Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

HISTORIA YA KANISA

Katika safu hii ya Chimba Chimba Historia ya Kanisa wiki iliyopita tuliwaletea mada ya historia ya uinjilishaji katika nchi ya Rwanda. Leo tunaendelea kuwaletea historia ya uinjilishaji nchini Burundi na Kongo Brazaville. Sasa endelea…

Wamisionari wa kwanza, Wamisionari wa Afrika, walifika Burundi kutokea Ujiji, Tanzania, mwaka 1879 wakingozwa na Padre Deniaud, na kufungua misioni Rumonge. Lakini mwaka 1881 kwa chuki ya Waarabu wakishirikiana na baadhi ay Waafrika, walimwua Padri na wenzake wawili. Hapo ikabidi misioni isitishwe. Sehemu ya Burundi walibaki Kibanga ukingoni mwa Ziwa Tanganyika.
Mwaka 1895 Burundi iliunganishwa na Vikariati ya Unyanyembe, Tanganyika.  Parokia za kwanza zilifunguliwa ni Muyinga mwaka 1898 na Mugera mwaka 1899. Historia ya mwanzo ya Burundi ilienda sambamba na historia ya Rwanda.
Mwaka (1912-1922), ziliunganisjwa katika Vikariati moja ya Ruvu, chini ya Askofu Hirth. Jamii ya Burundi ilikuwa na mshikamano mkubwa kuliko ule wa Rwanda. Vile vile kati ya watawala, licha ya Watutsi yalikuwepo makabila mengine mawili, Bahima ambao ni ukoo mmojawapo wa Watutsi, na Ganwa ambao ni Wahutu, lakini wa damu ya kifalme. Hii ilileta kidogo changamoto kati ya Watutsi.
Vile vile, kuna familia nyingi zaidi zenye damu mchanganyiko wa Kitutsi na Kihutu. Dini ilienea haraka zaidi Burundi kuliko Rwanda, baada ya Vita Kuu ya Pili (1939-1945) palikuwepo Wakatoliki 600,000 ambao walikuwa mara mbili ya wale wa Rwanda, na miaka kumi baadaye kabla ya Uhuru mwaka 1959 walishafikia Wakatoliki 1,200,000 ambao walikuwa asilimia 55 ya wakazi wote.
Miito ya Upadre ilikuwa michache, walipata Padre wa kwanza Mwafrika mwaka 1925 na Askofu wa kwanza Michael Ntuyahaga mwaka 1959.
Mauaji yaliyotokea Rwanda mwaka 1960 yalliwafanya Watutsi wa Burundi wajihami.  Mwaka 1962 chama cha Watusi UPRONA kilichukua madaraka Burundi ilipopata Uhuru chini ya mwana mfalme Rwagasore, ambaye bahati mbaya aliuawa miezi michache baadaye.
Ingawa katika uchaguzi wa mwaka 1965 Wahutu walishinda, lakini madaraka yalichukuliwa na Watutsi.  Wahutu walipoasi wakipigania haki yao, viongozi 131 wa Kihutu na Wahutu wengine waliuawa na Kanali Micombero wa kabila la Kitutsi.
Baadaye Micombero alimpindua mfalme Ntare V.  Wahutu walinyanyaswa sana. Mwaka 1972 Wahutu walijaribu kujikomboa na kuwaua Watusi 1200.  Watusi walilipiza kisasi kwa kuwaua zaidi ya Wahutu 120,000 wakianza na wasomi.  Zaidi ya waalimu na Makatekista 2,300 Wahutu waliuawa.
Kanisa nchini Burundi lilisimama imara katika majaribu haya, kuna Watutsi wengi walioteseka au kuuawa wakiwalinda Wahutu, na Wahutu vilevile wakiwatetea Watutsi, kati yao wakiwemo Mapadre na Watawa. Hata hivyo hata wale waliokuwa wanaua walikuwa Wakristo.
Mwaka 1976 Jean Baptist Bagaza alimpindua Micombero. Bagaza alichukia Kanisa Katoliki. Aliwafukuza Wamisionari 300, akawafunga Mapadre 20, akapiga marufuku misa za kila siku na vyama vya kitume na kufunga Seminari zote.
Hata hivyo Kanisa liliendelea likitumia ukomavu wa Waamini wake katika kueneza Dini. Kwa wastani Padri mmoja alliwahudumia waamini zaidi ya elfu kumi na tano. Huu ulikuwa wakati mgumu kwa Kanisa, lakini ulilikomaza na kuliimarisha.
Kumekuwepo na  Maaskofu shupavu kama Askofu Simon Ntamwana wa Bujumbura, Mhutu, ambaye alipoteza karibu ndugu zake wote kwa kuuawa na Watutsi lakini bado anapigania amani kwa upendo na utulivu bila kuwa na kisasi.
Mwaka 1987 Pierre Buyoya, naye Mtutsi, alimpindua Bagaza.  Buyoya alikuwa mtu mstaarabu; alifanya amani na Kanisa na kushirikiana nalo, akawaingiza Wahutu katika Serekali yake na kutayarisha uchaguzi mwaka 1993.
Kutokana na uchaguzi huo Mhutu, Melchior Ndadaye, akiongoza chama cha FRODEBU, alichaguliwa kuwa Rais, ila miezi michache baadaye aliuawa na Jeshi la Watutsi lililoasi.  Rais Mhutu aliyemrithi aliuawa katika ndege iliyotunguliwa Rwanda pamoja na Raisi wa Rwanda Habyarimana.
