Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

Wagonjwa waaswa kumkimbilia Mungu

VIKINDU, PWANI

Na Mathayo Kijazi

Wagonjwa wametakiwa kumlilia Mungu ili awaponye matatizo yao, badala ya kutafuta msaada kwa waganga wa kienyeji, kwani Mungu ndiye anayesikia kilio cha kila mmoja na kumwondolea mahangaiko yake.
Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Henry Mchamungu alitoa wito huo wakati akitoa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Kuwaombea Wagonjwa na Watoa Huduma kwa Wagonjwa, iliyoadhimishwa katika Kituo cha Mafungo kilichopo Parokia ya Mtakatifu Vincent wa Paulo – Vikindu, iliyomo wilayani Mkuranga, mkoani Pwani.
“Kwa hiyo ndugu zangu, tunapougua tufahamu kwamba kuugua ni sehemu ya ubinadamu, tunatakiwa tumlilie Mungu kwa sababu Mungu anasikia kilio chetu. Tuache kuhangaikahangaika huko kutafuta mambo ya kidunia, mara kwa waganga wa kienyeji. Tukimlilia Mungu, yeye atatuondolea mahangaiko yetu,” alisema Askofu Mchamungu.
Alibainisha kuwa wengi wanakosa baraka katika maisha yao kwa kuwa hawakumtanguliza Mungu katika mahitaji yao ya kila siku, hivyo akawataka waepuke kutegemea mambo ya kidunia, ili baraka za Mungu ziwafikie.
Aidha, akifafanua kuhusu Sakramenti ya Wagonjwa, Askofu Mchamungu alisema kuwa Sakramenti hiyo siyo tu kwa ajili ya wagonjwa ambao wanakaribia kufa, bali ni Sakramenti ambayo hutolewa kwa wagonjwa wote, bila kuangalia wanaumwa kwa kiasi gani.
“Watu waliogopa sana Sakramenti ya Mpako wa Wagonjwa. Kwa hiyo hakuna ambaye alikuwa tayari kwa ajili ya kupokea Sakramenti hiyo, kwa sababu dhana ilikuwa kwamba ukishapokea Sakramenti ya Wagonjwa, kinachofuata unakufa…..,
“Na hata sehemu nyingine, mtu akishapatiwa Sakramenti ya Wagonjwa, basi ndugu zake wanaanza kuandaa utaratibu wa mazishi, hata kabla hajafa. Na kabla ya Mtaguso wa Pili wa Vatikano (1962-1965), watu walikuwa wanasubiri wagonjwa wao hadi wawe mahututi, ndipo wanaanza kumtafuta Padri ili aende akawapake mafuta. Sasa Mtaguso wa Pili wa Vatikano ukabadilisha hayo mambo, kwamba hiyo siyo Sakramenti ya Wanaokufa, bali ni Sakramenti ya Wagonjwa,” alisema Askofu Mchamungu.
Askofu huyo alisema kuwa hata mzee anapoamua kuomba Sakramenti hiyo kutokana na uzee wake, ni vyema akapatiwa, kwani Sakramenti hiyo ni vizuri kutolewa kwa mtu ambaye ana uelewa pindi inapotolewa, kuliko kwa mtu aliyepoteza fahamu.
Vile vile, Askofu huyo aliongeza kuwa Sakramenti hiyo inaruhusiwa kutolewa zaidi ya mara moja, akisema kwamba mgonjwa anapopatiwa Sakramenti hiyo, kisha akapona, na baadaye akaumwa tena, anastahili kupatiwa Sakramenti hiyo kwa mara nyingine.
Wakati huo huo, Askofu alibainisha kwamba mtu anayeishi maisha ya hovyo, na hataki kumrudia Mungu katika maisha yake, huyo hastahili kupatiwa Sakramenti ya Mpako wa Wagonjwa, bali atakapotubu na kubadilika, ndipo anastahili kupatiwa.
Aidha, aliongeza kuwa miongoni mwa watu ambao hawawezi kupatiwa Sakramenti hiyo, ni pamoja na watu wanaokwenda vitani, kwani licha ya kwamba wanakwenda kwenye hatari ya kifo, bali kifo hicho hakitokani na ugonjwa wala uzee.
Pia, alisema kuwa licha ya kwamba anayekwenda kunyongwa, anakwenda kwenye hatari ya kifo, bali hawezi kupatiwa Sakramenti ya Mpako wa Wagonjwa, kwa sababu kifo chake hakitatokana na ugonjwa wala uzee.
Katika homilia yake, Askofu Mchamungu aliwaasa watoa huduma kwa wagonjwa, kuendelea kutoa huduma hiyo kwa upole na kwa uaminifu mkubwa, akisema kuwa hiyo si kazi rahisi, na si kila mtu anaweza kuifanya.
Aliwasisitiza Madaktari kutoa huduma hiyo kwa upendo, huku wakiepuka kuwa na uso wa ‘mbuzi’ katika utoaji huo wa huduma, kwani wagonjwa wanahitaji zaidi upendo na faraja katika kipindi walicho nacho.
Kwa upande wake Katibu wa Afya Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Pauline Archard, alitoa wito kwa wauguzi kutambua kwamba wanapotoa huduma kwa wagonjwa, wawe wakarimu, na kuwahudumia kwa upendo.

Rate this item
(0 votes)

Leave a comment

Make sure you enter all the required information, indicated by an asterisk (*). HTML code is not allowed.