligi ya Afrika Kusini katika hatua ya Robo Fainali ya michuano hiyo, huku watani zao Simba wakiangukia mikononi mwa Al Ahly ya nchini Misri.
Kupitia ukurasa wa kijamii wa Instagram wa Mamelodi Sundowns ujulikanao kama Sundowns FC, washabiki hao wamefurika kwenye eneo la maoni (comments) na kuitisha miamba hiyo ya Afrika Kusini kwa maneno ya kejeli.
Katika maoni hayo wapo mashabiki walioonyesha kuwakaribisha Tanzania, na wapo ambao waliwatisha kwa kutaja majina ya nyota wao kama vile Aziz Ki, Max Nzengeli, Mudathir Yahya na wengineo.
Washabiki hao waliibuka hasa baada ya Mamelodi kuweka picha katika mtandao huo inayoonyesha kwamba watakutana na Yanga katika hatua hiyo ya Robo Fainali.
“Masandawana out” aliandika shabiki mmoja wa Yanga aitwaye Chollo Chalile, akimaanisha Mamelodi itatupwa nje ya mashindano hayo. Masandawana ni neno la utani la timu hiyo.
Shabiki mwingine aitwaye Amani Eliji, aliandika, “Mnajua kitu kinachoitwa 5G?”
Mikwara hiyo pia imekuwa ikiendelea kutolewa hata pale klabu hiyo ilipochapisha vitu ambavyo havihusiani na mechi yao dhidi ya Yanga, mfano pale walipoweka chapisho la kuwapongeza baadhi ya wachezaji wao walioitwa kwenye timu ya taifa, bado washabiki wa Yanga waliwajia juu na kuwatambia.
Mara ya mwisho timu hizo zilikutana kwenye hatua za awali za michuano ya CAF mwaka 2001 ambapo mchezo wa kwanza Yanga ilifungwa 3-2 ugenini na kisha kulazimishwa sare ya 3-3 nyumbani.
Mchezo wa nyumbani ulichezwa kwenye uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Timu hizo zitakutana tena, huku mambo mengi yakiwa yamebadilika kwenye soka ikiwemo muundo wa uongozi na wachezaji wa timu zote mbili.

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Miaka ya Utume wa Uaskofu inatajwa kuwa ni Baraka na huruma ya Mungu, kwani ni kuteuliwa na Kristo, na si kwa mastahili ya mtu binafsi.
Hayo yalisemwa hivi karibuni na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi, wakati akizungumzia kuhusu Jubilei ya Miaka 25 ya Uaskofu wake inayotarajiwa kuadhimishwa Mei mwaka huu.
“Kuhusu Miaka 25 ya Uaskofu wangu, naitazama kama ni miaka ya baraka na huruma ya Mungu, kwa sababu siyo kwa mastahili yangu, bali ni kwa kuteuliwa na Kristo Mwenyewe,” alisema Askofu Ruwa’ichi.
Aidha, Askofu Ruwa’ichi alisema kuwa kila Askofu anapowekwa mahali, anawekwa ili kukita mizizi ya kuliimarisha Kanisa, pamoja na Waamini wake.
Wakati huo huo aliongeza kuwa licha ya kwamba katika kipindi cha Uaskofu wake amehudumu katika Majimbo matano tofauti, bali alitii kila uhamisho wake, kwani hali hiyo ilimjenga kuwa imara katika Uchungaji wake, huku akishukuru mapokezi ya kila Jimbo alikotumwa.
Alisema kwamba wazazi wake walipomwita jina Ruwa’ichi, yaani ‘Mungu anajua’, yeye hakufahamu walimaanisha nini, bali limekuwa jina lenye baraka kwake.
Katika mazungumzo yake, Askofu Mkuu Ruwa’ichi alisema kuwa kazi alizozifanya kwenye Shirika lake akiwa kama Mkuu wa Shirika hilo, zimemwonyesha namna anavyoweza kuwa Mchungaji.
Akizungumzia kuhusu vijana, Askofu Ruwa’ichi alisema kuwa Kanisa nchini Tanzania lina utajiri mkubwa wa vijana, ila lina kazi kubwa ya kuendelea kuwajenga katika imani thabiti.
Aidha, alisema kuwa katika Majimbo yote aliyowahi kuhudumu kama Askofu, kumekuwa na changamoto tofauti tofauti kutokana na mazingira yaliyopo
Aliongeza kuwa alijitahidi kukabiliana na kila changamoto zilizokuwepo, bila kuwapendelea Waamini wala kuwakimbiza, yaani kuwapelekesha.
Akizungumzia juu ya familia yao, Askofu Ruwa’ichi alisema kuwa wamezaliwa watoto tisa, ambapo yeye ni wa kwanza, akiongeza kwamba licha ya familia yao kutokuwa ya kitajiri, bali walilelewa na kusomeshwa vizuri.
Askofu Mkuu alitumia nafasi hiyo kutoa pole kwa Askofu wa Zanzibar pamoja na Kanisa Visiwani humo kutokana na mtu mmoja ambaye aliingia kanisani na kufanya uharibifu, ukiwemo wa vitu vitakatifu.
Alisema kwamba ana imani kuwa vyombo vinavyohusika vitachukua hatua juu ya hilo, pamoja na kulikomesha, kwani kufanya hivyo ni tabia ya kutokuziheshimu imani za wengine.

