Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

Mchakato Bagamoyo kuwa Jimbo mbioni

Kanisa la Parokia ya Bagamoyo, Jimbo Katoliki la Morogoro. Kanisa la Parokia ya Bagamoyo, Jimbo Katoliki la Morogoro.

DAR ES SALAAM

Na Mathayo Kijazi

Mchakato wa Bagamoyo kuwa Jimbo Katoliki, bado unaendelea huku ikielezwa kwamba katika Kanisa Katoliki, hakuna Jimbo linalotokea bila kuwa na mradi, yaani (project), kuhusu kuanzishwa kwa Jimbo husika.
Ufafanuzi huo ulitolewa hivi karibuni na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi wakati akizungumza na gazeti Tumaini Letu katika mahojiano kuhusu Jubilei ya Miaka 25 ya Uaskofu wake, inayotarajiwa kuadhimishwa Mei mwaka huu.
Katika mahojiano hayo, Askofu Ruwai’cihi alizungumzia Mchakato wa Bagamoyo kuwa Jimbo, ambapo alisema kuwa Jimbo Katoliki la Morogoro ndilo Jimbo Mama litakalozaa Jimbo tarajiwa la Bagamoyo, bado linaendelea na mchakato huo.
“Kwanza ifahamike kuwa hakuna Jimbo linalokuwepo bila ‘project’, kwani ni lazima kuwepo na ‘project’. Kama tunavyofahamu kwamba Jimbo Katoliki la Morogoro ndilo Jimbo mama, hadi sasa bado linaendelea na ufuatiliaji juu ya mchakato huo,” alisema Askofu Mkuu Ruwa’ichi.
Mchakato wa eneo kuwa Jimbo Katoliki
Kwa mujibu wa Askofu Mkuu Ruwa’ichi, Mchakato wa Bagamoyo kuwa Jimbo, suala la mahali kupewa hadhi ya kuwa Jimbo, haliendi kiholela, bali kuna majukumu ambayo yanapaswa kutekelezwa, ikiwemo kukusanya taarifa za kutosha kuhusu eneo hilo.
“Kwanza ni kweli kwamba kuna shauku ya Bagamoyo kupewa hadhi ya kuwa Jimbo, hii shauku imekuwepo kwa muda mrefu, na wengi walitegemea kwamba tulipoadhimisha Miaka 150 ya Kanisa Katoliki Tanzania kule Bagamoyo, kuwa ingetangazwa, na wengi walilichukulia kwa urahisi sana,” alisema Askofu Mkuu, na kuongeza;
“…Jukumu la kwanza ni kukusanya taarifa ambazo zinabainisha mambo kadhaa, na kwa nini hilo eneo linafikiriwa lipewe hadhi ya kuwa Jimbo.”
Miongoni mwa mambo yanayoangaliwa ili eneo lipewe hadhi ya kuwa Jimbo, kadri ya Askofu Mkuu Ruwa’ichi ni pamoja na idadi ya Waamini waliopo, kuzifahamu tamaduni zinazotawala katika eneo hilo, na pia kuufahamu uchumi utakaosaidia kuliendesha Jimbo hilo.
Aliongeza pia kuwa kabla ya eneo kupewa hadhi hiyo, ni lazima kwanza ifahamike kwamba watendakazi wa Jimbo hilo wakiwemo Mapadri, Watawa, na Makatekista, ni wangapi na watatoka wapi.
Kufuatia shauku hiyo, Askofu Ruwa’ichi aliwasihi Wakristo kufahamu kuwa licha ya kwamba Jimbo tarajiwa la Bagamoyo litazaliwa kutokana na kumegwa kutoka Jimbo Katoliki la Morogoro, bali pia Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam litachangia baadhi ya Parokia zitakazounda Jimbo la Bagamoyo.
