Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

Dekano wa Dekania ya Mtakatifu Gaspar na Paroko wa Parokia ya Bikira Maria wa Mlima Karmeli, Bunju, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Padri Dominick Somola, akisalimiana na Waamini wa Chama cha Moyo Mtakatifu wa Yesu wa Parokia ya Bikira Maria wa Rozari Takatifu, Makongo Juu, baada ya kushiriki Adhimisho la Misa Takatifu iliyofanyika katika Parokia ya Bunju, hivi karibuni.

Paroko mpya wa Parokia ya Bikira Maria Mama wa Mungu, Mbopo-Madale, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, (wa tatu kutoka kushoto), akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Kamati Tendaji ya Parokia hiyo, baada ya Adhimisho la Misa Takatifu ya Kumsimika Paroko huyo, iliyofanyika hivi karibuni parokiani hapo. (Picha zote na Yohana Kasosi)

Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, akiwa na Mapadri katika picha ya pamoja na vijana 153 waliopata Sakramenti Takatifu ya Kipaimara iliyofanyika katika Parokia ya Mtakatifu Augustino, Salasala jimboni humo, baada ya Adhimisho la Misa Takatifu ya Kipaimara. Kulia kwa Kardinali ni Paroko wa Parokia hiyo, Padri Peter Assenga.

DAR ES SALAAM

Na Mathayo Kijazi

Imeelezwa kuwa hakuna kitu kinachoweza kufanywa na Waamini katika Parokia, bila kumshirikisha Askofu Mkuu, kwani vitu vyote ni mali ya Jimbo.
Kauli hiyo ilitolewa hivi karibuni na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Stephano Musomba wakati wa homilia yake katika Adhmisho la Misa Takatifu ya Sakramenti Takatifu ya Kipaimara kwa vijana 80 wa Parokia ya Mtakatifu Teresa wa Benedicta wa Msalaba – Msumi, jimboni Dar es Salaam.
“Maeneo yote hayo mliyoyanunua, mjue kwamba ni mali ya Jimbo, sawa jamani. Kwa hiyo, msije mkaanzisha kitu chochote kile, bila kumhusisha Askofu Mkuu, kwa sababu nilisikia tetesi tetesi kwamba mnataka kununua sijui shamba la kuzikia, mkienda kienyeji bila baraka ya Askofu Mkuu, ni kosa,” alisema Askofu Musomba.
Awali, katika homilia yake Askofu huyo aliwataka wazazi kuongeza usimamizi kwa watoto wao waliopokea Sakramenti Takatifu ya Kipaimara, kwani hiyo itawasaidia watoto hao kutambua wajibu wao walioitiwa.
“Kwa hiyo wazazi na walezi, ni jukumu lenu kuongeza usimamizi kwa watoto hawa kwa sababu hiyo ndiyo njia itakayowafanya watambue wajibu wao. Hakikisheni watoto hawa wasiyumbishwe wala wasichanganywe katika imani,” alisema Askofu Musomba.
Vile vile, alisema kuwa mtoto anapopokea Sakramenti Takatifu ya Kipaimara, anatakiwa kushuhudia kile anachokiishi, kwani kwa Sakramenti hiyo, tayari ameimarika.
Aliongeza kuwa Sakramenti hiyo Takatifu ina umuhimu mkubwa kwa kila anayeipokea, kwa sababu inamkamilisha katika Neema ya Ubatizo, na kumkamilisha pia katika imani Katoliki.
Sambamba na hayo, Askofu huyo Msaidizi aliwakumbusha Wakristo kutambua kwamba zawadi ya Kristo mfufuka kwa Waamini wake, ni amani.
Wakati huo huo, Askofu huyo, aliwasihi Waamini wa Parokia ya Msumi kumshukuru Mungu, kwani kupitia Adhimisho hilo la Misa Takatifu, wamepata Wakristo wengine 80 waliokomaa ambao ni Waimarishwa.
Aliwashukuru Waamini wa Parokia hiyo kwa kuwachangia Skauti Shilingi laki 3 kwa ajili ya Kongamano lao linalotarajia kufanyika jimboni humo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Parokia hiyo, Frank Werema, katika risala yake, alisema kuwa miongoni mwa mambo wanayoendelea kuyafanya kiroho, ni pamoja na kuwahamasisha Waamini ambao bado hawajafunga ndoa, wafunge, kwani kaya zaidi ya 482, wakazi wake hawajafunga ndoa.
Akizungumzia changamoto zinazowakabili hadi sasa parokiani hapo, Mwenyekiti huyo alisema kwamba kubwa ni ubovu wa miundombinu ya barabara katika maeneo ya Parokia hiyo.
Naye Mwandishi Laura Chrispin, anaripoti kuwa, Watoto wanaopokea Sakramenti Takatifu ya Kipaimara wametakiwa kufahamu kuwa wanampokea Roho Mtakatifu kwa mara ya pili atakayewaongoza siku zote za maisha yao.
Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Stephano Musomba wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya Sakramenti Takatifu ya Kipaimara iliyofanyika katika Parokia ya Mtakatifu Martha -Mikocheni, alisema kuwa hata kipindi cha Mitume kabla ya kumpokea Roho Mtakatifu, Mitume mara zote walikuwa ni watu wa kuuliza maswali lakini baada ya kumpokea Roho Mtakatifu, walikuwa ni watu wa ushuhuda zaidi.
Hiyo ikiwa ni kama funzo kwenu kuwa inawapasa kuwa ni watu wa kumshuhudia Kristu kwa matendo yenu wenyewe, pamoja na kueleza makuu ya kristu kwa watu wengine.
Alisema hata katika Sinodi ya Maaskofu, inatuelekeza kutembea pamoja na kuwataka wengine wasibaki nyuma bali kutembea pamoja, ndiyo maana ukisema Kanisa la Kisinodi unaseama Ushirika na Ushiriki wa Kimisionari.
Katika Ushirika hawa ni Wanajumuiya, Wanafamilia ambayo kuna huduma wana hudumiana na kufanya kazi zote kwa pamoja na ni washiriki, ndo mana wanakuwa Wamisionari.
Mhashamu Musomba alisema “Roho Mtakatifu anavyokuja kwetu, anatufanya tuzungumze Lugha moja, hiyo ambayo ni katika upendo zaidi”.
Askofu Musomba aliwataka Waamini kuwa na amani katika familia zao na kumwomba zaidi Mungu awaepushe na dhambi kwani dhambi ni mojawapo ya sababu inayopelekea kupotea kwa amani.
Aidha, aliwataka Waamini kutosahau baadhi ya dhambi, hasa dhambi ya jamii ambayo ni kwa mtu yeyote anaweza kufanya mfano kwa wafanya biashara kutengeneza chakula kwa uchafu na kusababisha magonjwa kwa jamii, hiyo ni dhambi na inakupasa kuiungama mara moja.
Askofu Musomba alitoa wito kwa wazazi na walezi kwa kuwataka wasaidie kuwasindikiza katika imani moja ya Kanisa Katoliki, na siyo kuwachanganya watoto katika imani zingine.