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Paroko wa Parokia ya Roho Mtakatifu – Segerea, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Padri Denis Kunambi amewataka Wakristo kutumia kipindi cha Kwaresma kutengeneza vyema uhusiano kati yao na Mungu.
Padri Kunambi alisema hayo wakati wa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Kupokelewa na Kuteuliwa kwa Wakatekumeni 37, iliyoadhimishwa parokiani hapo.
“Tumieni kipindi hiki cha Kwaresma kuanza upya na kutengeneza vyema uhusiano yenu na Mungu. Licha ya kwamba hizi siku 40 ni zenye changamoto kubwa, lakini kumbukeni kwamba hata Kristo alijaribiwa,” alisema Padri huyo.
Aliongeza kuwa nguvu ya Mungu ni kubwa katika maisha ya Wakristo, huku akiwasihi kufahamu kwamba adui shetani hawezi kuishinda nguvu hiyo.
Padri Kunambi alisema kuwa kipindi cha Kwaresma ni cha kujichotea neema na baraka, kwani Mama Kanisa anamwezesha kila mmoja kuipokea neema hiyo.
“Ndugu zangu, kipindi hiki cha Kwaresma ni cha kujichotea neema na baraka, kwa sababu Mama Kanisa anamwezesha kila mmoja kuipokea neema na baraka hiyo katika maisha yake…
“Hiki ni kipindi cha kulitafakari Neno la Mungu, hasa katika nguzo kuu tatu, ambazo ni sala, kufunga, pamoja na majitoleo,” alisema Padri Kunambi.
Aliwasisitiza Waamini kutokuwa wazembe wa kuikimbilia Sakramenti ya kitubio, huku wakijitafakari na kuona kwamba nini kinachowasababisha kutokuikimbilia Sakramenti hiyo.
Padri Kunambi aliwataka kutafakari na kuondoa vizuizi vinavyowafanya washindwe kupokea matakatifu, ili waweze kubadilika.
Wakati huo huo aliwataka Wakatekumeni hao kuwa waaminifu, huku wakiwa tayari kumshuhudia Kristo siku zote za maisha yao.