Katika vita vya wenyewe kwa wenyewe, maelfu ya Watutsi na malaki ya Wahutu waliuawa. Mwaka 1996, Buyoya kwa mara nyingine tena alishika madaraka ya serikali na kidogo kuleta hali ya utawala, ingawa mapigano yaliendelea kwa sababu vikundi kadhaa vya Wahutu viliingia vita vya msituni.
Mazungumzo ya maelewano yalisimamiwa kwanza na Mwalimu Julius Nyerere, Raisi mstaafu wa Tanzania, na baada ya kifo chake yakasimamiwa na Mzee Nelson Mandela, Rais mstaafu wa Afrika ya Kusini, ambayo mwaka 2000 yalianza kuzaa matunda, na mwaka 2003 vikundi vikuu vilitia sahihi ya kusitisha mapigano.
Katika uchaguzi wa mwaka 2005 alishinda na kiongozi  waasi Pierre Nkurunziza wa chama cha CNDD-FDD. Ila chama cha Paripehutu, bado kiko msituni kikipigana.
Katika vita hivi Kanisa lilihusika kama mtume wa amani na uelewano, na limejaribu kufanya juhudi nyingi kupatanisha raia. Mwaka 2010 kati ya wakazi milioni nane, asilimia 65 walikuwa Wakatoliki, Waislamu asilimia 10 na Waprotestanti asilimia 5. Asilimia 20 zilizobaki za watu wa dini za asili, wengi wao wakiwa wakereketwa Wakatoliki ambao bado hawajabatizwa.
Uinjilishaji Kongo Brazaville:
Akishindana na Stanley, Sarvagnon de Brazza, aliweza kusimika bendera ya Ufaransa Kaskazini, mwa Mto Kongo na kushika sehemu yote ya Kaskazini na hivyo kuunda koloni za Kifaransa karibu na Ekweta. Koloni hizo zilikuwa Kongo-Brazaville, Gabon, Ubangi Shari (ambayo sasa ni Jamuhuri ya Afrika ya Kati) na Chad. De Brazza alipofanywa mtawala baada ya mkutano wa Berlin, aliwaalika Shirika la Roho Mtakatifu kuunda Vikariati.
Kufikia mwaka 1883 Wamisionari wa Shirika la Roho Mtakatifu walikuwa na misioni imara kwenye mwambao na katika mji wa Brazaville. Augourd alipewa Uaskofu mwaka 1894, na alifanya kazi kubwa ya uinjilishaji hadi alipokufa mwaka 1921.
Wakazi wengi wa Kongo-Braza ni wa kabila la ‘Bakongo’, watu wa dini waliomwita Mungu ‘Nzambi’. Hata leo nyimbo zao nyingi hata za kiraia humtukuza huyo Mungu wao. Kabila hili liko vile vile Kongo Kinshasa. Kutoka n’gambo ya mto kule Kongo-Kinshasa walipokea Wamisionari Waprotestanti kutoka Sweden mwaka 1909.
Kanisa hilo liliendelea vizuri sana. Tangu mwaka 1961 linaongozwa na Waafrika na Waamini wao leo wana asilimia 10 ya wakazi wote. Vile vile, kutoka Kongo Kinshasa walipokea dini ya Wakristo Waafrika ya Kibanguisti.
Kule Kongo Braza vile kulizaliwa dini nyingine za Kikristo za Kiafrika kama dini ya ‘Mungu wa Mshumaa’, na nyingine ya kisiasa iliyotaka kumkomboa Mwafrika kutoka katika ukoloni. Dini hiyo ilianzishwa na Andre Matswa. Matswa alifia gerezani chini ya Wafaransa, lakini Waamini wake wanamwona kama Messiha na wanangojea ujio wake.
Vile vile palikuwepo dini ya ‘kujipiga na Msalaba’ iliyoanzishwa na mkatekista Mkatoliki, Victor Malanda’ ambayo Waamini wake walipakwa mafuta kwa ajili ya kuacha ushirikina. Pia palikuwepo na dhehebu la ‘Jeshi la Wokovu,’ ambao alama yao ni bendera. Dhehebu hili la Wokovu ambalo ni kama maaskari liko katika nchi nyingi hata hapa Tanzania.
Licha ya madehebu mengi, Wakatoliki waliongezeka sana ingawa hawakufadhiliwa sana na serikali kama wenzao wa Kongo-Kinshasa katika kufadhili shule. Mwaka 1960 Kanisa lilimpata Askofu wake wa kwanza Mwafrika, Theophile Mbemba ambaye mwaka 1964 aliteuliwa kuwa Askofu Mkuu wa Brazaville.
Wakati huo Wakatoliki kwa uelekeo au mashabiki walikuwa asilimia 52 ya wakazi wote, wakifuatiwa na Waprotestanti asilimia 27, Makanisa ya kiafrika asilimia 9. Ingawa asilimia ni kubwa, kati yao kuna wengi waliokuwa washabiki tu wa Ukristo bila kujiunga rasmi kwa kubatizwa. Katika Sensa walijiandikisha katika madhehebu hayo. Mwaka 1973 Kongo-Brazaville ilipata Kardinali wake wa kwanza Emile Biayenda.