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, amewataka Waamini wamtangulize Mungu, wanapofanya jambo lolote, ili wapate neema kamili.
Kardinali Pengo alisema hayo katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Sakramenti ya Kipaimara kwa vijana 150, iliyofanyika katika Parokia ya Mtakatifu Augustino – Salasala, jimboni Dar es Salaam.
“Watu wengi huwa wanapenda kujifanyia mambo wanayoyajua wao, na kuamua kumuacha Mungu. Ukijifanyia kitu bila kumtanguliza Mungu huwezi kufanikiwa,” alisema Kadrinali Pengo na kuongeza, “Hata kama unatamani na wewe uje kuwa Rais wa Taifa hili la Tanzania, au unataka uje kuwa mfanyabiashara mkubwa katika nchi hii, lazima umtangulize Muumba wako ambaye ni Mungu Baba iliyekubariki ili uweze kufaulu vizuli.”
Aliwasihi vijana waliopokea Sakramenti Takatifu ya Kipaimara kufahamu kwamba, sasa wamekuwa Wakristo kamili, akiwasisitiza kuyazingatia mafundisho ya Kanisa ili waendelee kudumu katika imani.
Kwa upande wake Paroko wa Parokia hiyo, Padri Peter Assenga aliwaomba wazazi na walezi wa vijana hao wasihame imani yao Katoliki, kwani ndiyo imani ya kweli.
Alimshukuru Kardinali Pengo kwa kuwapatia vijana hao Sakramenti Takatifu ya Kipaimara.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Walei wa parokia hiyo, Boniface Ngowi alisema kuwa kwa sasa Parokia hiyo imepata mafanikio makubwa, kwani wamejenga kanisa jipya kubwa ambalo lilitabarukiwa na Kardinali Pengo, alisema kuwa wao kama Parokia, wamejenga nyumba kubwa ya kisasa ambayo ilibarikiwa na kuzinduliwa na Askufu Mkuu wa Jimbo hilo, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi.

