Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Henry Mchamungu (aliyeshika fimbo ya kichungaji) akiwa katika picha ya pamoja na Mapadri, Sista mlezi, Viongozi wa Parokia na watoto waliopokea Komunio ya Kwanza katika Parokia ya Mtakatifu Andrea Mtume, Bahari Beach jimboni humo. Kushoto kwa Askofu ni Paroko wa Parokia hiyo, Padri Marco Loth. (Picha zote na Yohana Kasosi)

KUSANYIKO LA  KILITURUJIA-I
1.    Maana ya Kusanyiko la Kiliturujia:
Kusanyiko la kiliturujia ni watu walioitwa na Mungu kwa njia ya Kristo kukusanyika kama jumuiya, ili kueleza imani yao na kuikuza zaidi kupitia ushiriki wao kamili na wa dhati katika sala ya jumuiya ya Kanisa. Kusanyiko la kiliturujia linaundwa na kila mtu anayekuja kuadhimisha Misa au Sakramenti nyingine. Kusanyiko la kiliturujia kwa hakika ni dhihirisho la Kanisa katika uhalisia wake kwa wakati wa kibinadamu na wa Kimungu: ni watu waaminifu waliokusanyika kumzunguka Bwana kuadhimisha fumbo la Pasaka.
Sala za kiliturujia daima hufanywa katika umoja kwa kuwa Mwadhimishaji hunena kwa jina la wote, au huendelea na mazungumzo na watu kwamba Neno la Mungu linasomwa.
2.    Kusanyiko la Liturujia katika Mapokeo ya Kanisa:
Umuhimu wa Kusanyiko la Kiliturujia:
Kukusanyika mara kwa mara kwa ajili ya sala  ni sifa ya maisha ya Kikristo 1 Kor, 11:14; Jam, 2.1-4.
Kuna faida za Kiroho zinazopatikana katika kukukutanika, “wakutanapo wawili au watatu kwa jina langu, nipo kati yao”
Kusanyiko la kiliturujia hudhihirisha mkusanyo wa wanadamu ambao Kristo ametimiza.
Neema ipatikanayo kwenye mkusanyiko ni ya kifumbo katika kila adhimisho la Liturujia.
3.    Sifa za Kusanyiko la Kiliturujia:
i. Asili Takatifu ya Kusanyiko la Liturujia:
Kusanyiko la kiliturujia ni takatifu kwa kuwa mwanzilishi wake ni Mtakatifu, na Roho Mtakatifu analiongoza.
ii. Asili ya Agano la Kale:
Kusanyiko lilianza kwa mwito wa Abrahimu, lakini Kusanyiko rasmi linaanzia chini ya Mlima Sinai. Sheria ilitolewa, na Agano lilifanywa (Kut, 19-24, Kumb, 4.10, 9.10, 8.16, 23.1-8). Kwa Kiyunani, Kusanyiko huitwa  “Ekklesia” na kwa Kiebrania “Qahal Yahweh”. Ni Kusanyiko la Yahweh lililoitishwa na Mungu Mwenyewe (Kut, 19:17-18, Kum, 4:12-13). Yaani Mungu alikuwepo na akasema na watu wake.
iii. Kanisa la Kristo, Asli ya  Watu Wapya wa Mungu:
Kusanyiko ni Kanisa, Mt 16.18. Warithi ambao Kristo anawatuma wanaliitisha Mt, 38.18-20. Agano Jipya limetiwa muhuri kwa damu ya Kristo, Agano ambalo ni moja na la milele, na lisiloweza kubatilishwa, damu ambayo inamwagika kwa ajili ya ondoleo la dhambi. Kusanyiko hili jipya, zaidi ya lile la Agano la Kale, ni la watu wa Kifalme na Kikuhani (Kut 19.6, 1 Pet, 2.4-10, Ufu, 1.6, 5.9-10, Ufu, 20.6). Watu hao wanapaswa kutoa dhabihu ya Kiroho kwa vile wanaunda Ukuhani Mtakatifu.
iv. Kusanyiko la Kiliturujia hudhihirisha Kanisa:
Kusanyiko linadhihirisha ishara ya Kanisa, ni Kusanyiko la Kristo, yaani, Mwili mmoja wenye viungo mbalimbali. Misa katika Kusanyiko ni kumbukumbu ya dhabihu ya Kristo.
v. Mungu ndiye anayewaita watu:
Mungu ndiye mwanzilishi; wengine ni vyombo vyake tu vya utumishi. “Sio ninyi mlionichagua mimi, bali mimi niliyewachagua mimi”.  Hii inaonyesha kwamba, Mungu ndiye mwanzilishi wa kila kitu. Katika uumbaji, Mungu alianzisha kila kitu. Wanadamu walipewa mamlaka ya kutunza na kuendeleza kile ambacho Mungu tayari ameanzisha.
vi. Uwepo wa Mungu katika Kusanyiko:
“Wawili au watatu wakusanyikapo kwa jina langu, mimi nipo katikati yao, Mt, 18.20. Hii inaonyesha kwamba, Mungu anapendelea Liturujia ya kijumuiya badala ya Liturujia ya kibinafsi. Katika muktadha huu, Liturujia siyo jambo la kibinafsi.
