Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Sesilia-Kisarawe II, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Padri Rodger Kamuzinzi (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Utume wa Wanaume Katoliki (UWAKA) parokia hiyo baada ya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa kanisa jipya parokiani hapo.
Kansela wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Padri Hamilton Kikoti (katikati), Mapadri, Masista na Frateri wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Halmashauri ya Walei Parokia ya Bikira Maria wa Rozari Takatifu - Makongo Juu baada ya adhimisho la Misa Takatifu ya Sakramenti Takatifu ya Kipaimara iliyoadhimishwa parokiani hapo. Kulia ni Paroko wa Parokia hiyo, Padri Musa Kihoo.
Dominika iliyopita parokiani kwetu tulitembelewa na Frateri aliyekuja kutangaza kitabu alichokiandika kinachohusu falsafa.
Falsafa, ambayo uhusisha mpangilio wa kufikiri, ni sehemu muhimu kwenye maisha ya wakatoliki ndio maana Frateri ambaye amesoma pia teolojia anaona umuhimu wa kuandika kitabu hicho.
Ndio sababu pia kwa ujasiri anasimama kwenye mimbari na kukitangaza. Hivyo hivyo haishangazi Padri aliyeongoza Misa anaposisitiza tangazo hilo kwa waamini.
Kuweka jitihada ya kutumia akili na maarifa ni njia mojawapo muhimu ya kuinjilisha na kuyatakatifuza malimwengu. Kwa bahati mbaya wakati mwingine tunashindwa kutumia akili zetu kwa manufaa ya Kanisa na kujiliwaza kwamba pengine kutotumia akili ni unyenyekevu. Galileo Galilei alikuwa sahihi kutoamini kuwa Mungu aliyetujalia kipawa cha akili alikusudia tusikitumie.
Kutotumia vema akili zetu ni kukiuka “kanuni ya dhahabu” tuliyopewa ambayo inatuhimiza kumpenda Mungu pamoja na mambo mengine, kwa akili zetu zote.
Sisi ni wana wa nuru lakini kushindwa kutumia akili zetu kunasababisha; “wana wa ulimwengu huu katika kizazi chao wenyewe huwa na busara kuliko wana wa nuru” (rej: Lk 16:8b).
Bwana wetu Yesu Kristo hakutuamuru tuwe wapole kama hua tu, bali alitutaka pia tuwe na busara kama nyoka (rej Mathayo 10:16). Mara nyingi, pengine, msisitizo unawekwa zaidi kwenye sehemu ya upole kuliko ya busara.
Inawezekana ikaonekana kuwa ni rahisi zaidi kuishi bila kutumia akili kwa kuwa matumizi ya akili ni zoezi gumu ambalo wengi wetu tungependa kuliepuka. “Mwanadamu atatumia kila aina ya ujanja kuepuka mzigo wa kufikiri,” ndivyo anavyosema mgunduzi maarufu, Thomas Edison.
“Ukilinganisha na tunavyopaswa kuwa” anaandika Profesa William James wa Harvard. “Ikilinganishwa na jinsi tunavyopaswa kuwa, sisi ni kama watu walioamka nusu tu. Moto wetu umepunguzwa nguvu na mtiririko wa hewa unaohitajika kuchochea moto huo umezuiwa.
Tunatumia sehemu ndogo tu ya uwezo wetu wa kiakili na kimwili. Kwa ujumla, mwanadamu huishi akiwa anatumia sehemu ndogo sana ya uwezo wake halisi; anamiliki aina mbalimbali za nguvu ambazo mara nyingi hushindwa kuzitumia”.
Jitihada hii ya kuepuka “mzigo wa kufikiri” ndiyo inayochangia sisi waamini kushiriki katika baadhi ya matendo ambayo si tu yanatuingiza dhambini, lakini pia yanadhalilisha utu wetu. Mathalani ni aibu iliyoje katika karne ya sasa bado kuna wakatoliki wanaoamini hadithi za kishirikina zisizoingia akilini.
Mtume Paulo anaonya dhidi ya tabia ya kutumia akili zetu “kitoto” bila kufikiri kwa utulivu unaowapasa watu wazima. Anawaandikia Wakorintho: “Ndugu zangu, msiwe watoto katika akili zenu, lakini katika uovu mgeuzwe watoto wachanga, bali katika akili zenu mkawe watu wazima” (1 Kor 14: 20).