KIGOMA

Na Mwandishi wetu

Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amewahakikishia Watanzania kuwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuleta mapinduzi kwenye Sekta ya Umwagiliaji, hivyo miradi yote aliyoahidi itatekelezwa.
Waziri Bashe alisema hayo wakati akizungumza na wadau wa umwagiliaji katika eneo la mradi wa Luiche, ambapo amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufanikisha utekelezaji  wa mradi huo.
“Leo tumefanya uzinduzi wa Mradi Mkubwa wa Umwagiliaji katika Bonde la Luiche Wilayani Kigoma katika Mkoa wa Kigoma. Miradi hiyo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 60 itakwenda kunufaisha zaidi ya wakulima 9312 kupitia Kilimo cha Umwagiliaji,”alisema Bashe.
Waziri Bashe alisisitiza kwamba utekelezaji wa miradi hiyo unaofanywa na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, si hadithi, bali umelenga  kuinua Sekta ya Kilimo cha Umwagiliaji, na kuchochea ukuaji wa uchumi nchini.
Aliitaka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kujipanga kuhakikisha wanatekeleza miradi hiyo, na wananchi wapuuze wanaowalaghai kuuza mashamba.
Aliongeza kuwa wizara inamshukuru Rais Dk. Samia kwani anafanya kwa vitendo na hataki utani katika kilimo cha umwagiliaji.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Raymond Mndolwa alimshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kufanikisha utekelezaji wa mradi wa Bonde la Luiche, ambao umekuwa ukizungumzwa tangu nchi ilipopata Uhuru, na kwamba uwekezaji huo mkubwa uliofanywa na serikali unakwenda kuleta mapinduzi makubwa kiuchumi kwa wananchi wa Kigoma.
Mndolwa pia ametumia fursa hiyo kupokea maagizo ya Waziri wa Kilimo.
“Mradi huu ni mkubwa na utazingatia uwekaji wa miundo mbinu muhimu kama barabara na itazingatia kulinda vyanzo vya maji na mazingira”, alisema Mndolwa.
Mndolwa pia aliongeza kuwa Tume ilipokea maelekezo ya Serikali  kuwa mradi ujumuishe ujenzi wa   ghala, nyumba ya watumishi, pamoja na Ofisi ya Umwagiliaji.
Akiwasilisha Taarifa ya Umwagiliaji kwa Mkoa wa Kigoma, Mhandisi Umwagiliaji Mkoa wa Kigoma, Katuta Mustang, alisema kwamba Mkoa wa Kigoma una eneo linalofaa kwa umwagiliaji lenye ukubwa wa hekta 147,000 ukiwa na skimu 59 za umwagiliaji skimu 6 pekee ndizo zilizoendelezwa.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Salum Kalli alisema serikali itahakikisha ulinzi wa mradi huo.
Akimkaribisha Waziri wa Kilimo, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto Thobias Andengenye, aliishukuru serikali kwa uwekezaji Mkubwa unaofanywa katika Mkoa wa Kigoma, kupitia kilimo cha umwagiliaji.
Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini, Ngenda Shabani Kirumbe,alimshukuru raid Dk. Samia Suluhu Haasan kwa kufanikisha utekelezaji wa Mradi wa Luiche.
Mradi wa Luiche upo katika wilaya ya kigoma, mkoa wa Kigoma. Mradi huu unajumuisha vijiji vya Kamara, Simbo, Kaseke, Nyamori, Msimba, Matiazo pamoja na Kagera. Mradi huu utakuwa na  ya hekta 3000 zitakazomwagiliwa baada ya ujenzi kukamilika. Mradi huu wa Luiche umegawanyika katika mikataba miwili ambayo ni Mkataba wa ujenzi wa bwawa pamoja na mkataba wa ujenzi wa skimu ya umwagiliaji.

