Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

KUZUNGUMZA KATIKA HADHARA – AINA ZA HADHIRA

Rais Mstaafu wa Marekani, Donald Trump. Rais Mstaafu wa Marekani, Donald Trump.

Na Dk. Deoscorous B. Ndoloi

Mpendwa msomaji, katika safu hii, wiki iliyopita tuliona vijitabia zoelefu (offending mannerisms) ambavyo vinaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa namna tunavyozungumza katika hadhara. Tulivitaja vijitabia hivi kama sehemu ya mawasiliano silonge.

Kwa kukumbushana tu, na kwa wale ambao hawakupata fursa ya kusoma makala husika, vijitabia hivi vinahusu kuwa na kitu chochote mdomoni (pipi au kimbaka), kujikuna kusikofaa, kutoa kicheko ‘kichafu’, kuwakonyeza ama kuwagusa wasikilizaji, kupiga chafya ama kukuohoa kusiko na staha, nk. Pengine tulishau vilevile kugusia juu ya vijitabia vya kuchezea vitu wakati tunapotoa wasilisho, kwa mfano hutikisatikisa funguo mkononi ama sarafu mfukoni, hutafuna kucha au mfuniko wa kalamu, kutingishatingisha magoti hasa wakati unapotoa wasilisho umemeketi, ‘kuvunja vidole’ (cracking knuckles), kugusagusa simu nk. Haya yote yatakufanya uonekane hujatulia.

Leo, katika safu hii, tushirikishane maarifa kidogo juu ya kujenga uhusiano wenye tija na hadhira (audience). Kwa wale ambao wanafuatilia mada zetu, tulisema kwamba haitoshi tu kwa mwasilishaji kuwa mbobezi katika uwanja wake, na kuwa na weledi katika kuzungumza katika hadhara, ni muhimu vilevile kujua aina ya wasikilizaji na sababu zinazowafanya wakusikilize. Hii itasaidia jinsi ya kujipanga kuwakabili. Tuone kwa kifupi aina za hadhira.

Aina ya kwanza tunaweza kuiita ni ya ‘hadhira-mateka’ (captive audience). Wasikilizaji wa aina hii wanajikuta kwamba, kimsingi, hapo walipo hawakuja kwa ajili ya kukusikiliza wewe. Kwa mfano wanachuo wapo chuoni kwa sababu moja ya msingi – elimu. Lakini, hata kama somo lako hawalipendi, unapoingia darasani, inabidi wakae kimya na kukusikiliza, kinyume na matakwa yao kwa vile sheria inawabana.

Wafungwa wanaweza kuwa mfano mwingine wa hadhira ya aina hii. Wapo kama kundi kwa sababu wanatumikia adhabu kwa makosa mbalimbali, na ‘wamekusanywa’ bila ridhaa yao. Katika sehemu za kazi, wapo wafanyakazi wengine wanaona kama kuhudhuria mikutano inayoitishwa na uongozi ni kama kupotezeana muda. Wafanyakazi wa namna hii, katika mikutano, ni hadhira-mateka. Wapo kwa sababu tu, wasipotii mamlaka, wanaweza kukaripiwa.

Ukujikuta unazungumza na hadhira kama hii, kwanza, unakuwa na kazi ngumu sana kuwabadilisha mtazamo/msimamo na kuwasabibishia kiu ya kukusikiliza. Katika mazingira haya, dakika chache za mwanzo za kutoa wasilisho ni muhimu sana – waaminishe kwamba una uzoefu na ujuzi katika mada husika, lakini pia washawishi kwamba mada yenyewe ni ya muhimu mno katika maisha yao na hasa katika kuimarisha mahusiano. Ikiwezekana tumia mifano ya watu ambao walishawahi kufanikiwa kimaisha kwa sababu walizingatia unayozungumza.