DAR ES SALAAM

Na Alone Mpanduka

Wiki hii tunaitazama Bendi ya Zaiko Langa Langa ambayo ilizaliwa mwaka 1970 huko nchini Congo DR (zamani Zaire).
Mwanzo kabisa ilijulikana kama Orchestra Zaiko, lakini baadaye likaibuka jina la Langa Langa kufuatia kutumbuiza kwenye vilabu vya pombe. Langa Langa ni Kilingala, kikiwa na maana ya kulewa.
Zaiko inaweza kulinganishwa na bendi ya Msondo Ngoma ya hapa nchini kwa historia zao zinavyokaribiana kwenye ukongwe na kuzalisha wanamuziki wengi mahiri. Msondo Ngoma na Zaiko Langa Langa, zimetoa wanamuziki wengi wenye majina makubwa kimuziki.
Wanamuziki nyota wa nchini humo akina Papa Wemba, Bozi Boziana, Dindo Yogo, Evoloko Ley Ley ‘Joker’, Defao Matumona, Koffi Olomide, na wengine wengi, chimbuko lao limetoka kwenye shina la Zaiko Langa Langa.
Bendi nyingi kama Isifi Lokole, Yoka Lokole, Viva la Musica, Langa Langa Stars, Zaiko Familia Dei, Choc Stars, Le Anti Choc, Le Grand Zaiko Wawa, Quartie Latin na nyinginezo nyingi, zimetoka kwenye chimbuko la Zaiko ambayo sasa inajulikana kama Zaiko Langa Langa Nkolo Mboka, yaani ‘Wakuu wa Mji’.
Idadi kubwa ya bendi zilizotokea ubavuni mwa Zaiko Langa Langa zimekuwa zikijiita ‘Ukoo wa Langa Langa’ (Clan Langa Langa).
Bendi hizo ni Isifi Lokole iliyoanzishwa na Papa Wemba, Bozi Boziana, Evoloko Jocker na Mavuela Somo, Yoka Lokole iliyoanzishwa na Papa Wemba, Bozi Boziana na Mavuela Somo.
Bendi ya Grand Zaïko Wa Wa iliyoanzishwa na Felix ‘Pepe’ Manuaku Waku aliyeungana na Shimita El Diego na Djo Poster. Bendi ya Viva La Musica iliyoanzishwa na Papa Wemba akiwa na Emeneya Mubiala na Theodore Djangi Dindo Yogo.
Bendi ya Choc Stars iliyoanzishwa na wanamuziki akina Bozi Boziana, Tshimpaka Roxy na kuungana na akina Ben Nyamabo, Carlito Lassa, na Defao Matumona.
Bozi Boziana akiungana na Deyesse Mukangi, Jolie Detta, Dodoli, Walingonda, Fifi Mofude, na wengineo, waliungana na kuanzisha bendi ya L’Orchestre Anti-Choc.
Langa Langa Stars iliyoanzishwa na Waze la Mbongo Kiamuangana Mateta ‘Verckys’, Evoloko Jocker, Tshimpaka Roxy, Emeneya Mabiala na Djo Mali.
Zaiko Langa Langa Familia Dei, ilianzishwa na akina Lengi Lenga, Ilo Pablo, Bimi Ombale, Beniko Popolipo, Petit Poisson, na Djimi Yaba.
Zaïko Langa Langa Nkolo Mboka yenyewe chini ya N’Yoka Longo, Meridjo, Oncle Bapius, Zamuangana, Nono Atalaku, Mbuta Matima, Malage de Lugendo, Adamo Ekula, Baroza, na Shiro Shiro, ikaanzisha bendi zingine za Zaiko Universel chini ya wanamuziki Meridjo na Oncle Bapius Muaka wakati bendi ya Langa Langa Rénove ikiongozwa na mwanamzuiki Evoloko Jocker.
Histori ya bendi ya Zaiko Langa Langa imekuwa ikikosolewa na baadhi ya watu, wakitaja kwamba ilianzishwa mwaka 1970.
Inasadikika kwamba bendi hiyo ilianzishwa rasmi Desemba 24 mwaka 1969 jijini Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, wakati huo ikijulikana kama Orchestra Zaiko.
Wakati huo muziki wa Kongo ulitawaliwa zaidi na bendi za African Jazz ya Joseph Athanase Tchamala Kabaselleh ‘Le Grand Kalle’, African Fiesta ya Nicolas Kassanda wa Mikalay maarufu kama Dk. Nico, Tout Puisant Orchestre Kinnie Jazz (TP OK Jazz) ya L’Okanga La Ndju Pene Luambo Luanzo Makiadi Franco na hata African Fiesta National ya Pascal-Emmanuel Sinamoyi Tabu, maarufu Tabu Ley Rochereau, aliyoianzisha baada ya kutengana na Dk. Nico na mwaka 1970 akaibadili jina na kuiita Orchestre Afrisa Intanationale.
Waanzilishi wa Zaiko Langa Langa walikuwa wanamuziki ambao baadhi walikuwa wanapigia bendi ndogo ndogo za mitaani, na wengine walikuwa wanafunzi.
Baadhi yao ni mpiga Konga maarufu D.V. Moanda, ambaye jina lake halisi ni Vital Moanda-di Veta Marcelin Delo, Henry Mongombe, Olemi Eshar-Eshar dem’belina, Andre Bita, Mavuela ‘Somo’ Simeon, Evoloko Lay Lay ‘Joker’, Teddy Sukami, Oncle Bapius aliyekuwa akipiga bass, Zamuangana Enock le Meilleur, baba ya wapiga solo wa kizazi kipya Kongo Felix Manuaku Waku na N’Yoka Longo Mvula, anayejulikana kama Jossart, ama Vieux Mbombas ambaye asili yake ni kutoka nchini Angola.
Hawa walikuwa wakipiga muziki wa Soukous. Katika upande wa Pop waliokuwa wakifungua pazia katika shoo zote za bendi hiyo, kulikuwa na akina Bimi Ombale, Mbuta Matima Zephirin na Mashakado Mbuta.
Hiyo ndiyo Zaiko Langa Langa, bendi kongwe nchini humo kwa sasa ambayo bado inaendelea kujikongoja, licha ya wanamuziki wengi kuondoka.
Ikumbukwe kwamba Januari mwaka huu, alifariki Nono Monzuluku ambaye alijiunga na Zaiko Langa Langa mwaka 1982 akiwa na miaka 22 tu. Baadaye bendi (Zaiko) iliongeza rapa mwingine (Doudou Adoula) miaka ya 1980 katikati kuelekaa mwishoni.
Bendi inahesabika kama Chuo cha Muziki katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kwa sababu bendi nyingi zinazotamba hivi sasa, ambazo zilianzishwa kuanzia miaka ya 1970, zimetoka ubavuni mwake.