Umoja wa Mataifa (UN) unaeleza kwamba amani ni zaidi ya kutokuwepo kwa vita.
Hali hii inahusiana kwa karibu na usalama, utu, heshima na haki msingi za binadamu, fursa sawa; ushirikiano na mshikamano wa udugu wa kibinadamu na ni muhimu katika kushughulikia changamoto zinazoikabili Jumuiya ya Kimataifa.
Maadhimisho ya mwaka 2026 yanatoa kipaumbele maalum kwa “wajenzi wa amani wa kila siku”: Watu wanaohamasisha hatua za kijamii, kuimarisha mshikamano wa kijamii na kuchangia katika amani.
Septemba 21, mwaka huu, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Amani Kimataifa iliyoanzishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa tangu mwaka 1981 na kutengwa ambapo kuanzia mwaka 2001, imekuwa ni kama kipindi cha kujitolea kwa kutotumia nguvu na hivyo kusitisha mapigano.
Kaulimbiu ya mwaka 2026 ni “Wekeza katika Amani: Kwa Kila Mtu, Kila Mahali, Kila Siku”, “Invest in Peace For Everyone, Everywhere, Every Day” ikitoa wito kwa watu binafsi, taasisi na jamii kutambua amani kama jukumu la pamoja na kuchangia katika kuiendeleza katika maisha ya kila siku.
Umoja wa Mataifa unasisitiza kuwa amani ni zaidi ya kutokuwepo kwa vita.
Hii inahusiana kwa karibu na usalama, utu, heshima na haki msingi za binadamu, fursa sawa; ushirikiano na mshikamano wa udugu wa kibinadamu na ni muhimu katika kushughulikia changamoto zinazoikabili Jumuiya ya Kimataifa.
Hivyo, maadhimisho ya mwaka 2026 yanatoa kipaumbele maalum kwa “wajenzi wa amani wa kila siku”; watu wanaohamasisha hatua za kijamii, kuimarisha mshikamano wa kijamii na kuchangia katika kujenga amani ya kudumu kuanzia ngazi ya chini kabisa.
Amani haipatikani tu kupitia katika majadiliano ya Kimataifa au makubaliano ya kisiasa.
Amani ya kweli inajengwa pia madarasani, mitaani na katika jamii, popote ambapo watu hukutana kwa uwazi, katika mazungumzo na kwa kuheshimiana na kuthaminiana kama binadamu.
Kwa muktadha huu, kuendeleza amani kunahusiana kwa karibu na kulinda haki msingi za binadamu, usawa, utu sanjari na kukomesha kabisa sera za kibaguzi.
Umoja wa Mataifa pia unakazia umuhimu wa kujenga na kudumisha amani. Tume ya Umoja wa Mataifa ya Kujenga Amani, iliyoanzishwa mwaka 2005, ikishirikiana na Ofisi ya Kusaidia Ujenzi wa Amani pamoja na Mfuko wa Kujenga Amani, inaunga mkono juhudi zinazolenga kuzuia na kutatua migogoro pamoja na kukuza haki, maridhiano, haki msingi za binadamu na usawa wa kijinsia.
Mfuko wa Kujenga Amani umesaidia miradi mbalimbali katika nchi zaidi ya 70. Siku ya Kimataifa ya Amani kwa mwaka 2026, inatoa wito kwa kila mtu kuchukua hatua madhubuti za kuunga mkono amani; kuwasaidia wengine, kutetea mabadiliko chanya, kuandaa mazingira ya majadiliano na kutumia majukwaa ya mawasiliano kueneza ujumbe wa amani na matumaini.
Hatua hizi za kila siku huchangia katika juhudi pana zaidi za kujenga jamii zenye amani zaidi, zinazojumuisha watu wote na zenye haki.
Hivyo, Siku ya Kimataifa ya Amani ni fursa ya kusisitiza tena kuwa amani na haki msingi za binadamu huimarishana na kwamba kujenga utamaduni wa amani kunahitaji ushiriki wa kila mtu, popote pale alipo na kwamba huu ni mchakato wa kila siku.