vii.    Kusanyiko ni tarajio la Mbingu:
Kusanyiko ni taswira inayotarajia Kanisa la Mbinguni kama mtazamo katika giza la imani. Tarajio hili linaonyeshwa vyema katika kitabu cha Ufunuo. Yaani mbinguni kama Kusanyiko la Liturujia; watu ambao wamefua nguo zao katika damu ya mwana-kondoo (Ufu, 7:14)
4. Watu wa Mungu katika Kusanyiko:  
i. Kusanyiko la Watu Wote:
Kusanyiko la kiliturujia ni kwa ajili ya watu wote wanaotimiza masharti mawili. Wale ambao wameikubali imani ya Kanisa, na hawajaikana hadharani, na wale ambao wamepokea Ubatizo au angalau wanajiandaa kwa Ukatekumeni.
Wajumbe wa Kusanyiko hilo ni wakosefu wanaotafuta huruma ya Mungu. Hii ndiyo sababu sala za kawaida zinajumuisha kukiri hadharani dhambi na kuomba rehema ya Mungu. Kanisa linaanzia ngazi ya chini (familia, jumuia, Kigango, Parokia, Jimbo, Taifa, n.k.), hadi ngazi ya ulimwengu. Huo ni umoja katika utofauti.
ii. Mkusanyiko  Katikati ya Utofauti:
Moja ya sheria muhimu katika Historia ya Wokovu ni kwamba watu wapya wa Mungu lazima wawalete wanadamu pamoja, licha ya yote ambayo yanasababisha mgawanyiko (Efe 2:14, Mdo, 2:6-11). Hakuna tena aliyetahiriwa wala asiyetahiriwa, Myahudi wala mtu wa Mataifa, Myunani na Mrumi, Mtumwa na Mtu Huru. Wabatizwa wote ni wamoja katika Kristo ambaye ni Bwana wa wote. Kuna Imani moja tu, Ubatizo mmoja, Mkate mmoja tunaomega, kikombe kimoja cha damu ya Kristo na Mwili mmoja (Rum, 10:12, 1 Kor, 12:13, Gal, 3:28, Efe, 2:19, Ufu, 5:11).
Kwa hiyo, Kusanyiko ni kuleta muungano, sio mgawanyiko. Kusanyiko linaleta neema ya upendo wa kindugu na umoja.
iv. Ushiriki hai na wa Kiakili:
Waamini sio watazamaji tu, pia wanalo jukumu la kushiriki. Kushiriki Kikamilifu katika mafumbo Matakatifu na katika sala ya hadhara na kuu ya Kanisa ni chanzo cha kwanza na cha lazima cha Roho wa kweli wa Kikristo. Haki na wajibu wa Waamini kushiriki kikamilifu katika Liturujia, inatokana na asili ya Kanisa kuwa ni watu wa Kifalme na Kikuhani wanaoshiriki kadri ya hali zao, katika Ukuhani wa Kristo na kuunda mwili ambao una kazi mbalimbali, lakini hufanywa mmoja na Roho Mtakatifu.
Wanashiriki na kudhihirisha umoja huu kwa kusikiliza pamoja Neno la Mungu, wakijishikamanisha na Sala ya Mwadhimisho, kushiriki kwa njia ya mazungumzo, kuimba, matendo ya kimwili, ishara, na Misa kwa kushiriki katika Sadaka na Ushirika wa Ekaristi.
Ushiriki wa kiakili na uchaji pia unahitajika. Matendo ya kiliturujia ni ishara ambayo kwayo imani inatakiwa kugusana na Fumbo la Kimungu linalotimizwa humo; hatua hiyo inahitaji umakini wa kidini. Akili na mioyo ya Waamini lazima iendane na sauti zao wanapoimba, au kufanya mazungumzo.
Waamini lazima waifanye sala ya Mwadhimishaji kuwa yao wenyewe wanapoisikiliza. Ni lazima wasikilize Neno la Mungu kwa Uaminifu. Wakati fulani, adhimisho litawahitaji kujiweka wenyewe katika ukimya mtakatifu. Kwa hiyo, waamini lazima wapewe ufahamu wa taratibu na Maandiko hivi kwamba, ndani ya Kusanyiko hakuna mtazamaji, ila wote ni washiriki na watendaji.
v. Watu wanaoadhimisha:  
Kusanyiko linaunda adhimisho. Waamini wanakusanyika kimsingi kuadhimisha kwa shukrani tukio la Fumbo la Wokovu. Kusanyiko linaweza kufanyika kwa ajili ya uchaji binafsi kama vile litania, mikesha n.k, lakini ibada hizi za uchaji, karibu kila mara ni maandalizi ya maadhimisho ya kiliturujia.