MANCHESTER, Uingereza
Meneja wa Manchester United, Erik ten Hag amesema kuwa kocha wa zamani wa muda Ralf Rangnick alikuwa sahihi kabisa kwamba klabu hiyo inahitaji kufanyiwa upasuaji wa moyo.
Ten Hag (54), aliteuliwa kuwa meneja mnamo 2022 baada ya Rangnick kutawala kwa miezi saba.
Mjerumani huyo ambaye kwa sasa anainoa timu ya Taifa ya Austria, aliiongoza United hadi nafasi ya sita kwenye Premier League, lakini alishinda mechi 11 pekee kati ya 29 alizocheza.
Ten Hag ambaye alitia saini nyongeza ya mkataba wa mwaka mmoja mwezi huu, alisema kwamba uchambuzi wa Rangnick ulikuwa sahihi.
“Rangnick alikuwa sahihi kabisa,” Ten Hag alisema katika mahojiano na gazeti la Uholanzi AD Sportwereld.
“Tumekuwa tukifanya kazi kwa bidii juu ya hili kwa miaka miwili, lakini alilosema ni sawa kabisa: ni operesheni ya kina, ngumu sana. Na nilipoanza nilijua kuwa itakuwa kazi ngumu.”
United wamefanyiwa mabadiliko makubwa nje ya uwanja tangu Sir Jim Ratcliffe apate asilimia 27.7 ya hisa za klabu hiyo Desemba mwaka jana.
Omar Berrada, Dan Ashworth, Jason Wilcox na Christopher Vivell wote wamejiunga katika nyadhifa katika ngazi ya bodi mwaka huu, wakati klabu imetoa £50m kuboresha uwanja wa mazoezi.