Dar es Salaam
Na Violet Tillya
Waamini wa Kanisa Katoliki katika Jimbo Kuu la Dar es Salaam, wameadhimisha Sikukuu ya Kutukuka kwa Msalaba Mtakatifu kwa sala, maombi, vifijo, nderemo na matumaini, licha ya changamoto za kiuchumi zinazowakabili wananchi.
Kwa mujibu wa mafundisho na mapokeo ya Kanisa, Sikukuu ya Kutukuka kwa Msalaba huadhimishwa Septemba 14 kila mwaka. Sikukuu hii pia inahusishwa na kumbukumbu ya kupatikana kwa Msalaba wa Yesu Kristo na Mtakatifu Helena, mama wa Kaisari Konstantino, katika karne ya nne na baadaye kuwekwa katika eneo la Yerusalemu.
Hata hivyo, kutukuza Msalaba si kuabudu mbao, bali ni kumtukuza Kristo aliyekufa na kufufuka juu ya Msalaba huo. Kama ilivyoandikwa katika Injili ya Yohane 12:32: “Nami nikiwa juu nitawavuta watu wote kwangu.”
Waamini wakusanyika Pugu
Jumamosi ya Septemba 12, 2026, mamia ya waamini kutoka Parokia mbalimbali ndani ya Jimbo Kuu la Dar es Salaam, walikusanyika katika Kituo cha Hija Pugu kwa ajili ya kusherehekea Sikukuu ya Kutukuka kwa Msalaba Mtakatifu.
Maadhimisho hayo yaliambatana na Adhimisho la Misa Takatifu iliyoongozwa na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mhashamu Henry Mchamungu.
Akizungumza katika mahubiri yake, Askofu Msaidizi Mchamungu aliwakumbusha waamini maana halisi ya Msalaba katika maisha ya Mkristo.
Sikukuu hii inahusishwa na kupatikana kwa Msalaba wa Yesu Kristo, tukio linalohusishwa na Mtakatifu Helena, ambaye alikuwa mama wa Kaisari Konstantino. Kipindi cha utawala wa Konstantino kilifungua njia kwa Wakristo wa wakati huo kuabudu kwa uhuru zaidi baada ya kipindi kirefu cha mateso chini ya baadhi ya watawala wa Kirumi.
Askofu Mchamungu aliwataka waamini kutambua kwamba Msalaba si hirizi ya kuvaa kwa ajili ya kujilinda dhidi ya magonjwa, mabalaa au matatizo mbalimbali. Badala yake, Msalaba ni ishara ya imani inayowaalika waamini kutafakari maisha ya Kristo na kuishi mafundisho yake katika maisha yao ya kila siku.
“Msalaba ulio mzito kwetu sisi waamini ni wa kusamehe hata pale ambapo ni pagumu. Ukiweza kufanya hivyo, kwa kweli hapo ndipo utakapokuwa umebeba msalaba wako katika imani. Kumsamehe yule aliyekujeruhi ni jambo gumu, lakini hatuna budi kufanya hivyo.
“Ujumbe wa Kikristo si kwamba mateso ni mazuri yenyewe na hivyo tuyatafute. Yanapotujia, tuyabebe pamoja na Kristo. Kristo aliyabeba katika ubinadamu wake. Alijua yatakayotokea; atateswa na atakufa. Lakini sioni mahali katika Maandiko Matakatifu aliposema, ‘Jamani, nisulubisheni’. Alijua hayo yangetokea.
“Anasema: ‘Njooni kwangu ninyi nyote mnaosumbuka na kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha’. Kwa hiyo, mateso unayokutana nayo yabebe pamoja na Kristo, nawe utapata faraja kwake.”
Aidha, Askofu Mchamungu alieleza kuwa kufanya Ishara ya Msalaba ni namna ya kutangaza imani ya Mkristo.
“Tunapofanya Ishara ya Msalaba tunatangaza imani yetu na kusema: Mimi ni wa Kristo. Ninaamini katika kifo na ufufuko wake. Msalaba unatukumbusha kuwa upendo wa Kikristo si wa maneno tu.”