5.    Majukumu  katika Kusanyiko:
5.1 Utangulizi:
Katika Kusanyiko, kila mshiriki huchukua sehemu hai yenye majukumu tofauti. Ni hivyo ili kudhihirisha asili ya Kanisa. Adhimisho lina Mkuu, ambaye ni Mwadhimishaji Mkuu, na kati ya Mwadhimishaji Mkuu na Waamini, kuna wasaidizi wanaofanya huduma za utumishi.
Katika adhimisho la Liturujia, kila mmoja, Mhudumu Mlei, ambaye ana ofisi ya kuhudumu, anapaswa kufanya yale tu yanayohusika na ofisi hiyo kwa asili ya ibada na kanuni ya Liturujia (VSC 28). Utofauti huu wa majukumu, hufanya Kusanyiko kuwa mwili hai ambao ni udhihirisho wa Mwili wa Fumbo wa Kristo (1 Kor, 12:12-30). Utekelezaji wa majukumu hayo tofauti unaifanya Liturujia iwe katika utaratibu madhubuti ambapo kila mshiriki anatekeleza wajibu wake ipasavyo.
5.2 Mwadhimishaji
Mwadhimishaji, ambaye ni Askofu au Padri, anaongoza Kusanyiko katika nafsi ya Kristo. Yeye ndiye anayesimamia vyema Kusanyiko, na anaongoza sala. Anafanya matendo matakatifu, anamega mkate wa Neno la Mungu na mkate wa Ekaristi kwa ajili ya watu. Nafasi yake si kwa kuteuliwa na Kusanyiko au kwa sababu ya sifa za kibinadamu, bali kwa sababu kwa kuwekwa wakfu ana sifa ya Kikuhani. Kwa nguvu ya sifa hii, anachukua nafasi ya Kristo. ‘Anatenda katika nafsi ya Kristo’. Anapoadhimisha mafumbo matakatifu, Kristo anakuwa ndani yake.
Askofu wa Mahalia ni Mwadhimishaji Mkuu kwa kuwa Utume wake ameurithi kutoka kwa Mitume. Hakuna awezaye kuongoza shughuli ya Liturujia jimboni, isipokuwa kwa amri yake na idhini yake. Kiti chake katika Kusanyiko kimewekwa hivi kwamba yeye aonekane kwamba ndiye kitovu na kiini cha Kusanyiko zima.
Mapadri , ambao ni watenda kazi pamoja na Askofu Mahalia na wanaopokea Utume wao kutoka kwake, wanaliongoza Kusanyiko mahali pake na kwa muungano naye. Hata hivyo, hawawezi kufanya maadhimisho fulani ambayo yametengwa kwa ajili ya Askofu  kwa mujibu wa taratibu za kiliturujia na sheria za Kanisa.
Shemasi, kama Padri hayupo, anaweza kuongoza na kuadhimisha ibada fulani kama vile Ubatizo, Liturujia ya Masaa, mazishi, na mengine, kulingana na Kanuni za Kiliturujia na sheria za Kanisa. Katika Kusanyiko la Dominika, ibada maalum bila Padri inaweza kutambuliwa kwa kuzingatia miongozo iliyotolewa.
Itaendelea makala ijayo.

BOURNEMOUTH, Uingereza
Bournemouth wamekubali mkataba wa mkopo wa msimu mzima kwa mlinda mlango wa Chelsea, Kepa Arrizabalaga.
Uhamisho huo unatarajiwa kumaliza nia ya Bournemouth kwa mlinda mlango wa Arsenal Aaron Ramsdale, lakini pia Kepa, 29, pia ameongeza mkataba wake Stamford Bridge hadi mwisho wa msimu wa 2026.
Mkataba wake ulitarajiwa kukamilika Juni 2025, ambao ungemruhusu kuondoka Chelsea kwa uhamisho wa bure mwishoni mwa muda wake wa mkopo na Chelsea.
Kepa anasalia kuwa kipa ghali zaidi duniani kuwahi kuhamia The Blues mwaka 2018 kutoka klabu yake ya utotoni, Athletic Bilbao, kwa £71m.
Amekuwa akifanya mazoezi, pamoja na wachezaji wengine 14, mbali na kikosi cha kwanza cha meneja Enzo Maresca, na inaaminika kuwa hana mustakabali Stamford Bridge.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Uhispania alitumia msimu uliopita kwa mkopo Real Madrid, ambapo alicheza mechi 20 kama mbadala wa Thibaut Courtois aliyejeruhiwa, akishinda La Liga na Ligi ya Mabingwa.

LONDON, Uingereza
Mipango ya Kituo cha Tenisi karibu na mji wa Sir Andy Murray wa Dunblane, imefutwa kutokana na masuala ya kupanga na kupanda kwa gharama.
Mradi wa (£20m), ulioongozwa na mama yake Judy Murray, ulilenga kujenga jumba la jamii la michezo mingi katika Park of Keir, kuashiria urithi wa tenisi wa familia ya Murray.
Chama cha Tenisi cha Lawn (LTA) kiliahidi pauni milioni 5 kwa mradi huo lakini kilikutana na upinzani kutoka kwa wanakampeni ambao walisema haupaswi kujengwa kwenye ardhi ya ukanda wa kijani.