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, ameonya tabia ya unyanyasaji na ukatili unaofanyika dhidi ya watu wenye ualbino, kwani hali hiyo inaleta hofu kubwa katika jamii.
Kardinali Pengo alitoa onyo hilo katika Adhmisho la Misa Takatifu ya Sakramenti ya Kipaimara kwa vijana 35, wa Parokia ya Utatu Mtakatifu – Changanyikeni, jimboni Dar es Salaam.
“Unaposikia kuna mtoto anauawa, eti kisa ni albino, na moja kati ya watu waliohusika, ni baba yake mzazi, unaanza kupata hofu ya ajabu. Mtoto bila kosa lake amezaliwa vile,” alisema Kardinali Pengo.
Alisema kuwa Waimarishwa hao, moja ya mambo wanayotakiwa kuyafanya, ni kuleta utofauti, ikiwemo kuhakikisha kwamba kila wanapokwenda, wanapeleka mwanga wa Injili.
Aidha, aliongeza kuwa wasiruhusu popote walipo pakose mwanga wa Injili, badala yake watekeleze wajibu huo kwa matendo, na si kwa maneno pekee.
Katika homilia yake, Kardinali Pengo aliwataka Waimarishwa hao kutambua ukuu wa jukumu walilopewa kwa mfano wa maisha, na si vinginevyo.
Aliwashauri Wanachanganyikeni kwamba kama wataweza, wajenge shule ya Chekechea itakayohudumiwa na Watawa katika eneo la Parokia yao.
Kwa upande wake, Rita Mzava, mmoja wa Waimarishwa, akisoma risala yao kwa niaba ya vijana wenzake, aliuomba Uongozi wa Jimbo hilo kuwawekea utaratibu wa kuendelea kupatiwa Mafundisho ya Imani, ili waendelee kuiishi imani yao.
Kwa mujibu wa risala iliyosomwa, Parokia ya Utatu Mtakatifu – Changanyikeni, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, ina jumla ya Waamini wapatao 1,500.

DAR ES SALAAM

Viongozi wa Halmashauri ya Walei wa Parokia za Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, wametakiwa kuacha kuingia kwenye mizozo na malumbano na Maparoko, ili kazi ya Mungu isonge mbele.
Wito huo ulitolewa hivi karibuni na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Henry Mchamungu wakati akitoa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Sakramenti ya Kipaimara kwa vijana 34, katika Parokia ya Bikira Maria Mama wa Mungu – Mbopo Madale, jimboni Dar es Salaam.
“Viongozi mhakikishe mnadumisha mshikamano na Maparoko wenu, kwani kwa kufanya hivyo, kazi ya Mungu itasonga mbele,”alisema Askofu Mchamungu.
Akitoa nasaha kwa Wasimamizi, Askofu Mchamungu alisema kuwa: “Wasimamizi nawaomba sana mshikamane na wazazi au walezi wa vijana hawa kuwalea kiimani, maana wewe umepewa jukumu hili umsaidie mlezi au mzazi kumsimamia huyu kijana…
“Sasa jukumu ni lako, umuongoze ili aweze kuiishi vizuri imani yake ya Ukristo, maana wasimamizi wengi wakimsimamia kijana wakafurahi siku hiyo, basi hana muda naye tena, hamfuatilii wala kuwajulia hali, inakuwa imetoka,” alisema Askofu Mchamungu.
Aliwasisitiza Waimarishwa kutoacha kwenda kusali, kujifuza, pamoja na kushiriki shughuli mbalimbali za Kanisa, kwani wakifanya hivyo, watakuwa vijana wema na wenye nguvu ya Roho Mtakatifu waliyempokea.
Aidha, aliwaasa vijana hao kutodanganywa na manabii wa uongo katika maeneo wanayoishi.
Padri Luwena asimikwa rasmi:
Katika Adhimisho hilo la Misa Takatifu, Askofu Mchamungu alimsimika rasmi Paroko wa Parokia hiyo, Padri Joseph Luwena akiwaomba Waamini kushirikiana naye vizuri katika kazi zake za Kitume.
Aidha, aliwasihi Waamini wa Parokia hiyo kuongeza jitihada juu ya ujezi wa nyumba ya Mapadri, ili ujenzi huo ukamilike kwa wakati, na Paroko aweze kuishi sehemu bora.
“Hakikisheni Paroko wenu anakaa mahali pazuri, kwa sababu anawahudumia kiroho. Mmpende, mmjali, mthamini, kwa kuwa Paroko huyu mmekabidhiwa na Askofu Mkuu wa Jimbo, kwa hiyo msipomjali, sio vizuri…
Kwa upande wake, Padri Joseph Luwena aliwaomba Waamini wa Parokia hiyo kumpa ushirikiano, ili aweze kufanya kazi kwa amani, akimshukuru Askofu Mchamungu kwa kuwapatia sakramenti vijana hao.