DAR ES SALAAM

Na Devotha Mwang’ata

Taasisi ya Taifa ya Tafiti za Magonjwa ya Binadamu (NIMR) kwa kushirikiana na Wizara ya Afya inatatarajia kuanza kufanya utafiti wa magonjwa yasiyoambukiza kwa njia ya simu ili kuwafikia wananchi wengi.
Njia hiyo itasaidia kuwafikia Watanzania wengi kwa muda mfupi na kuokoa gharama.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mkuu wa NIMR Profesa Said Aboud alisema NIMR imechagua njia hiyo ili kuwafikia watu wengi kwa muda mfupi na kwamba suala hilo linawezekana kutokana matumizi ya simu kuwa makubwa nchini.
“Kutokana na ongezeko kubwa la matumizi ya simu za mkononi, NIMR tumeona ni wakati muafaka kutumia simu za mkononi katika ukusanyaji na uchakataji wa takwimu, kwani itakuwa njia rahisi sana na itaweza kukabiliana na vizuizi vya muda mrefu katika ukusanyaji wa takwimu na ufuatiliaji, hii itasaidia upatikanaji wa taarifa muhimu kwa wakati,”alisema Aboud.
Mpango huo utasaidia kufanya tafiti kwa ufanisi wa matumizi ya simu za mkononi kwenye kukusanya taarifa za tafiti nchi nzima na kutuwezesha kuishauri serikali kama matumizi ya tecknolojia yanawezesha upatikanaji wa taarifa sahihi.
Alisema kuwa lengo la kuzungumza na wanahabari ni kuufahamisha umma juu ya kuwepo kwa utafiti huo utakaowashirikisha wanachi moja kwa moja.
Aboud alisema kuwa utafiti huo utajumuisha sampuli ya wananchi wenye umri kati ya miaka 18 na kuendelea na utafanyika Tanzania Bara pamoja na Zanzibar na unategemea kuchukua wiki nne hadi sita.
Kwa upande wake, Dk. Mery Maige Mtafiti kiongozi wa Magonjwa yasiyo ya kuambukiza pia Mtafiti Mkuu Mwandamizi na Mkurugenzi wa Taarifa za Utafiti Taasis ya Utafiti ya Magonjwa ya Binaadamu NIMR amesema kuwa lengo la utafiti huo ni kuangalia hali ya Magonjwa yasiyoambukiza na viashiria vyake kwa njia ya simu .
Aliongeza kwamba utafiti huo utakaokuwa unaangalia viashiria vya magonjwa unatakiwa kufanywa mara kwa mara ili kubaini na mabadiliko ya mwenendo wa maisha unavyoathiri afya za watu.
“Kwa kuangalia hilo tumeona kuwa hatuwezi kufanya tafiti za nyumba kwa nyumba kwa sababu ya gharama na muda na changamoto ya kuwafikia wananchi wengi hivyo kutumia njia ya simu ni nyenzo muhimu ya kufanya utafiti mara kwa kwa mara,” alisema Dk. Maige.
Alisema kuwa ili kudhibiti wahalifu wa mtandaoni watu wataofanyiwa utafiti watatumiwa meseji maalum itakayowafahamisha juu ya kufanyiwa utafiti ili kuepushwa kupigiwa na matapeli.
Takwimu ya Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonesha kuwa magonjwa yasiyoambukiza yaliongezeka mara mbili kutoka asilimia 19 mwaka 1990 hadi asilimia 34 mwaka 2015 na yanakadiriwa kuchangia asilimia 33 ya vifo vyote.
Nchini Tanzania katika kipindi cha Julai 2022 hadi Machi 2023, magonjwa yasiyoambukiza ambayo yamesababisha wagonjwa wengi kuhudhuria vituo vya huduma za Afya ni pamoja na shinikizo la juu la damu wagonjwa 1,456,881 sawa na asilimia 49 ikilinganishwa na asilimia 34 kipindi kama hicho mwaka 2021/22, kisukari wagonjwa 713,057 sawa na asilimia 24 na magonjwa ya mfumo wa hewa 386,018 sawa na asilimia 13 ikilinganishwa na asilimia 10 kwa kipindi kama hicho mwaka 2021/22.