Shirika la hisani la Judy Murray, Murray Play Foundation, lilisema, “Kwa masikitiko makubwa na huzuni,” sasa halitaendelea.
Ongezeko kubwa la gharama za ujenzi na nishati, mchakato wa upangaji wa muda mrefu na mijadala inayoendelea na bodi zinazosimamia, zilitajwa kuwa sababu za kuuacha mradi huo.

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Mwaka 2024 unaendelea kushuhudia tasnia ya muziki nchini Tanzania ikiendelea kushamiri, huku wasanii wakizidi kujipatia umaarufu na utajiri mkubwa.
Muziki wa Bongo Flava umevuka mipaka ya Afrika Mashariki, ukiwavutia mashabiki lukuki duniani kote.
Kupitia vipaji vyao vya kipekee na bidii katika kazi zao, baadhi ya wanamuziki wamefanikiwa kujikusanyia utajiri mkubwa wa kutikisa.
Taarifa zinadai kuwa orodha hii ya wasanii matajiri zaidi Tanzania mwaka 2024, na kuufanya muziki wa Tanzania kupata thamani sokoni, na hivyo kuzibwaga nchi nyingi za jirani kutopata mpenyo.
Diamond Platinumz,
Nasibu Abdul Juma almaharufu kama Diamond Platnumz au Simba wa WCB anaendelea kutamba kileleni mwa orodha ya wasanii matajiri zaidi Tanzania.
Utajiri wake unatokana na muziki wake unaoendelea kutikisa pande mbalimbali za Afrika na Dunia kiujumla mathalan katika biashara mbalimbali, ikiwemo lebo yake ya WCB, uwekezaji katika mali isiyohamishika, na mikataba kibao ya matangazo.
Maisha yake ya kifahari yamekuwa yakionekana kupitia magari yake ya kifahari, nyumba za kifalme, na safari kwenda nchi za kigeni.
Juma Jux
Juma Mussa Mkambala almaharufu kwa jina la kisanii kama Juma Jux amejizolea utajiri mkubwa kupitia muziki wake unaovuma, hasa nyimbo zake za mapenzi zinazogusa hisia za wengi.
Uwezo wake wa kuandika nyimbo zenye mashairi ya kuvutia na sauti yake tamu vimemfanya kuwa mmoja wa wasanii wanaotafutwa sana Tanzania.
Jux amekuwa miongoni mwa wasanii wanaoishi maisha ya kifahari nchini Tanzania, uku akishuhudiwa kumiliki imagari ya kifahari mbalimbali, ikiwemo Mercedes Benz E-Class ya mwaka 2021, ambayo gharama yake ni zaidi ya dola elfu 53 bila ya kodi ambazo ni karibia shilingi milioni 160 za Kitanzania.
Harmonize
Konde Boy, Harmonize, amejipatia nafasi ya tatu katika orodha hii kutokana na muziki wake unaopendwa na mamilioni, lebo yake ya Konde Music Worldwide, na biashara zake nyingine, ikiwemo ya Redio.
Ubunifu wake katika muziki na mtindo wake wa kipekee, umemfanya kuwa miongoni mwa wasanii wanaolipwa pesa nyingi zaidi kwa show nchini.
Nafasi ya tatu ikifuatiwa na msanii Zuchu, Marioo, Nandi, Ommy Dimpoz, Rayvanny, Ali Kiba na Niki wa pili akimalizia nafasi ya kumi.
Muziki unalipa ukiiufanya kwa bidii na kwa ubunifu zaidi, kwani ni sehemu ya ajira ya vijana wengi kwa sasa nchini.

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Uongozi wa klabu ya soka ya KMC umejitoa katika mbio za ubingwa msimu huu kutokana na kutokuwa na misuli ya kutosha katika kushindana na vilabu vingine.
Mtendaji wa klabu hiyo Daniel Mwakasungura alisema kuwa bado wanaendelea kujitafuta, huku akiweka wazi kuwa bado hawapo katika ramani za waokupambana na wenye uwezo wa kifedha .
Mwakasungura alifunguka kuwa wameliona hilo kwa mwaka huu, na kuamua kuijenga timu yao ili ikishakuwa sawa, waanze kupambana kwa misimu mingine ya ligi huko baadaye lakini kwa sasa bado hawana wachezaji wenye uwezo wa kiushindani.
Alisema kuwa kwenye upande wa soko la usajili, wenzao wamewaacha mbali sana kuliko wao, kwani gharama ambazo wanatumia vilabu vingine katika kusajili wachezaji, ni kubwa kuliko za wao, na hivyo kusababisha hata kupokonywa wachezaji wengi wzuri.
“Unajua kwenye soko la ushindani unatakiwa ujitutumue kweli sasa sisi tunamuona mchezaji, na tunatamani kumsajili lakini unakuta fedha tunayotoa ni ndogo kuliko ambayo wenzetu wakiamua kuitoa kwa mchezaji huyo huyo”, alisema Mwakasungura.