DAR ES SALAAM

Na Alone Mpanduka

Katika nchi ya Finland kuna mashindano ya kukimbia riadha, huku ukiwa umemmeba mkeo mgongoni. Mashindano hayo yalianza mnamo karne ya 19, na kuwa mchezo rasmi mwaka 1992, huku baadaye wakiruhusu raia wa nchi zingine kushiriki mwaka 1995.
Mchezo huo ambao umetokea kupendwa na wengi hadi kupewa hadhi ya Kimataifa, unahusisha wapenzi au wanandoa na lazima mke atakayebebwa awe wa mwanaume husika.
Pamoja na hayo, mwanamke atakayebebwa atatakiwa kuwa na uzito usiopungua kilo 49, na kama itakuwa pungufu, basi itabidi afungashiwe mzigo ili uzito wake ufikie kilo 49.
Sheria inasema wenza wawe na zaidi ya miaka 18, na uzito wa kilo 50 na kuna adhabu ikiwa utamuangusha mwenza wako.
Mshindi hupatikana kwa mwanaume aliyeweza kukimbia kwa kasi zaidi na mkewe kichwani, na zawadi kuu ambayo ni pombe, itatolea kwa katoni sawa na uzito wa mke wake kwa kutumia mzani maalum yaani ‘bembea’.
Wazungu wameupa mchezo huo jina la Kiingereza la ‘Wife Carrying Competition’. Si kwamba mtu hubeba mke wake, bali mwanamume hubeba mwanamke na kuanza mbio akiwa naye.
Mwanamke huyo huwa ni mwanatimu mwenza wa manamume. Mashindano haya hufanyika na kupendwa sana Finland, na ratiba yake ni Julai ya kila mwaka.
Kwa kawaida mwanaume mchezaji hutakiwa kukimbia na mzigo huo wa mwanamke umbali wa mita 254, akiwa kamuweka ama mgongoni au mabegani.
Kuna changamoto kadhaa kwenye mchezo huo, kwani maeneo ya kukimbia si tambarale, kuna maeneo yenye maji na matope na mengine makavu lakini ya milima.
Mshindi wa mashindano hayo huzawadiwa simu ya mkononi, na mke hupewa bia, na anayeshika nafasi ya mwisho anapatiwa tambi na chakula cha mbwa.
Wazo la kuanzisha shindano hilo lilipatikana mnamo karne ya 19 kupitia matukio ya kihalifu ya mtu mmoja aitwaye Ronkainen ambaye aliwashawishi vijana wenzake kuiba na kubeba gunia la mbegu ama kumbeba nguruwe na kukimbia naye.
Inaelezwa kwamba jamaa huyo alikuwa mwizi aliyeishi karibu na mwanzo wa karne ya 19, yeye pamoja na genge lake, walishambulia vijiji vya karibu na kuiba mizigo mikubwa na kisha kukimbia nayo wakiwa wameibeba kichwani.
Genge lake la uhalifu liliiba chakula na wake za watu kutoka vijijini, na kisha kuwabeba migongoni huku wakikimbia.
Mwanamume huyo aliwapa changamoto watu wake kuonyesha nguvu zake, kwanza kubeba mizigo, na pili kukimbia nayo.

PARIS, Ufaransa
Klabu ya Paris Saint-Germain (PSG) ya Ufaransa, inataka kumsajili mshambuliaji wa Manchester United ya Uingereza, anayecheza kwa mkopo katika klabu ya Borussia Dortmund ya Ujerumani, Jadon Sancho.
PSG ilisema kuwa kuhusu raia huyo wa Uingereza, bado hakuna mbinu rasmi, lakini upande wa Ligue 1 umechunguza masharti ya makubaliano.
Juventus na Borussia Dortmund bado wana hamu ya kumsajili Sancho, ingawa kwa jinsi mambo yalivyo, hawawezi kufikia thamani ya United.
Sancho amerejea kwenye mazoezi na kikosi cha kwanza cha United na anatarajiwa kuwa sehemu ya kikosi kitakachosafiri kuelekea Marekani kwa ajili ya ziara ya kujiandaa na msimu mpya wa klabu hiyo.
Meneja wa Manchester United Erik ten Hag alifanya mkutano chanya na Sancho huko Carrington mapema mwezi huu, huku akilenga mchezaji huyo kushiriki kikamilifu katika maandalizi ya msimu mpya.