DAR ES SALAAM

Na Mathayo Kijazi

Mchakato wa Bagamoyo kuwa Jimbo Katoliki, bado unaendelea huku ikielezwa kwamba katika Kanisa Katoliki, hakuna Jimbo linalotokea bila kuwa na mradi, yaani (project), kuhusu kuanzishwa kwa Jimbo husika.
Ufafanuzi huo ulitolewa hivi karibuni na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi wakati akizungumza na gazeti Tumaini Letu katika mahojiano kuhusu Jubilei ya Miaka 25 ya Uaskofu wake, inayotarajiwa kuadhimishwa Mei mwaka huu.
Katika mahojiano hayo, Askofu Ruwai’cihi alizungumzia Mchakato wa Bagamoyo kuwa Jimbo, ambapo alisema kuwa Jimbo Katoliki la Morogoro ndilo Jimbo Mama litakalozaa Jimbo tarajiwa la Bagamoyo, bado linaendelea na mchakato huo.
“Kwanza ifahamike kuwa hakuna Jimbo linalokuwepo bila ‘project’, kwani ni lazima kuwepo na ‘project’. Kama tunavyofahamu kwamba Jimbo Katoliki la Morogoro ndilo Jimbo mama, hadi sasa bado linaendelea na ufuatiliaji juu ya mchakato huo,” alisema Askofu Mkuu Ruwa’ichi.
Mchakato wa eneo kuwa Jimbo Katoliki
Kwa mujibu wa Askofu Mkuu Ruwa’ichi, Mchakato wa Bagamoyo kuwa Jimbo, suala la mahali kupewa hadhi ya kuwa Jimbo, haliendi kiholela, bali kuna majukumu ambayo yanapaswa kutekelezwa, ikiwemo kukusanya taarifa za kutosha kuhusu eneo hilo.
“Kwanza ni kweli kwamba kuna shauku ya Bagamoyo kupewa hadhi ya kuwa Jimbo, hii shauku imekuwepo kwa muda mrefu, na wengi walitegemea kwamba tulipoadhimisha Miaka 150 ya Kanisa Katoliki Tanzania kule Bagamoyo, kuwa ingetangazwa, na wengi walilichukulia kwa urahisi sana,” alisema Askofu Mkuu, na kuongeza;
“…Jukumu la kwanza ni kukusanya taarifa ambazo zinabainisha mambo kadhaa, na kwa nini hilo eneo linafikiriwa lipewe hadhi ya kuwa Jimbo.”
Miongoni mwa mambo yanayoangaliwa ili eneo lipewe hadhi ya kuwa Jimbo, kadri ya Askofu Mkuu Ruwa’ichi ni pamoja na idadi ya Waamini waliopo, kuzifahamu tamaduni zinazotawala katika eneo hilo, na pia kuufahamu uchumi utakaosaidia kuliendesha Jimbo hilo.
Aliongeza pia kuwa kabla ya eneo kupewa hadhi hiyo, ni lazima kwanza ifahamike kwamba watendakazi wa Jimbo hilo wakiwemo Mapadri, Watawa, na Makatekista, ni wangapi na watatoka wapi.
Kufuatia shauku hiyo, Askofu Ruwa’ichi aliwasihi Wakristo kufahamu kuwa licha ya kwamba Jimbo tarajiwa la Bagamoyo litazaliwa kutokana na kumegwa kutoka Jimbo Katoliki la Morogoro, bali pia Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam litachangia baadhi ya Parokia zitakazounda Jimbo la Bagamoyo.
“Lakini ikumbukwe kuwa mzazi wa Jimbo hilo, siyo Dar es Salaam, bali ni Morogoro. Pamoja na hilo, lakini mwenye uzito hapa, kwa kweli ni Dar es Salaam. Na hili suala la minong’ono lililotawala kwa kipindi mpaka mwaka ule wa 2018, niseme tu wazi kwamba lilibaki minong’ono, halikuwa limewekwa kwenye karatasi. Ni lazima ‘data’ zikusanywe, ziwekwe vizuri, halafu zipelekwe Roma,” alisema Askofu Mkuu.
