Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

Kanisa chini ya Uongozi wa Papa Paulo VI (1963 – 1978)

Wiki iliyopita tuliwaletea kazi alizozifanya Papa Yohana XXIII katika kipindi kifupi cha uongozi wake. Leo tunawaletea historia ya uongozi wa Mrithi wake Papa Paulo VI na kuendeleza yale ya mtangulizi wake. Sasa endelea

Papa Yohana XXIII (1958 - 1963: wa 261) alipofariki Juni 3 1963, mambo yote ya Mtaguso yalisitishwa kumsubiri Papa mpya ambaye angeliamua kama Mtaguso uendelee au uishie hapo. Tarehe 21 Juni 1963 alichaguliwa Kardinali Yohana Baptista Montini, Askofu Mkuu wa Milano.

Montini alikuwa mmoja wa Makardinali wenye msimamo wa kati. Siku moja baada ya kuchaguliwa, alitangaza kwamba Mtaguso utaendelea na kwamba atajaribu kutimiza malengo yaliyowekwa na Papa Yohana XXIII. Alisisitiza kuwa  Mtaguso ndio utakuwa kipaumbele chake cha kwanza.

Kardinali Montini alizaliwa tarehe 26 Septemba 1897 huko Concesio Italia. Alipadrishwa mwaka 1920 na kutumwa Roma kwa masomo, ambako baadaye aliingizwa katika Idara ya Mambo ya Nje na kutumwa Ubalozini Warsaw, Poland, mwaka 1923 na baadaye kurudi ofisini katika idara hiyo Roma.

Mwaka 1954 Papa Pius XII (1939 - 1958: wa 260) alimteua Montini kuwa Askofu Mkuu wa Milano, na Papa Yohana XXIII akamfanya Kardinali mwaka 1958. Tarehe 21 Juni 1963, akachaguliwa kuwa Papa na kuchukua jina la Paulo VI.

Papa Paulo VI (1963 - 1978: wa 262) aliamini katika muendelezo wa mapokeo ya Kanisa bila kuyachakachua, lakini pia aliamini mapokeo yasiyokuwa ya msingi na yanayokinzana na alama za nyakati yanapaswa kuhuishwa na kufanywa upya.

Mara moja aliimarisha Tume alizoziweka Papa Yohana XXIII na kuongezea sura mpya. Kati ya Wenyeviti wa Mikutano, jumla aliweka mchanganyiko wa wanamapinduzi kama Kardinali Suenens wa Ubelgiji, Kardinali Doepfner wa Ujerumani, na Kardinali Lercaro wa Bologna, Italia, na wale wenye msimamo wa wastani kama Kardinali Agagianian. Makardinali hawa wanne ndio walikuwa mpini wa mwenendo wa Mtaguso.
 
Papa Paulo VI aliwaalika Walei kuhudhuria vikao vya jumla bila kusema au kipiga kura. Aliruhusu vile vile habari za mwenendo wa Mtaguso kutolewa mara kwa mara kwa Waandishi wa Habari.

Kikao cha Pili, Septemba 29 hadi Desemba 4, 1963:
Papa Paulo VI aliitisha kikao cha pili kuanzia tarehe 29 Septemba hadi Desemba 4 mwaka 1963. Katika ufunguzi wa kikao hicho, alirudia nia yake ya kufuata nyayo za mtangulizi wake. Wakati wa ufunguzi, alitoa madhumuni manne ya msingi kwa Mtaguso huo:

1.    Kanisa lijitambulishe kwa Ulimwengu kwa tamko rasmi, likijielezea kwa kujielewa.

2.    Aggiornamento, yaani kufanya upya, lazima iendelee, si kwa kuvunja mila na mapokeo msingi, bali kwa kuondoa kile ambacho kina kasoro.

3.    Kanisa lazima lifanye kazi kuelekea kwa umoja kati ya Wakristo wote. Wakati wa ufunguzi akisema hivyo, aliwageukia waangalizi wasio Wakatoliki na kuomba msamaha kwa jeraha lolote ambalo Kanisa Katoliki lingekuwa limewasababishia Wakristo wengine.

4.    Kanisa lazima lijihusishe na mazungumzo na Ulimwengu: “siyo kushinda na kuuteka, bali kutumikia, si kudharau bali kuthamini, si kuhukumu bali kufariji na kuokoa”.

Kikao cha Tatu, Septemba 14 hadi 21 Novemba 1964:
Katika kikao cha tatu, kutokana na manung’uniko ya Kardinali Suenens kwamba kulikosekana Wanawake Walei Waangalizi kwa sababu kulikuwepo Masista tu, Papa aliwateua Wanawake 15 Walei Waangalizi kuungana na Masista 10.
 
Kipya kingine katika ufunguzi wa kikao hicho, Papa aliadhimisha Misa na Maaskofu 24 kutoka nchi 19. Hii ilikuwa mara ya kwanza katika Kanisa la Kirumi, kwa sababu kabla ya hapo kila Padre aliadhimisha peke yake. Mapinduzi ambayo sasa ni jambo la kawaida yalikuwa yameanza.

Kikao cha Nne, Septemba 14 hadi Desema 8, 1965:
Kikao cha nne na cha mwisho kilikuwa tarehe 14 Septemba hadi 8 Desemba mwaka 1965. Kikao hiki kilikuwa kirefu zaidi ya kingine chochote kilichotangulia  kwa wiki mbili, kwani hiki kilikuwa cha wiki 12.

Katika ufunguzi wa kikao hiki, alitangaza kwamba kutakuwepo na Sinodi za Maaskofu pamoja na Baba Mtakatifu katika ngazi ya Kimataifa ili kumshauri Papa. Hii iliwafurahisha wengi. Hadi sasa, Sinodi hizi zinafanyika.

Mwishoni mwa kikao cha nne ambacho ndicho kilikuwa kikao cha mwisho, kuna matukio muhimu yalifanyika. Kitu kipya kabisa Papa alisali pamoja na Wakristu wa madhehebu mengine waliokuwa katika Mtaguso.

Tarehe 6 Desemba 1965, alitangaza Mwaka wa Jubilee kuanzia tarehe 8 Desemba 1956 hadi tarehe 8 Desemba 1966, kwa ajili ya kutangaza na kueneza Mafundisho ya Mtaguso wa Vatikani II (1962 - 1965).

Tarehe 7 Desemba akiwa pamoja na Patriarka Athenegoras wa Konstantinople, ambaye alikuwa Mkuu wa Kanisa la Kiortodosi, walilaani utengano, chuki na kuhukumiana (Excommunications) zilizofanyika mwaka 1054, zilizotenganisha Kanisa la Kiortodosi na Kanisa Katoliki.

Wote walisameheana rasmi, na kuahidi kufanya wawezavyo ili kurudisha umoja. Tarehe 8 Desemba 1965, Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatikano ulifungwa kwa Misa Takatifu iliyoadhimishwa na Papa katika Uwanja wa Basilica ya Mtakatifu Petro, huko Vatikano.

Matokeo ya Mtaguso wa Pili wa Vatikano ni kwamba kwanza uligeuza muono wa Kanisa Katoliki na kulileta katika mtazamo wa nyakati zake, bila kugeuza Mafundisho na Mapokeo Msingi ya Kanisa.

Rate this item
(0 votes)

Leave a comment

Make sure you enter all the required information, indicated by an asterisk (*). HTML code is not allowed.