Katika safu hii ya Chimba Chimba Historia ya Kanisa wiki
iliyopita, tulianza kuwaletea historia ya Mtaguso Mkuu wa Trento uliokutana katika kipindi ambacho Kanisa lilikuwa na changamoto. Leo tunaendelea kuwaletea historia ya Mtaguso Mkuu wa Trento licha ya upinzani mkubwa kutoka kwa wafalme, Papa Pius IV, aliweza kukiitisha Kikao cha Tatu cha Mtaguso wa Trento. Sasa endelea…
Papa Pius IV (1559-1565):
Papa Paulo IV, alifuatwa na Papa Pius IV mtu wa wastani. Papa Pius alijaribu kuyapa mageuzi ya Papa Paulo IV sura ya utu bila kuyageuza.
Katika kazi hii alisaidiwa na mpwa wake Karoli Borromeo aliyempa ukardinali na uwaziri mkuu akiwa na umri wa miaka 21 tu.
Bahati nzuri Borromeo alikuwa mtu mtakatifu na mwenye busara.
Kikao cha Tatu 1562-63:
Licha ya upinzani kutoka kwa wafalme, Papa Pius IV, aliweza kukiitisha Kikao cha Tatu cha Mtaguso wa Trento. Hitimisho hili liliwezekana kwa msaada wa uelewa na diplomasia ya Kardinali Karoli Borromeo.
Baada ya kuweka vizuri matokeo ya mazungumzo yote ya vikao vya mtaguso yaliyoweka bayana mafundisho ya Kanisa Katoliki na kuweka sheria za kudhibiti utovu wa nidhamu, Mtaguso ulihitimishwa Desemba 3, 1563.
Maazimio yake yaliwekwa sahihi na wawakilishi wanne wa Papa, mapatriarka 3, maaskofu wakuu 25, maaskofu 169, maabate 7 wa monasteri kubwa, wakuu wa mashirika ya watawa 7 na wasimamizi wa majimbo 10.
Vilevile wawakilishi mabalozi wa wafalme Wakatoliki waliweka sahihi zao. Papa alithibitisha maamuzi ya mtaguso huo na kutoa hati ya kuyafanya mafundisho rasmi ya kanisa.
Ni vizuri kuona baadhi ya mafundisho ya Mtaguso wa Trento kwa kifupi na sheria zilizowekwa kudhibiti utovu wa nidhamu. Kwanza tuone baadhi ya mafundisho ya imani ya Trento.
1. Tofauti na Waprotestanti waliosema kwamba imani inatokana na Biblia tu, Mtaguso wa Trento ulisema ukweli wa imani ya dini unatokana na Biblia pamoja na mapokeo ya kanisa.
Mapokeo ni yale mafundisho na desturi zilizotoka katika kanisa la mitume na kuja kwetu bila kuwa katika Injili.
2. Vitabu vyote vya Biblia kama vinavyokutwa katika Biblia ya Septuaginta, vimeandikwa chini ya uvuvio wake Roho Mtakatifu na ni sehemu ya maandiko matakatifu.
Vitabu vya Agano la kale kwa Wakatoliki toka asili ni 46 wakati Waprotestanti wengi wana vitabu 39 tu.
3. Kanisa Katoliki pekee, lililoanzishwa na Kristo ndilo lenye mamlaka ya kufafanua neno la Mungu na si kila mmoja anavyoona kivyake.
4. Wakati Luteri alisema mtu anaokolewa na imani tu, Mtaguso Mkuu wa Trento, ulifundisha kwamba muumini anaokolewa kwa imani yenye matendo mema.
Imani bila matendo haiwezi kuleta wokovu. Walikosoa mafundisho kwamba baada ya dhambi ya asili binadamu hana utashi tena wa kusema hapana kwa dhambi.
Mtaguso unafundisha kwamba Mungu anampa binadamu uwezo wa kukubali au kukataa dhambi.
Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Sesilia-Kisarawe II, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Padri Rodger Kamuzinzi (mwenye kanzu nyeupe) akiwa katika picha ya pamoja na Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) wa parokia hiyo baada ya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa kanisa jipya parokiani hapo.
Kansela wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Padri Hamilton Kikoti (katikati), akiwasikiliza Paroko wa Parokia ya Bikira Maria Rozari Takatifu Makongo Juu, Padri Musa Kihoo na Mwenyekiti wa Kamati Tendaji ya Halmashauri ya Walei, Deogratius Mwarabu wakati wa kumwonesha maendeleo ya Parokia hiyo baada ya Kansela kufanya ziara ya kichungaji parokiani hapo.