Alisema kuwa andiko la kwanza lilifanyika mwaka 2019, na baada ya hapo likatumwa kwenda Roma, na hivyo Roma ikarudisha ujumbe kwa kuuliza maswali ya nyongeza, ambayo yalilengwa kwa Jimbo Katoliki la Morogoro, pamoja na Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.
“Tumejipanga, tumezungumza mimi na Askofu wa Jimbo Katoliki la Morogoro, tukaafiki kwamba yale maswali, majibu yake yatakuwaje. Kwa kifupi maswali yalikuwa kama haya, ‘je, mnapoomba lizaliwe Jimbo la Bagamoyo kutoka Jimbo la Morogoro, mnalirithisha nini Jimbo la Bagamoyo? Ni vitu gani ambavyo mnalirithisha Jimbo lianze maisha navyo? Na Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam pia likaulizwa, je ni vitu gani ambavyo mtalirithisha Jimbo ambalo nyie mtakuwa wazazi wenza?” alisema Askofu Mkuu.
Askofu Mkuu alisema kuwa moja ya vitu ambavyo Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam limefanya, ni kwamba tayari limeshajenga nyumba ya Askofu katika Jimbo hilo tarajiwa la Bagamoyo, ambayo imegharimu zaidi ya Shilingi milioni 600.
Aliongeza pia kuwa bado kuna uhitaji wa kujenga nyumba ya Watawa watakaoihudumia nyumba ya Askofu, Ofisi za Askofu au Ofisi za Jimbo, ambazo bado hazijajengwa, akisema kuwa katika harakati za kuifanya Bagamoyo kuwa Jimbo, ni lazima kwanza mambo hayo yafanyiwe kazi.
Maeneo yanayotarajiwa kuunda Jimbo Katoliki la Bagamoyo:
Hapo awali alipozungumzia kuhusu maeneo yatakayomegwa ili kuifanya Bagamoyo kuwa Jimbo Katoliki, Askofu Mkuu alisema kwamba wamependekeza kuwa Wilaya ya Chalinze, Wilaya ya Bagamoyo, pamoja na sehemu ya Wilaya ya Kinondoni ni miongoni mwa maeneo yanayotarajiwa kuunda Jimbo hilo Katoliki tarajiwa.
Aidha, Askofu Mkuu alisema kuwa kinachosubiriwa kwa sasa, ni majibu kutoka Roma, endapo Roma itaridhia Bagamoyo kupewa hadhi hiyo, hatua nyingine zitafuata ili kulipata Jimbo hilo jipya.
Athari Majimbo yatakayomegwa
Askofu Mkuu alibainisha kuwa hakuna athari kwa Majimbo mengine kumegwa, kwa sababu kuundwa kwa Jimbo lolote, kuna lengo la kuboresha huduma za Kichungaji kwa Waamini, hivyo hakuna Jimbo linaloumia pale huduma zinaposogezwa karibu zaidi na Waamini, badala yake ni faida kwa Majimbo yaliyokuwepo, na Jimbo linalozaliwa.
Aidha, Askofu Mkuu Ruwa’ichi aliwasihi Waamini kwa ujumla kuwa wajiweke vizuri kwa kupania kuuishi Ukristo, akiwasisitiza pia kwamba wawe ndani ya Jimbo Katoliki la Bagamoyo au nje ya Jimbo hilo, bali wawe ni Wakristo wanaotoa ushuhuda imara wa Kikristo.