Alisema pia kuwa kwa sasa wao wanajenga timu ili iwe tishio kwa miaka inayokuja, kwani tayari wameshaanza kujipata katika namna ya uchezaji, hivyo vimebaki vitu vichache ambavyo wao kwa kusaidiana na bechi la ufundi, wanavitengeneza.
KMC msimu uliopita ilibaki kidogo kushuka kwenda kucheza Ligi ya Championship, lakini walijipapatua na kuendelea kubaki katika Ligi Kuu. Kwa msimu, na sasa wanachokifanya ni kujihakikishia nafasi ya kutoshuka Daraja ili malengo yao ambayo waliyaweka, yaweze kutimia.

DAR ES SALAAM

Na Deus Helandogo

Uongozi wa klabu ya soka ya Simba kupitia kwa Meneja wake Ahmed Ally, umefunguka sakata la kuachana ghafla na mshambuliaji wao Fredy Michael, ambaye amedumu ndani ya klabu hiyo kwa miezi michache tu.
Ahmed Ally aliweka wazi kwamba sababu za kuachana na nyota huyo ni kutokana na kuwa alishindwa kufundishika, mara baada ya kocha wao Fadlu Davis kumfanyia mazoezi mengi na kuzungumza naye, lakini bado kiwango chake kilikuwa hakiridhishi.
Ahmed alisema kuwa moja kati ya wachezaji ambao wao kama uongozi walikuwa wanafikiri a kuwa atakuwa kiongozi kwa wachezaji wengine, ni yeye, lakini kutokuwa timamu kimwili kumesababisha kocha kuomba kutafutiwa mchezaji mwingine.
Alisema pia kuwa wakati wa maandalzi ya msimu mpya wa ligi walipoweka kambi kule Misri, kocha Fadlu alikuwa akimfuatilia na kuzungumza naye mara kwa mara, lakini bado hakuwa katika utimamu wa mwili.
“Kocha alizungumza naye mara kwa mara tangu alipowasili kambini lakini hakuweza kufanya zaidi atu alikuwa akishuka kila siku na ndiyo maana kocha alitaka kutafutiwa mchezaji mwingine haraka zaidi, ndipo tukamtafuta mwamba Christian Lionel Ateba”, alisema Ahmed.
Alisema pia kwamba suala la kuachana na Fredy, ni kutokana na matakwa ya kocha na ni kutokana na kutopedezwa na kiwango chake alichoonyesha kwenye mazoezi laini. Kwa sasa wamemalizana naye na hivyo wanaanza upya.
Aidha, alizungumzia juu ya kulidhishwa na kikosi chao, huku akiweka wazi kuwa msimu huu, pamoja na kuwa wanajenga timu, lakini wana mipango ya kuchua ubingwa msimu huu na kurudisha ufalme wao ambao waliupoteza kwa watani zao Yanga, lakini watahakikisha wanafanya vyema.
Mpaka sasa, klabu ya Simba imefanikiwa kucheza michezo miwili ya ligi dhidi ya Tabora United na Fountaine Gate na kufanikiwa kubeba alama zote 6 na kujikusanyia mabao 7 wakiwa juu katika msimmo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Papa  Fransisko katika  tafakari  yake, Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni mwili na roho, tarehe 15 Agosti 2024 anasema, Mama Kanisa anawaalika watoto wake kumtafakari Bikira Maria baada ya  kupashwa  habari kuwa atakuwa ni Mama wa Mungu aliondoka, akaenda hata nchi ya mlimani kwa haraka mpaka mji mmoja wa Yuda, akaingia nyumbani kwa Zakaria akamwamkia Elizabeti, binamu yake! Rej Lk, 1: 39-56. Shuhuda wa furaha, matumaini na uzima wa milele.
Ilikuwa ni tarehe Mosi, Novemba 1950, katika Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu, Papa Pio wa kumi na mbili (1939-1958: wa 260) katika Waraka wake wa kitume.
 “Munificentimus Deus” yaani “Mungu Mkarimu” alipotangaza kwamba, “Bikira Maria, Mama wa Mungu ambaye daima ni Bikira, amepalizwa mbinguni mwili na roho baada ya kuhitimisha safari yake ya hapa duniani,” kuwa ni fundisho tanzu la imani ya Kanisa Katoliki.
Hii ilitokana na sababu kwamba tangu mwanzo kabisa, Kanisa limekuwa linamwadhimisha Mama Bikira Maria kama Eva mpya, huku akihusishwa na Adam mpya, Mwanaye Bwana wetu Yesu Kristo.
Kumbe, kwa maneno mengine, Sherehe hii inapata chimbuko lake katika Mapokeo ya Kanisa, na hasa zaidi wakati wa Maadhimisho ya Mtaguso wa Efeso uliofanyika  mwaka 431, ulipotamka kuwa Bikira Maria ni Mama wa Mungu, “Theotokos.”
Waamini wa Kanisa la Mashariki kwa miaka mingi walikuwa wanaiadhimisha Sherehe hii ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni mwili na roho, kama kielelezo cha kulala usingizi wa amani “Dormitio,” na wataalam wengine wakaongeza kusema, “Somnum Mariae.”