Waamini wa Parokia ya Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu-Kilimahewa, Salasala Jimbo Kuu la Dar es Salaam, wakiwa katika adhimisho la Misa Takatifu ya Dominika iliyoadhimishwa parokiani hapo.
Dar es Salaam
Na Remigius Mmavele
Mzee anajiuliza, huku Pepe Kalle wala hamjali, akamfuata Djouna pale alipokua amesimama, akaanza kumkaripia, wewe inakuaje nilikuambia uwe unafika nyumbani sasa umetimiza mwezi mzima hujatokea tangu tumesafiri hadi tunarudi hujafika hata mara moja. Djouna akaomba samahani, basi Pepe Kalle akatoa begi la nguo nakumpa Djouna kama zawadi, ishara ya upendo na uaminifu.
Baada ya Pepe Kalle kuondoka, Baba yake Djouna alimwita mwanae kwa mazungumzo na kumuuliza swali moja tu: “Kati ya masomo na muziki, unachagua nini?” Djouna akajibu bila kusita: “muziki”.
Baba yake akambariki.
Siku iliyofuata baada ya mazungumzo yao ya kwanza ya kina, Pepe Kalle alifika nyumbani anakoishi Djouna Mumbafu akiendesha gari lake aina ya Mazda. Akamtazama na kumwambia maneno ambayo yamebaki moyoni mwa Djouna Mumbafu hadi leo: “Sikiliza kijana, wewe uko hapa si kwa kupendeza watu hapana. Wataendelea kukuwekea vikwazo na vijembe. Unachotakiwa ni wewe kufanya kazi vilivyo, uthibitishe uwezo wako. Najua kabisa kama unaweza”.
Bahati nzuri, safari mpya ilikuwa imepangwa ziara ambayo ingewafikisha hadi Mali, wakianzia na onesho kubwa nchini Burkina Faso. Huo ulikuwa mwanzo wa safari zake za kimataifa akiwa na Empire Bakuba. Walipowasili Burkina Faso, walitarajiwa kutumbuiza katika uwanja uliofurika watu. Ndani ya kundi lao, alikuwepo pia Zwazwe, dansa mwenye kipaji cha kipekee. Kati ya Djouna Mumbafu na Zwazwe kulizuka ushindani wa kisanii; nani angeutawala uwanja?
Siku ya onesho, Zwazwe alikuwa wa kwanza kupanda stejini na bila kuchelewa akaanza show. Alimiliki jukwaa kwa ustadi wa ajabu, akicheza kwa umahiri na fimbo yake. Uwanja mzima ukalipuka kwa makofi.
Ndipo Pepe Kalle akamgeukia Djouna Mumbafu na kumpa ishara ya kwamba akaingie yeye kazi kwake sasa. Djouna akiwa mwanamichezo na mchezaji wa judo aliyepata mafunzo, alipiga sarakasi kujirusha kuanguka kwa kishindo kikubwa, akawatolea rapa zake zilizowasha moto wa umati. Alivua shati lake, akapanda hadi kwenye majukwaa ya watazamaji na umati ukashangilia kwa nguvu.
Kwa kumaliza mchuano huo wa furaha, Pepe Kalle akapaza sauti yake maarufu: “Zabale! Zabale Chacha!” Akiashiria mwisho wa sehemu hiyo, kisha akamtania: “Wewe mwizi, rudi hapa!” (Kicheko.) Kwa Djouna Mumbafu kukubalika zaidi ndani ya kundi, alijiweka karibu kwa wazee ambao walikua tayari ni wakongwe ndani ya kundi ambao ni Vieux Elvis Nkunku, Mpiga Bass Layo Layo na Mpiga solo ya Doris.
Baada ya ziara yao Burkina Faso na Mali, walirejea jijini Kinshasa,
ndipo wakatangaziwa kuwa yupo mtayarishaji wa muziki (Producer) ambaye amejitokeza kuwapeleka ziara Ulaya. Kila mtu aliingia kwenye maombi ili jina lake liongezwe kwenye orodha.
Dar es Salaam
Na Arone Mpanduka
Asili ya jezi ya mpira ilianzia nchini England. Mwanzoni kabisa mpira wa miguu haukuwa na jezi. Miaka ya 1860 watu walikuwa wanacheza soka na nguo za kawaida walizonazo, wengine na shati nyeupe za kriketi, wengine na flana na kofia tu. Ndipo wakaona inaleta fujo kutofautisha timu.