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Klabu ya soka ya Simba imesema kuwa kinachoendelea hivi sasa katika sajili zao za wachezaji wa Kitanzania, ni sehemu ya hujuma za kuwachafua ili waonekane hawajui wanachokifanya.
Hivi karibuni Klabu za Coastal Union ya Tanga, Geita Gold ya Geita, na KMC ya Kinondoni, kwa nyakati tofauti zilikuja juu zikipinga sajili za wachezaji wake waliosajiliwa na wekundu hao kwamba hazikuwa halali kwa sababu wachezaji bado wana mikataba nao.
Simba ilimtangaza beki Lameck Lawi kutoka Coastal Union kwamba imemsajili, kisha Valentino Mashaka wa Geita Gold, pamoja na Awesu Awesu wa KMC, lakini hadi sasa imeonekana kukwama kwa Lawi, huku wengine ikiwanasa kwa tabu.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa wekundu hao wa Msimbazi, Ahmed Ally alisema kuwa wanahisi kuna jambo linaendelea, kwa sababu haiwezekani usajili wa wachezaji wa ndani uonekane una makosa, halafu wa wachezaji wa nje uonekane hauna dosari.
“Simba hatujawahi kukosea katika eneo la usajili, na ndiyo maana hata siku moja huwezi kusikia mchezaji katupeleka FIFA kisa anatudai. Tunafanya mambo yetu kwa weledi mkubwa. Leo hii haiwezekani tusajili wachezaji kutoka nje ya Tanzania bila malalamiko halafu ikitokea tunasajili mchezaji kutoka Geita au Kinondoni tu hapo, ikaja kuonekana hatukufuata utaratibu. Hizi ni namna za kutuchafua,” alisema.
Alisema kuwa wamesajili wachezaji wapatao nane wa Kimataifa, lakini hakuna klabu yoyote kutoka nje iliyoibuka kuzungumzia makosa ya usajili kwa wachezaji hao.
Simba imefanya usajili wa wachezaji 13 hadi sasa, ambao ni Lameck Lawi kutoka Coastal Union, Joshua Mutale kutoka Power Dynamos, Steven Dese Mukwala kutoka Asante Kotoko, Jean Charles Ahoua kutoka Stella Club d’Adjamé na Abdulrazack Mohamed Hamza kutoka Super Sport United.
Wengine ni Valentino Mashaka kutoka Geita Gold FC, Augustine Okejepha Kutoka Rivers United, Debora Fernandes Mavambo Kutoka Mutondo Stars, Omary Omary Kutoka Mashujaa FC, Karaboue Chamou Kutoka Racing Club d’Abidjan, Valentin Nouma kutoka St. Eloi Lupopo, Yusuph Kagoma kutoka Singida Black Stars FC na Kelvin Kijili kutoka Singida Fountain Gate.
Dirisha la usajili kwa Ligi Kuu soka Tanzania Bara, Ligi ya Championship, First League na Ligi Kuu ya Wanawake msimu wa 2024/25 ambalo lilifunguliwa Juni 15, litafungwa Agosti 15 mwaka huu, ikiwa ni siku moja kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu Tanzania Bara.

DAR ES SALAAM

Na Mathayo Kijazi

Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini chini ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (Tanzania Episcopal Conference: TEC), wanmekutana katika Mkutano wao Mkuu, huku changamoto za kichungaji, ikiwemo kumomonyoka kwa maadili, zikichukua mjadala mkubwa.
Kwa upande wake Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Tabora, Mwadhama Protase Kardinali Rugambwa, amesema kuwa ni vyema kutafakari vema, kama yote yanayoigwa katika Ulimwengu, yanastahili kuigwa ili kuenenda Kiibada na Kiliturujia.
Kardinali Rugambwa alisema hayo wakati akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Maaskofu, uliojadili mambo mbalimbali yanayolihusu Kanisa, Mada kuu ikiwa ni ‘Kuchagiza Hatima ya Waamini Wakatoliki: Changamoto ya Kichungaji katika Maadhimisho ya Miaka 60 ya Lumen Gentium (Mwanga wa Mataifa), uliofanyika Makao Makuu ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Kurasini jijini Dar es Salaam.
“Ukitazama baadhi ya mambo yanayoendelea katika Ulimwengu huu, utaona kuwa ni mengi sana. Kwa hiyo tutafakari kwamba, je, yote yanayoigwa katika ulimwengu huu, yanastahili kuigwa ili kuenenda Kiibada na Kiliturujia?
Binadamu wahama misingi ya Imani:
Akizungumzia juu ya mada hiyo kuhusu Changamoto ya Kichungaji katika Maadhimisho ya Miaka 60 ya Lumen Gentium (Mwanga wa Mataifa), Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Arusha, Mhashamu Isaac Amani, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kurugenzi ya Kichungaji, alisema kuwa binadamu wengi wamehama katika misingi ya kiimani, jambo linalosababisha machafuko na ukosefu wa hali ya amani.
Askofu Amani alisema kwamba uwepo wa Watakatifu, ni mwaliko mama, ambao kila mmoja anatakiwa kuufuata ili kuleta tunu ya kiulimwengu.
Wazazi chanzo kubomoka maadili:
Naye Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Henry Mchamungu, akichangia mada kuhusu changamoto hizo, alisema kuwa wazazi wanachangia kwa namna fulani watoto kutokuwa na maadili, kwani hawana muda wa kutosha kukaa nao na kujua tabia zao.
“Wazazi wengi hawana muda wa kukaa na kufuatilia mwenendo na tabia za watoto wao, kwa sababu utaona wazazi wanatoka alfajiri kwenda kazini kabla watoto hawajaamka, halafu wanarudi usiku sana, muda ambao watoto wameshalala,” alisema Askofu Mchamungu.
Usafirishaji haramu Binadamu mwiba:
Naye Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi aliwataka wananchi wanaokwenda kufanya kazi katika Mataifa ya mbali kuwa makini, kwani wengi huambulia manyanyaso wanapofika katika Mataifa hayo.
Askofu Mkuu Ruwa’ichi alitoa rai hiyo wakati akichangia mada kuhusu nini kifanyike, katika kupunguza changamoto zinazowakumba watu mbalimbali, hasa suala la biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu.
“Mwezi uliopita nilisafiri kwenda Adis Ababa, Ethiopia, nilipofika kwenye ndege, nikakutana na wanawake ambao nao walikuwa wanasafiri, nikawauliza ‘mnakwenda wapi?’ wakajibu ‘Muscat’, walisema kwamba wametafutiwa kazi huko wanakwenda kufanya;
“Mimi nikawaambia ‘kuweni makini na hizo kazi mlizoitiwa huko, na mkifika huko msikubali kumpa mtu yeyote Passports zenu, kwa sababu mkiwapa watu Passports zenu, mkifanyiwa jambo baya hamtaweza hata kutoroka,” alisema Askofu Mkuu Ruwa’ichi.
Kwa upande wake Sista Digna Chuwa -CPS, Mratibu wa Mradi wa Taasisi ya TCAS, aliyetoa mada ya usafirishaji wa binadamu, alisema kuwa ipo haja ya kushirikiana na jamii kuzuia biashara haramu ya usafirishaji binadamu, kwani hali hiyo huanzia katika familia.
Vyombo vya Kanisa kunasua mtanziko:
Akichangia kuhusu nini kifanyike, Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Stephano Musomba alisema kuwa vyombo vya habari vya Kanisa, ni vyema vikatumika ipasavyo, kuandaa vipindi vitakavyosaidia kutoa mafundisho ya imani.
Askofu Kilaini agusia Mtaguso:
Kwa upande wake Askofu Mstaafu wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Mhashamu Method Kilaini alisema kuwa lengo la kuwepo na Mtaguso ni kwenda na wakati, na kuweka vizuri Kanisa kuwa na usawa.
Aliongeza kuwa miongoni mwa malengo hayo, ni pamoja na kutengeneza umoja na kuunganisha urika wa Kanisa zima, mambo ambayo yalichagizwa na Baba Mtakatifu kwa ajili ya kuleta amani ndani ya Kanisa.
Akitoa neno la kufunga Mkutano huo wa Maaskofu, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania,aliyemaliza muda wake, Mhashamu Gervas Nyaisonga, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya, aliwashukuru wote walioshiriki mkutano huo, akisema kwamba anaamini kwamba yote yaliyojadiliwa, yatakuwa msaada katika suala zima la Kichungaji.