Aina ya pili ya hadhira ni ‘hadhira-chuki (hostile audience). Hadhira ya namna hii inaweza kuwa inaonesha dalili zote za chuki na kukosa shauku ya kutaka kujua/kuambiwa jambo. Chuki hii inaweza kulenga katika mada yenyewe; kwa mfano, wasilisho linalohusu kuwahamisha na kuwapeleka sehemu nyingine ya nchi kupisha suala ya maendeleo kama ujenzi wa miundombinu ama kuendeleza hifadhi ya wanyama pori.

Kama hadhira hii haioni faida ya haraka na ya moja kwa moja, utapata shida sana kuzungumza nao. Katika hali isitotegemewa, hadhira hii inaweza hata kuzua tafrani, uhasama ama ushari (wa maneno au matendo). Tumeona kwa mfano viongozi wakijaribu kuzungumza na hadhira wakati wa migomo. Wakati mwingine katikati ya mgomo kunaweza hata kuzuka mapigano. Hali ikidorora vya kutosha hadhira kama hii kuamua kutojihusisha na jambo lolote (apathy).

Hadhira-chuki inaweza kuelekeza uhasama wake kwa mtoa mada binafsi, endapo atasema jambo linalowafedhehesha wasikilizaji. Ikumbukwe kwamba hadhira inaweza kuanza vizuri kwa usikivu wa kutosha, halafu polepole au ghafla hadhira inageuka kuwa na chuki, na kuamua kutotoa ushirikiano na mtoa mada.

Ni vizuri ukiwa unatoa mada kugundua iwapo kuna mabadiliko ya tabia-fiche kati ya wasikilizaji inayoashiria kwamba sasa ‘joto linapanda’ na hadhira inaanza kubadilika kihisia. Matendo na maneno yao madogomadogo yataashirika kinachoenda kutokea.

Vilevile tuliona juu ya mawasiliano silonge (non-verbal communication) na jinsi watu wanavyoweza kuzungumza hata kwa ‘kupiga kelele’ bila kufungua mdomo. Ukiwa mwasilishaji uwe hodari kugundua hili na kutumia mbinu zote kurudisha hali ya hewa katika hali ya utulivu.

Wakati mwingine hadhira inaweza kuwa na chuki na mamlaka yenye uhusiano na mwasilishaji, kama serikali. Hivyo kwamba chuki hii haielekezwi kwa mzungumzaji moja kwa moja, bali kwa serikali kupitia kwa mzungumzaji. Ni vema kama wewe ni mzungumzaji kujua uhasama au chuki hii inaelekezwa wapi, usije ‘ukanunua’ tatizo lisilokuhusu.

 Ni lazima kuwa mwangalifu na kuwa na weledi wa kisaikolojia kuweza kukabiliana na hadhira ya namna hii. Ni vema kutojitenga na tatizo, lakini ni vema zaidi kujua jinsi ya kukabili mabadiliko ya usununu wa hadhira. Kumbuka mhemko huambukiza; hivyo inasaidia kuukabili inavyofaa, pale unapoanza kwa mtu mmojammoja.

Jambo ambalo ningetaka kumalizia nalo, ni kwamba kama mwasilishaji mada, utakuwa umefeli kabisa ukiruhusu mhemko wa hadhira ukakuingia, na wewe ukapata hasira au ukaanza kuonyesha chuki, kwa sababu eti unahusishwa na masuala yasiyokuhusu.

Katika hali yoyote ile ya mhemko wa chuki toka kwa hadhira, uwe na busara ya kujizuia na usikubali kurubuniwa kisaikolojia, ukafanana na hadhira ya namna hii. Unapotoa mada uwe na utulivu ambao wasikilizaji wataona kwamba unayoyaona yahajakufanya ukatetereka toka kwenye kusudio lililokupeleka.
Tumsifu Yesu Kristu!
Itaendelea wiki ijayo.

Rate this item
(0 votes)

Leave a comment

Make sure you enter all the required information, indicated by an asterisk (*). HTML code is not allowed.