“Lakini ikumbukwe kuwa mzazi wa Jimbo hilo, siyo Dar es Salaam, bali ni Morogoro. Pamoja na hilo, lakini mwenye uzito hapa, kwa kweli ni Dar es Salaam. Na hili suala la minong’ono lililotawala kwa kipindi mpaka mwaka ule wa 2018, niseme tu wazi kwamba lilibaki minong’ono, halikuwa limewekwa kwenye karatasi. Ni lazima ‘data’ zikusanywe, ziwekwe vizuri, halafu zipelekwe Roma,” alisema Askofu Mkuu.
Alisema kuwa andiko la kwanza lilifanyika mwaka 2019, na baada ya hapo likatumwa kwenda Roma, na hivyo Roma ikarudisha ujumbe kwa kuuliza maswali ya nyongeza, ambayo yalilengwa kwa Jimbo Katoliki la Morogoro, pamoja na Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.
“Tumejipanga, tumezungumza mimi na Askofu wa Jimbo Katoliki la Morogoro, tukaafiki kwamba yale maswali, majibu yake yatakuwaje. Kwa kifupi maswali yalikuwa kama haya, ‘je, mnapoomba lizaliwe Jimbo la Bagamoyo kutoka Jimbo la Morogoro, mnalirithisha nini Jimbo la Bagamoyo? Ni vitu gani ambavyo mnalirithisha Jimbo lianze maisha navyo? Na Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam pia likaulizwa, je ni vitu gani ambavyo mtalirithisha Jimbo ambalo nyie mtakuwa wazazi wenza?” alisema Askofu Mkuu.
Askofu Mkuu alisema kuwa moja ya vitu ambavyo Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam limefanya, ni kwamba tayari limeshajenga nyumba ya Askofu katika Jimbo hilo tarajiwa la Bagamoyo, ambayo imegharimu zaidi ya Shilingi milioni 600.
Aliongeza pia kuwa bado kuna uhitaji wa kujenga nyumba ya Watawa watakaoihudumia nyumba ya Askofu, Ofisi za Askofu au Ofisi za Jimbo, ambazo bado hazijajengwa, akisema kuwa katika harakati za kuifanya Bagamoyo kuwa Jimbo, ni lazima kwanza mambo hayo yafanyiwe kazi.
Maeneo yanayotarajiwa kuunda Jimbo Katoliki la Bagamoyo:
Hapo awali alipozungumzia kuhusu maeneo yatakayomegwa ili kuifanya Bagamoyo kuwa Jimbo Katoliki, Askofu Mkuu alisema kwamba wamependekeza kuwa Wilaya ya Chalinze, Wilaya ya Bagamoyo, pamoja na sehemu ya Wilaya ya Kinondoni ni miongoni mwa maeneo yanayotarajiwa kuunda Jimbo hilo Katoliki tarajiwa.
Aidha, Askofu Mkuu alisema kuwa kinachosubiriwa kwa sasa, ni majibu kutoka Roma, endapo Roma itaridhia Bagamoyo kupewa hadhi hiyo, hatua nyingine zitafuata ili kulipata Jimbo hilo jipya.
Athari Majimbo yatakayomegwa
Askofu Mkuu alibainisha kuwa hakuna athari kwa Majimbo mengine kumegwa, kwa sababu kuundwa kwa Jimbo lolote, kuna lengo la kuboresha huduma za Kichungaji kwa Waamini, hivyo hakuna Jimbo linaloumia pale huduma zinaposogezwa karibu zaidi na Waamini, badala yake ni faida kwa Majimbo yaliyokuwepo, na Jimbo linalozaliwa.
Aidha, Askofu Mkuu Ruwa’ichi aliwasihi Waamini kwa ujumla kuwa wajiweke vizuri kwa kupania kuuishi Ukristo, akiwasisitiza pia kwamba wawe ndani ya Jimbo Katoliki la Bagamoyo au nje ya Jimbo hilo, bali wawe ni Wakristo wanaotoa ushuhuda imara wa Kikristo.

Rate this item
(0 votes)

Leave a comment

Make sure you enter all the required information, indicated by an asterisk (*). HTML code is not allowed.