RANGI ZA SHULE (1840 – 1857)
Ushahidi wa kwanza kabisa wa jezi za rangi ni kwenye shule ya Winchester College kabla ya 1840, walikuwa wameandika “Commoners have red and the college boys blue jerseys”. Baadaye Rugby School 1845 ikaweka sheria “hakuna mchezaji kuvaa kofia au jezi bila ruhusa ya nyumba yake”.
SHEFFIELD FC
Klabu ya kwanza ya mpira duniani iliyosajiliwa rasmi ni Sheffield FC (1857). Katika kanuni zao za 1857 waliamuru kila mwanachama anunue kofia moja nyekundu na moja bluu ya dark blue ili wagawane timu uwandani.
Baadaye ndio wakaanza kuvaa shati za rangi hizo hizo. Hii ndio inahesabiwa kama jezi ya kwanza ya klabu.
Wengine wanasema Nottingham Forest (1865) ndio wa kwanza kuvaa jezi kamili ya rangi moja. Walikutana kwenye Clinton Arms na wakaamua wanunue kofia 12 za “Garibaldi Red” - nyekundu iliyopewa jina la mpigania uhuru wa Italia na tangu hapo wamevaa nyekundu hadi leo.
Madrid, Hispania
Kylian Mbappe amezungumza moja kwa moja na mashabiki wa soka barani Afrika, huku kinyang’anyiro cha tuzo ya Ballon d’Or ya mwaka 2026 kikishika kasi.
Mshambuliaji huyo wa Real Madrid ametoa wito wa dhati unaozingatia asili ya familia yake pamoja na rekodi zake binafsi za kuvutia katika mwaka uliopita.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27, yuko kwenye orodha ya wachezaji 30 wanaowania tuzo hiyo ambayo itatolewa mjini London Oktoba 26.
Wapinzani wake ni pamoja na Lamine Yamal wa Barcelona, mshambuliaji wa Bayern Munich, Harry Kane na mshindi wa mwaka jana, Ousmane Dembele.
Villa Park, Uingereza
Kama ilivyokuwa msimu uliopita, maswali yanazuka kuhusu Alejandro Garnacho ambapo miezi miwili baada ya kujiunga na Aston Villa kwa mkopo wa awali, winga huyo bado hajathibitisha thamani yake kwa kocha Unai Emery.
Mshambuliaji huyo wa Argentina amecheza dakika 31 pekee akiwa na Villa, akitokea benchi katika mechi tatu tofauti na dakika 15 alizocheza dhidi ya Hull ndio muda mrefu zaidi alioutumia uwanjani katika mechi moja.
Garnacho amekuwa mchezaji wa akiba ambaye hakutumika katika mechi nne zilizopita za Villa, akishuhudia kutoka benchi timu hiyo ikishinda mabao 3-2 dhidi ya Tottenham siku ya Jumamosi.
Goli moja na pasi nne za mabao katika mechi 24 za Ligi Kuu ya England akiwa na Chelsea msimu uliopita, vilikuwa chini ya matarajio ya klabu hiyo kwa mchezaji huyo iliyemsajili kutoka Manchester United kwa pauni milioni 40, hivyo akaruhusiwa kuondoka.
Msimu huu ndio kwanza una mwezi mmoja, lakini Garnacho, mwenye umri wa miaka 22, huenda tayari anajikuta katika njia panda akiwa Villa Park.
Dar es Salaam
Na Arone Mpanduka
Wakati Ligi Kuu soka Tanzania Bara ikiwa imesimama kwa muda kupisha kalenda ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), jumla ya mabao 74 yamefungwa na timu zote zilizocheza viwanja vya nyumbani kwa nyakati tofauti.
Tumaini Letu limefuatilia mabao yaliyofungwa kwenye ligi hiyo tangu ilipoanza Agosti 14, mwaka huu hadi sasa na kubaini kuwa jumla ya mabao 121 yamefungwa katika mechi zote za raundi 6 zilizochezwa.
Mbali na mabao 74 yaliyofungwa nyumbani, mabao 47 pekee ndiyo yaliyofungwa na timu zilizocheza ugenini.