Hii ni Sherehe inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila Mwaka ifikapo tarehe 15 Agosti.
Mwili wa Bikira Maria uliokuwa umekingwa na dhambi ya asili, ukapalizwa mbinguni, hiki ni kielelezo makini cha imani ya watu wa Mungu kama alivyokiri Mtakatifu Yohane Paulo II (1978-2005 wa 264) mnamo mwaka 1997.
Baba Mtakatifu Francisko katika tafakari yake, Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni mwili na roho, tarehe 15 Agosti 2024 anasema, Mama Kanisa anawaalika watoto wake kumtafakari Bikira Maria baada ya kupashwa habari kuwa atakuwa ni Mama wa Mungu, aliondoka, akaenda hata nchi ya mlimani kwa haraka mpaka mji mmoja wa Yuda, akaingia nyumbani kwa Zakaria akamwamkia Elizabeti, binamu yake! Rej Lk, 1: 39-56.
Taarifa kwamba, atakuwa ni Mama wa Mungu, ili kumsukuma kuondoka kwa haraka, kwenda kutangaza na kushuhudia ile furaha iliyomwilishwa katika huduma.
Tangu wakati huo, Bikira Maria alianzisha mchakato wa kumfuasa Mwanaye Mpendwa Kristo Yesu, kama mfuasi halisi wa Ufalme wa Mungu, akadiriki hata kusimama chini ya Msalaba, na hatima ya hija hii ya maisha ya kiroho ni Kupalizwa kwake mbinguni, ambako huko juu mbinguni wanaendelea kufurahia pamoja na Kristo Yesu, maisha ya uzima wa milele.
Bikira Maria ni mfano wa mwamini anayesoma alama za nyakati, akawa tayari kufuata nyayo za Mwanaye mpendwa, akakutana na wafuasi wa Kristo Yesu, na baadaye safari yake ya kutangulia kwenda mbinguni, kwenye utukufu wa Baba wa milele.
Huu ni mwaliko kwa waamini kutambua kwamba maisha yao huku bondeni kwenye machozi, ni safari endelevu itakayofikia hatima yake kwa kukutana na Kristo Yesu, huko mbinguni.
Waamini wanahamasishwa kuhakikisha kwamba wanatunza moyoni mwao, kwamba Mwenyezi Mungu amewaumba, ili hatimaye, waweze kuwa na furaha ya uzima wa milele na kwamba, ndoto yake ni kuwachukua waja wake wote, ili wakaishi naye katika maisha ya uzima wa milele.
Safari ya maisha ya binadamu ni sehemu ya mpango wa upendo wa Mungu kwa binadamu. Hii ni hija inayowaongoza siku hadi siku, ili kukutana na Mwenyezi Mungu, chemchemi ya furaha isiyokuwa na mwisho; furaha ambayo amewaandalia waja wake.
Baba Mtakatifu Fransisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanarutubisha safari hii kwa matumaini na hasa pale, wanapokumbana na magumu pamoja na changamoto za maisha.
Maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni Mwili na Roho, iwe ni fursa makini kwa Waamini kujiuliza swali la msingi, ikiwa kama katika safari ya maisha yao hapa duniani, wanaendelea kuirutubisha kwa matumaini, kwa kutambua kwamba, mwisho wa safari yao, yuko Kristo Yesu anayewangoja.
Au katika safari hii ya maisha, tayari wamekwisha “kubweteka?” Je, Waamini wanakumbuka kwamba wameumbwa kwa ajili ya kufurahia maisha ya uzima wa milele; kwa kuwapenda na kuwathamini ndugu na jirani au Mwamini amejikuta akiwa amezama zaidi katika uchoyo na ubinafsi, na hatimaye kuzama katika malimwengu?
 Mwishoni mwa tafakari yake, Baba Mtakatifu Fransisko amewaalika Waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kumwangalia, na hatimaye, kumwomba Bikira Maria ili aweze kuwaombea, ili kamwe wasisahau kwamba hatima ya maisha yao ni furaha na matumaini ya uzima wa milele. “Macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo; na utajiri wa utukufu wa urithi wake katika Watakatifu jinsi ulivyo.” Efe 1:18.
Katika hatua nyingine, Kardinali Pierbattista Pizzaballa, O.F.M. Patriaki wa Yerusalemu na Mlinzi Mkuu wa Nchi Takatifu na Mlima wa Sion, katika Maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa mbinguni Mwili na Roho, yaliyofanyika kwenye Kanisa Kuu la Mateso lililoko kwenye Mlima wa Mizeituni ulioko Mashariki mwa mji wa Yerusalemu.
Papa Fransis alitumia fursa hii kwa ajili ya kuombea amani duniani, lakini zaidi huko Mashariki ya Kati.