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Wakatoliki wametakiwa kumtangaza Bwana Yesu Kristo mahali popote, bila uwoga sehemu yoyote na bila kujali jambo lolote na kuacha tabia ya kusaka miujiza.
Wito huo ulitolewa hivi karibuni na Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Ambrosi IPTL, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Padri Paul Sabuni katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Dominika, iliyofanyika katika Parokia Teule ya Utatu Mtakatifu Skaska, IPTL –Salasala jimboni humo.
“Mkristo yeyote inampasa kumtangaza Kristo popote pale anapokuwepo bila uwoga, kwani hiyo ni njia bora zaidi katika maisha yenu ya kila siku,”alisema Padri Sabuni.
Alisema pia kuwa Waamini wa Parokia hiyo Teule wanatakiwa kuwa na Imani thabiti, isiyo suasua hasa katika kuitangaza Injili.
Aliendelea kusema kwamba watu wengi sasa wamekuwa waoga kuzungumza habari za Yesu Kristo, hata kufundisha habari njema.
“Msije mkatetereka kwa kumwogopa mtu yeyote, kwani mkifanya hivyo mtakuwa mmetenda dhambi kubwa ya makusudi kabisa, kutokana na uwoga ndani mwenu wa kumtangaza Kristo,”alisema Padri Sabuni.
Awakanya wasaka miujiza:
Aidha Padri Sabuni, alisema kuwa watu wengi wamekuwa wakitangatanga, kutafuta miujiza na kujikuta wakiingia katika sehemu zisizofaa.
Alibainisha kwamba watu wanaopenda miujiza ni watu wenye imani ndogo, akiwasihi Wakatoliki kuishika imani yao.
“Yesu Kristo alisema kwamba katika siku za mbeleni watakuja manabii wengi wa uwongo,basi inawapasa mtambue  kwamba ndio hao wanaowatangazia miujiza kwa sasa,”alisema.
“Inawapasa kushika Imani moja ya Kanisa Katoliki, ambalo lina miujiza, imani kamilifu na muachane na kutangatanga katika madhehebu tofauti, mkifanya hivyo, wewe kama Mkatoliki unamkata Yesu Kristu,”alisema Padri Sabuni.
Padri sabuni pia aliwaomba Waamini wa Parokia hiyo kuchangia Tumaini Media ambayo ina vyombo vitatu navyo ni televisheni Tumaini Radio Tumaini pamoja na gazeti la Tumaini Letu ili Kituo hicho kiweze kupanua wigo wake katika Uinjilishaji.