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Diwani wa Kata ya Makurumla Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo Mkoani Dar es Salaam, Bakari Kimwanga, amewataka wazazi na walezi kuhakikisha wanakuwa na utulivu hasa kutokana na taharuki ya utekaji watoto kwenye shule.
Pamoja na hali hiyo, amesema kuwa mpaka sasa ndani ya Kata ya Makurumla, hakuna tukio la kutekwa kwa mtoto, huku akiweka wazi kuwa ni lazima kila mwana jamii ahakikishe anatoa ulinzi kwa mtoto, hasa wanapokuwa mitaani.
Kauli hiyo aliitoa hivi karibuni alipokuwa akizungumza na wazazi, walezi na waalimu katika shule za Msingi za Mianzini, Karume na Dk. Omari, ambapo juzi ilizuka taharuki ya kutekwa watoto kwenye shule hizo, na kuibua sintofamu kwa wazazi kulazimika kuvamia shule ili kuona usalama wa watoto wao.
“Tangu zilipoibuka taarifa hizi za taharuki Julai 22, 2024 (Jumatatu), tumefuatilia taarifa kwenye shule zetu, vyombo vya ulinzi na usalama, kwa maana ya Jeshi la Polisi, hali iko shwari wazazi wenzangu.
Aidha, aliwataka wazazi kutambua kuwa ni lazima kuweka mkazo kwenye suala la lishe kwa watoto kwa kuhakikisha wanachangia Shilingi 500 ya chakula kama walivyokubaliana kwenye mikutano ya wazazi, jambo ambalo litamsaidia mtoto kupata chakula shuleni badala ya kwenda mitaani wakati wa kipindi cha mapumziko.
Kwa upande wake Afisa Elimu Msingi, Manispaa ya Ubungo, Denis Nyoni aliwataka wazazi kuwa na utulivu kwani hadi kufikia jana hakuna taarifa za watoto kutekwa katika shule kwenye manispaa hiyo.
“Naomba waalimu msisahau wajibu wa kuandika mahudhurio ya watoto kila siku wawapo darasani, na hata wakati wanapomaliza masomo kwa siku, majina yaitwe. Hatua hii ndiyo njia ya kuendelea kudhibiti usalama wa watoto wetu,” amesema Nyoni
Naye Polisi Kata ya Makurumla, Insp Emmanuel Humba, alisema kuwa katika Kata ya Makurumla hali ni shwari, hakuna tukio la utekaji kwa watoto, huku akiwaomba wazazi wawe na utulivu wanapopata taarifa za taharuki.

Morogoro

Na Modest Msangi

Paroko Msaidizi wa Parokia ya Mtakatifu Augustino – Mzumbe, Jimbo Katoliki la Morogoro, Padri Dk. Romanus Dimoso amewataka Waamini kutafakari maisha yao na kutambua kwamba wao ni Viongozi bora.
Padri Dimoso alisema hayo wakati wa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Dominika ya 16 ya Mwaka ‘B’ wa Kanisa iliyoadhimishwa parokiani hapo.
Padri Dimoso ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, alisema kuwa katika familia, kaya, na jamii, Viongozi wameweka kipaumbele kutafuna mali za familia, na kuwaacha watu wakiteseka kwa kukosa huduma za kijamii.
“Ukiona maendeleo katika familia au jamii fulani, ujue kiongozi wao anawajibika vyema, lakini baadhi yao wamekuwa panya wa maendeleo ya watu, baba au mama katika familia anakuwa panya, huwezi kuona maendeleo katika familia au kaya yao,”alisema Padri Dimoso.
Padri Dimoso alisema kuwa Yesu Kristo ni mfano bora wa kuigwa alipowatuma Wafuasi wake waliporudi kutoa ripoti ya kazi waliyotumwa, aliwapongeza na kuwaambia waende mahali pasipo na watu, wakapumzike.
Azungumzia uchaguzi Mkuu
Aliongeza kusema kwamba huu ni mwaka wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, na mwakani ni Uchaguzi Mkuu, hivyo Waamini kama sehemu ya wananchi, wanapaswa kutafakari kwanza kabla ya kuamua wamchague nani.
Alisema kwamba kwa Miaka 60 ya Uhuru, maendeleo yamekuwa ni ya kupapasa, kwani baadhi yao wamekuwa na tabia zisizofaa katika jamii yao.
Padri Dimoso alibainisha kwamba ili kupata viongozi ambao hawatakuwa kama panya, kabla ya kuwachagua, wananchi wanapaswa kutafakari kwanza hali ya changamoto zilizopo katika jamii, na kuona kama anayechaguliwa, anaweza kuzitatua.