Katika mahubiri yake amewaalika Waamini kumtafakari Bikira Maria aliyepalizwa mbinguni mwili na roho kama zawadi kubwa kutoka kwa Mungu, changamoto kwa Walimwengu ni kuondokana na : vita, ghasia, machafuko; Utumwa mamboleo na biashara ya ubidhaishaji wa maumbile ya binadamu unaoendelea kudhalilisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu, aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, pamoja na ukoloni mamboleo.
Bikira Maria, Mama wa Yesu akiwa amekwisha kutukuzwa mbinguni mwili na roho, ni sura na mwanzo wa Kanisa ambalo litapata utimilifu wake katika ulimwengu ujao. Kadhalika anang’aa duniani kama alama ya hakika ya matumaini na ya faraja kwa taifa la Mungu lililo safarini, mpaka siku ya Bwana itakapokuja. LG 68.
Amezungumzia kuhusu madhara ya vita yanayowatumbukiza watu katika umaskini wa kisiasa, kiuchumi na kijamii, kwa kusigina, uhuru, utu, heshima na haki zao msingi. Bikira Maria aliyepalizwa mbinguni, awaombee Walimwengu haki, amani na upatanisho.

MWANZA

Na Paul Mabuga

Maureen Mwanawasa, Mke wa Rais wa zamani wa Zambia, Levy Mwanawasa [2002 – 2008], amefariki  Agost 13, 2024, jijini Lusaka nchini humo baada ya kuugua kwa muda mfupi. Kama ulipata nafasi ya kumfahamu, bila shaka utajiuliza kwa nini akina mama huku kwetu wanashindwa kuwashawishi wanaume wanne wao kwenda kanisani hasa baada ya kuonekana mahudhurio yao ni hafifu na yenye kulalamikiwa.
Fikiria mama wa ‘kibongo’ anaweza kumshawishi mume wake, kulipia hadi shilingi elfu 30 ama hata hamsini, kwa ajili ya kusuka nywele ili apendeze, ama anunulie gauni la mtoko la hadi shilingi 60,000/- na kumsaidia marejesho ya mikopo ya kausha damu, lakini anashindwa kumbembeleza mwanaume ahudhurie kanisani, jambo ambalo hata hivyo haligharimu fedha yoyote.
Safari yangu ya kukutana na Maureen Mwanawasa ilianzia uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Keneth Kaunda jijini Lusaka, ambapo wakati natoka nje  nikiwa miongoni mwa wageni waliowasili, nilipokelewa na mzee mmoja raia wa Tanzania. Nilishangaa baada ya kuwa licha ya mzee huyo kunizidi umri, lakini alipokea begi langu   ambalo lilikuwa mzigo wangu pekee, na kunielekeza kwenye gari ndogo tukielekea katikati ya jiji la Lusaka. Juhudi zangu za kukataa mzee huyu kunibebea mzigo ili kulinda mila za Kiafrika, zilizogonga mwamba.
Hapo safari ikawa moja kwa moja hadi katika hoteli ya Pamodzi [yaani pamoja] ambayo baadaye niliambiwa kuna Marais na Wakuu wa Nchi 14 wanalala hapo, na ndiyo maana ulinzi ulikuwa mkali. Nikajisemea kimya kimya, itakuwaje siye kwa mazoea ya kabila letu kwamba ukinywa hata kabia kamoja, unaanza kuimba. Lakini kwa bahati, mratibu wa mambo akaniambia, “Bwana mdogo twende huku.’’ Nikapelekwa hoteli nyungine jirani ambayo nayo ilikuwa kubwa. Hii ilikuwa ni Agosti 15, 2007.
Jioni hiyo kukawa na zoezi ambapo watu wote waliokuwa wanatarajia kuingia katika vikao vya Marais na wakuu wa Nchi katika Jumuiya ya Nchi zilizo Kusini mwa Afrika [SADC], walitakiwa kufika katika kituo maalum, ambapo baada ya kuhakikiwa, walipigwa picha na kupewa Kitambulisho maalum. Hakuna aliyekuwa akiachwa kwenye hatua hii, isipokuwa mabwana wakubwa.
Wakati nimefikia hatua ya kupigwa picha, akaingia mama mmoja aliyevaa kitamaduni, na baadaye nikabaini kuwa ni mmoja wa wafanyakazi katika Ikulu wa King Mswati lll wa Eswatini. Kwa heshima yake na kwamba anatoka katika familia ya kifalme, jambo ambalo inaelekea Wazambia wanalijali, nikaambiwa nimpishe ahudumiwe kwanza yeye. Nikafanya hivyo, na mimi baadaye nikapata kitambulisho changu.
Asubuhi wakati nakwenda kwenye mkutano, ile naingia geti la kwanza, nikakutana na askari ambaye baada ya kutambua kuwa ninatoka Tanzania, akanionesha kitambulisho cha mmoja wa Mawaziri wa  huku kwetu ambacho kumeokotwa. Akaniuliza, unamjua huyu na mimi nikamwambia, naam namjua ni mmoja wa mawaziri wetu, na akanionya, mtafute umpe hiki kitambulisho, vinginevyo hataingia humo ndani. Niliifanya kazi hiyo na baadaye kumkabidhi kitambulisho chake.