DAR ES SALAAM

Na Mathayo Kijazi

Baadhi ya Wawakilishi wa Mpango wa Nia Njema wameomba kuwahishwa kupewa kadi zao za bima na kuongezewa hospitali za kwenda kutibiwa wanapopatwa na matatizo ya kiafya, kwani wanazoruhusiwa kwenda ni chache.
Waliyasema hayo wakati wakieleza changamoto zilizojitokeza tangu baada ya Semina Elekezi katika Mkutano wa Kazi wa Wasimamizi wa Mpango wa Nia Njema uliofanyika katika Viwanja vya Kituo cha Msimbazi, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.
Katika changamoto walizozitoa kwenye mkutano huo, waliomba pia kufanyiwa kazi kwa suala la baadhi ya magonjwa kutokutibiwa na kadi za bima hiyo, ili kuweza kumsaidia kila mgonjwa anayekwenda kufuata huduma.
Waliomba elimu na semina mbalimbali ziendelee kutolewa kwa wazee na wajane, ili nao waone kwamba Kanisa limewatambua.
Aidha, baadhi ya Wawakilishi wa mpango huo wa Nia Njema waliomba kupatiwa sare ili kujenga imani ya kusikilizwa pale wanapotoa elimu kwa wenigine.
Waliushauri Uongozi wa mpango huo, kuwaongezea timu ya Wawakilishi, ili kuongeza kasi ya uhamasishaji pamoja na utoaji wa elimu juu ya Nia Njema.
Miongoni mwa changangamoto walizobainisha Wawakilishi hao, ni pamoja na kutokupatiwa huduma kutokana na kutokupokelewa simu kwa wakati pale mtu anapohitaji huduma.
Wakati huo huo pia walipendekeza kutolewa mipaka suala la umri wa kupatiwa huduma hiyo, kwani kila rika lina haki ya kupatiwa matibabu pale mtu anapopatwa na magonjwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa ACCLAVIA, Nindiu Mpangile alisema kuwa ili kupunguza baadhi ya changamoto za kupatiwa matibabu, watahakikisha baadhi ya Hospitali za Wilaya ziingie katika mpango huo.
Nindiu alitumia nafasi hiyo kusema kwamba wao kama ofisi, wanaomba radhi kwa ucheleweshwaji wa kupata kadi, akisema kuwa watajitahidi kuongeza kasi ya utendaji ili watu wapatiwe kadi zao kwa wakati.
Aliongeza kuwa wakati mwingine wanawaambia watu wasubiri kwa muda kabla ya kuwapatia kadi hizo, ili kuepusha udanganyifu unaoweza kujitokeza.
Pia, Mkurugenzi Mtendaji huyo alisema kuwa lengo siyo tu kuziingiza Hospitali zote za Kanisa katika mpango huo, bali ni zile tu ambazo zimekidhi vigezo katika suala zima la utoaji wa matibabu.
Alisema kuwa wameandaa utaratibu wa kuwa na vipindi mbalimbali katika vyombo vya habari vya Kanisa, ikiwemo Tumaini Media, ili kuwafanya wengi wawe na ufahamu juu ya mpango huo.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa ACCLAVIA, Dk. Anselmi Anselmi alisema kuwa hakuna bima ambayo ni ya lazima, bali wao wapo kwa ajili ya kutoa bima yenye kusaidia watu, hasa wenye kipato cha chini.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Sekretarieti ya Mpango wa Nia Njema, Emmanuel Tibaijuka aliwasisitiza Wakristo kutambua kwamba mpango wa Nia Njema una faida kubwa kwao, hivyo ni vizuri wakafanya maamuzi ya kujiunga na mpango huo.
Akihitimisha katika Mkutano huo, Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Henry Mchamungu aliwashukuru Wawakilishi kwa kukubali kupokea utume huo, akiwataka kuendelea kufanya kazi bila kukata tamaa.
Askofu Mchamungu aliwasihi Maparoko kutoa nafasi kwa Wawakilishi parokiani, ili waendelee kutoa elimu na uhamasishaji, akiwataka Wakristo kufahamu kwamba huo si utapeli, bali ni mpango wenye manufaa makubwa kwao.