DODOMA

Na Mwandishi wetu

Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI), limesema kuanzishwa kwa ada ya kuendeleza viwanda kwa bidhaa zinazotoka nje kwenye Bajeti Kuu ya Serikali, kutasaidia kulinda viwanda vya ndani, kuchochea uwekezaji, na kuongeza mauzo ya nje.
Mkurugenzi wa Shirikisho hilo, Leodegar Tenga alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maoni ya wenye viwanda waliojadili bajeti hiyo.
Alisema kuwa hatua ya serikali kupunguza ada na tozo zinazotolewa na wakala wa udhibiti ili kupunguza gharama za uzalishaji, kupunguza ushuru wa forodha wa malighafi za viwandani na pembejeo za uzalishaji, kutaongeza ushindani wa viwanda vya ndani.
Tenga alisema kwamba kuondoa kodi ya ongezeko la thamani kwa bidhaa za nguo zinazotengenezwa kwa pamba inayolimwa nchini kutachochea uwekezaji katika tasnia ya nguo nchini.
“Hatua za kodi zilizopendekezwa hapo juu zinalenga kusaidia viwanda vya ndani katika kupunguza gharama za uzalishaji, kuhimiza matumizi ya nyenzo za ndani, kuongeza ushindani, na kukuza ukuaji wa uchumi,” alisema Tenga.
Tenga alipongeza bajeti kuu ya Serikali kwa kuweka mambo muhimu ambayo yatachochea ukuaji wa viwanda nchini.
Alibainisha kuwa Serikali imekuwa sikivu kwa wenye viwanda na kila wanapokuwa na jambo, wamekuwa wakifunguliwa milango ya majadiliano, na kwamba hakuna jambo la wenye viwanda ambalo linakwama.
Tenga aliendelea kusema wenye viwanda wamefurahia sana bajeti ya serikali kwa kuzingatia uendelezaji wa miradi ya kimkakati kama reli ya kisasa (Standard Gauge Railway: SGR) ambayo alisema itasiadia kwa kiwango kikubwa kukuza viwanda vya ndani katika kuzalisha kwa wingi bidhaa.
Azungumzia mradi SGR
Tenga alisema kwamba miradi kama SGR inasaidia kukuza uchumi, kwani viwanda vitazalisha kwa wingi na bidhaa kusafirishwa kwa urahisi kwa haraka tofauti na sasa ambapo usafirishaji umekuwa ukisababisha bei kupanda.
“Nchi ambayo iko makini, inaendeleza miradi mikubwa kama ya ujenzi wa reli, barabara, miradi ya maji kama kuendeleza miradi ya kimkakati ya barabara maji, bandari kwa sabbau huwezi kuendeleza viwanda kama huna umeme au una matatizo ya usafirishaji,” alisema Tenga.
Tenga alifahamisha kwamba bajeti ya mwaka huu inakusudia kuhamasisha mapato ya ndani zaidi ikilinganishwa na bajeti ya 2023/24.
Kwa mujibu wa Tenga, jambo muhimu katika bajeti ya mwaka huu ni Serikali kufanya mageuzi mbalimbali ya muundo wa kodi, ada, tozo na marekebisho ya sheria na kanuni ili kuboresha mazingira ya biashara.
Alisema pia kuwa marekebisho ambayo yamependekezwa kuhusiana na sekta ya viwanda ni katika ongezeko la thamani VAT, ushuru wa bidhaa, ada na tozo za wakala, pamoja na ushuru wa forodha.
Tenga amesema kuwa baadhi ya hatua chanya, ni pamoja na kuanzishwa kwa tozo ya maendeleo ya viwanda kwa bidhaa zinazotoka nje, yenye lengo la kulinda viwanda vya ndani, kuchochea uwekezaji na kuongeza mauzo ya nje; kupunguza ada na tozo zinazotolewa na vyombo vya udhibiti, ili kupunguza gharama za uzalishaji.
Amesema pia kuwa wamefurahishwa na kupunguzwa kwa ushuru wa forodha kwenye malighafi za viwandani na pembejeo za uzalishaji, ili kuongeza ushindani wa viwanda vya ndani na kutozwa ushuru wa VAT kwenye bidhaa za nguo zinazotengenezwa kwa pamba inayolimwa hapa nchini ili kuchochea uwekezaji katika viwanda vya nguo vya ndani.
Alisema hatua za kodi zilizopendekezwa hapo juu zinalenga kusaidia viwanda vya ndani katika kupunguza gharama za uzalishaji, kuhimiza matumizi ya vifaa vya ndani, kuongeza ushindani, na kukuza ukuaji wa uchumi.

MOROGORO

Na Mwandishi wetu

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Business Reguratory and Licesing Authority: BRELA), umetaja siri ya mafanikio yake yanayosaidia kufanya kazi zake bila kusabababisha usumbufu.
Mkurugenzi wa Leseni BRELA, Andrew Mkapa,alisema hayo wakati akitoa mada kuhusu utoaji wa leseni za biashara Kundi A.