Wakati wa mapumziko, nilifanikuwa kuwa karibu na aliyekuwa Rais wa Namibia, Hifikipunye Pohamba, jamaa mrefu hivi, baada ya kumsalimia kwa Kiingereza na kuonesha nia ya kufanya naye mahojiano, aliinama na kusoma kutambulisho changu ambacho kilikuwa kikionesha pia ninatoka nchi gani. Baada ya kugundua ninakotoka akabadili lugha na kuniambia kwa Kiswahili, “habari za Dar es salaam, vipi Buguruni, mambo poa” Wakati naendelea kutafakari hatua ya kufuata, akaanza kuondoka na kuniaga. “Haya bwana, kazi njema!”
Jioni wakati wa mpango wa kazi, nikaitwa na mkuu wangu, nakwambiwa kuwa siku inayofuata, nitaambatana na wake wa Marais na Wakuu wa Nchi ambao watakuwa katika ziara wakiongozwa na mwenyeji wao, Mke wa Rais wa Zambia Maureen Mwanawasa. Siku hiyo ilipofika, tulianza ziara tukiwa katika mabasi mawili, moja likiwa la hao akina Mama Waheshimiwa na jingine la watu waliokuwa  kwenye kazi mbali mbali, tukiwemo wanahabari wachache.
Tulipomaliza ziara iliyochukua hadi muda wa mchana, tulirudi katika hoteli ya Pamodzi, ambapo kulikuwa na maonesho ya bidhaa mbali mbali  zinazozalishwa na wanawake nchini humo, ikiwa ni pamoija na vito. Mama Maureen hakusita kuwaambia kwa lugha yao akina mama wale, wafanye biashara, kwani hao waliowatembelea ni wake wa Marais. Nilitafsisriwa hicho alichokisema na mwandishi wa gazeti moja la nchini humo.
Baada ya ziara hiyo, akina mama hao wakawa na kikao chao, Mama Maureen Mwanawasa ambaye alikuwa Mwenyekiti wao, alisimama na kuwaambia juu ya ajenda muhimu, iliyohusu azimio lao la kutaka  wanawake kupewa nafasi ya madaraka katika kile kinachojulikana kama hamsini kwa hamsini, yaani kama mkakati wa kijinsia wanawake wapewe nafasi katika ngazi mbali mbali katika kiwango cha uwiano sawa na wanaume.
Cha kufurahisha ni kwamba aliwaambia kesho yake watawasilisha hoja, na kwamba kila mmoja aitangulize hoja hiyo kwa mwenzi wake. Na inawezekana kila mmoja aliwasilisha hoja hiyo, maana ilipowasilishwa  na Mama Maureen Mwanawasa siku iliyofuata mbele ya  Wakuu wa Nchi, hakukuwa na mjadala bali Viongozi hao  walipiga makofi kama ishara ya kuiunga mkono, na ikapita, na kuanzia hapo imekuwa ajenda ya kudumu katika Nchi hizo.
Ukiacha hilo, lakini Maureen Mwanawasa amekuwa na ushawishi mkubwa katika mambo mbali mbali enzi ya uhai wake, ikiwa ni pamoja na harakati ya kupambana na umaskini, na pia akiongoza Wake wa Marais na Wakuu wa Nchi katika Jumuiya ya SADC katika kupambana na madhira ya UKIMWI na Virus vya UKIMWI.
Ni Mwanamke ambaye alitumia nguvu ya ushawishi wake katika kupeleka ajenda. Anasifika pia katika kuendesha kampeni za kisiasa kupigania ushindi wa mume wake katika chaguzi.
Maureen alizaliwa April 28. Mwaka 1963 katika eneo la Kabwe nchini Zambia. Aliolewa na Mwanasheria Levy Mwanawasa Mei 07, 1987. Mumewe alifariki mwaka 2008 akiwa madarakani, na Mwenyezi Mungu aliwajalia  watoto wanne, ambapo watatu ni wa kike na mmoja ni wa kiume.
Kwa njia ya ushawishi wa akina mama kwenye hamsini kwa hamsini, dada zetu, shemeji zetu, shangazi na mama zetu wanashindwaje kuwashawishi wanaume kushiriki kwenda kanisani? Kwa nini nguvu hii ambayo haihitaji rasilimali fedha, haitumiki kupunguza changamoto hii, ambayo inaelekea kuwa sugu?
Kuna wakati ukihudhuria kanisani, unakuta uwiano ni wanawake kuwa theluthi mbili na wanaume theluthi moja. Unakaa kwenye jumuia unakuta ni wanawake na watoto, labda na mwanume mmoja. Kama akina mama wanaweza kuzengea fedha ya kucha, nywele na marejesho wanashindwaje kuwashawishi wanaume kwende kanisani?

Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Yohane Paulo ll, Buyuni, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es salaam, Padri Bartazari Minde akibariki vipaji wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya Sikukuu ya Bikira Maria, iliyoadhimishwa hivi karibuni parokiani hapo.