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Moja ya Mambo muhimu na ya Msingi ambayo Baba Mtakatifu Fransisko ameyakazia na kuyasisitizia katika ziara ya Kitaifa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan na ujumbe wake aliyoifanya hivi karibuni mjini Vatican, ni malezi na makuzi ya Watoto.
Katika ziara hiyo ya Kitaifa, Mama Evaline Malisa Ntenga, ambaye ni miongoni mwa ujumbe huo wa Rais, anasema kuwa Baba Mtakatifu Fransisko amekazia umuhimu wa malezi na makuzi ya watoto, sanjari na kujikita katika tunu msingi za maisha ya ndoa na familia.
Dalmas G. Gregory, M/Kiti Halmashauri Walei Jimbo la Zanzibar, anasimulia yale yaliyomgusa. Leonard Mapolu, Mwenyekiti wa VIWAWA, Taifa, anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema na baraka kupitia kwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (Tanzania Episcopal Conference: TEC).
Imegota takribani miaka 12 tangu Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete wa Tanzania alipotembelea mjini Vatican na kukutana na Baba Mtakatifu Benedikto XVI tarehe 19 Januari 2012.
Katika mazungumzo ya dakika kumi na tano, viongozi hawa wawili waligusia kuhusu: Majadiliano ya kidini, amani katika eneo la Maziwa Makuu, Afya, Ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.
Ni katika muktadha wa kujenga na kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia kati ya Tanzania na Vatican, tarehe 12 Februari 2024, Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania alikutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Fransisko mjini Vatican.
Aidha, Rais Samia alibahatika pia kukutana na kuzungumza na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu Mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu Mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa.
Katika mazungumzo yao ya faragha yaliyodumu kwa takribani dakika 25 wameridhika na uhusiano wa kidiplomasia kati ya Vatican na Tanzania; mchango na dhamana ya Kanisa Katoliki katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Tanzania, hususan katika sekta ya: elimu, afya, ustawi wa jamii pamoja na changamoto ambazo Tanzania inapitia kwa sasa.
Mama Evaline Malisa Ntenga, Mjumbe wa Bodi Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani na Rais wa Wanawake Wakatoliki Afrika WUCWO Afrika, ambaye pia ni Mwenyekiti wa WAWATA, Taifa, nchini Tanzania, katika mahojiano maalum na Radio Vatican, alionesha furaha kwa heshima waliyopewa waamini walei kuungana na Rais Samia Suluhu Hassan katika ziara yake ya kikazi mjini Vatican.
Mama Ntenga alimpongeza Rais Samia kwa juhudi zake za kukuza: Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Kusonga mbele; mambo yanayofumbatwa katika falsafa ya “Four R.” Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu Fransisko alipokutana na kuzungumza na Mama Ntenga amekazia umuhimu malezi na makuzi ya watoto sanjari na kujikita katika tunu msingi za maisha ya ndoa na familia.
Amewasihi waamini walei waendelee kushikamana na kutembea pamoja kama sehemu muhimu sana ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi nchini Tanzania; ujenzi ambao kimsingi unafumbatwa katika: Umoja, Ushiriki na Utume. Ameipongeza Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, (WAWATA), kwa kuendelea kuwa mstari wa mbele kwa malezi na makuzi ya Utoto Mtakatifu nchini Tanzania.
Pamoja na mambo mengine, Rais Samia Suluhu Hassan alikazia umuhimu wa kujenga, kuendeleza pamoja na kudumisha maridhiano ili kuendeleza misingi ya haki, amani, ustawi na maendeleo ya Tanzania.

LUSAKA, Zambia
Shirika la Huduma za Vyombo vya Habari vya Kikatoliki, limeadhimisha Siku ya Redio Duniani kwa kutambua mchango mkubwa wa redio katika kueneza ujumbe wa matumaini, upendo na haki ya kijamii.
Mkurugenzi Mtendaji wa Huduma za Vyombo vya Habari Katoliki nchini Zambia, Padri Winfield Kunda alisema kuwa Siku ya Redio Duniani mwaka huu imeadhimishwa chini ya kaulimbiu “Radio - A Century Informing, Burudani, na Kuelimisha.” Inaangazia athari kubwa ya redio katika kuunda maisha kwa kutuhabarisha na kukuza elimu tangu zamani.