Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

Kayanga: Jimbo Kongwe lililopitia mabonde, milima

KAYANGA

Na Angela Kibwana

Jimbo Katoliki la Kayanga ni mojawapo kati ya Majimbo 34 ya Kanisa Katoliki nchini Tanzania, ambalo limo katika Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza.
Jimbo hili linaundwa na wilaya mbili ambazo ni wilaya za Karagwe na Cherwa. Upande wa kaskazini linapakana na Uganda-Jimbo Kuu Katoliki la Mbarara. Upande wa Magharibi linapakana na Rwanda, na upande wa Mashariki linapakana na Wilaya ya Misenyi na kusini linapakana na wilaya ya Ngara nchini Tanzania.
Jimbo Katoliki la Kayanga lilitangazwa rasmi na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedict XVI Agosti 14 mwaka 2008, ambalo lilimegwa kutoka Jimbo Katoliki la Rulenge – Ngara, na hatimaye kuzaliwa majimbo mapya mawili, yaani Jimbo Katoliki la Rulenge – Ngara, na Jimbo Katoliki la Kayanga.
Kunako mwaka 1929 ilianzishwa  Apostolic Vicariate ya Rulenge-Ngara kutokana na Apostolic Vicariate ya Tabora, ambapo Machi 25  mwaka 1953 Rulenge ilitangazwa kuwa Dayosisi. Hivyo, tarehe 14 Agosti 2008, ikamegwa Dayosisi ya Rulenge na hivyo kuanzishwa Jimbo Katoliki jipya la Kayanga.
Jimbo Katoliki la Kayanga lilizinduliwa Novemba 06 mwaka 2008, ambapo Askofu Almachius Vincent Rweyongeza aliwekwa wakfu akiwa Askofu wa kwanza wa jimbo hilo lenye kilomita za mraba 70,716 likiwa na wakazi zaidi ya laki 6, Wakatoliki wakiwa ni asilimia 60 Jimboni humo, kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012.
Jimbo Katoliki la Kayanga lilianzishwa likiwa na Mapadri 24, hivyo kwa wastani, kila Padri mmojawao anahudumia waamini 11,200 katika Parokia 11 ilivyokuwa katika mwaka wa 2008, idadi ya watawa wa kike walikuwa 61 wa Shirika la Kijimbo.
Katika muktadha huo, Mhashamu Askofu Almachius Rweyongeza wa Jimbo Katoliki la Kayanga anamshukuru Mungu kwa mafanikio ya kiroho yaliyopatikana Jimboni humo, hasa ongezeko la Mapadre, Watawa wa kike, na Makatekesta ambao wamekuwa chachu ya kuimarisha katekesi kwa waamini.
Anabainisha kuwa hadi sasa Jimbo hilo lina jumla ya Mapadre 51, Watawa 94 wa kike, na ongezeko la Makatekesta kutoka 398 katika kipindi cha mwaka 2008, na kufikisha idadi ya Makatekesta 438 kwa mwaka 2022.
Aidha, alisema kuwa kwa kipindi cha miaka 14 tangu kuanza kwa Jimbo hilo kunako mwaka 2008 hadi mwaka huu 2022, kumekuwa na ongezeko kubwa la wahudumu, hasa Mapadre na miito ya Upadre, ambapo kwa mwaka huu amewapatia Daraja Takatifu Mapadre wapya watatu, na kufikisha idadi ya Mapadre 51 jimboni humo.
Hata hivyo ametaja pia mafanikio mengine, hasa ongezeko la familia za Kikatoliki kupitia Sakramenti ya Ndoa Takatifu, hali iliyosaidia kupunguza ndoa za mseto, uchumba sugu, ndoa mgando, ndoa za mitala, pamoja na kupungua kwa ndoa za kiserikali.
Miongoni mwa mafanikio mengine jimboni humo ni ongezeko la Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo kutoka Jumuiya 1,039 hadi kufikia Jumuiya 1657, pamoja na uwepo wa Vituo vya Hija ambavyo amevitaja kuwa ni ‘Zahanati za Kiroho’ kwa ajili ya kutibu mahangaiko ya waamini.
Alisema kuwa wakati jimbo linazinduliwa lilikuwa na Parokia 11 tu, Vigango 234, Jumuiya za Kikristu 1,039 na Mapadre 24, Masista wa Jimbo 61 wa Shirika la Mitume wa Upendo, Upendo ambalo ndilo Shirika la Jimbo Katoliki la Kayanga, wakiwamo Makatekesta 398.
“Wahenga wetu wamesema ‘daima mwanzo ni mgumu’, ugumu huu ulitokana na shida za kiuchumi, hasa kuweka miundombinu ya msingi ya kichungaji na kijamii.
Namshukuru Mungu wakati jimbo linazinduliwa, Kanisa Kuu la Mtakatifu George, Kayanga, lilishajengwa na kutabarukiwa na Askofu Severine Niwemugizi wa Jimbo Katoliki la Rulenge - Ngara, Septemba 1, 2008, siku tano kabla ya kuzinduliwa kwa Jimbo Katoliki la Kayanga” alisema Askofu huyo.
Askofu Rweyongeza anasema kwamba alipokabidhiwa Jimbo la Kayanga hakuwa na uzoefu wowote wa kuzindua jimbo, hakuwa na ujanja wala mbinu za kuongoza jimbo hilo. Hivyo, aliandika katika Ngao yake ya Kiaskofu akijisalimisha kwa Bwana kwa kutumia maneno yasemayo: “Mimi ni Mtumishi wa Bwana.”
“Nilijisalimisha kwa Mungu kwa kutumia maneno ya Bikira Maria. Nilimkabidhi yote Mungu kwa sababu Mwenyezi Mungu asipojenga Jimbo Katoliki la Kayanga, wajengao wanajisumbua bure, nami nikiwa mmojawapo. Kusema kweli, Mwenyezi Mungu amenitendea makuu kwa kipindi cha miaka 14, kwani nimeshuhudia mafanikio makubwa,” alisema Askofu Rweyongeza.
Anasema vile vile kuwa licha ya idadi ndogo ya Mapadri wanaotoa huduma za kiroho Jimboni humo, anashukuru pia mchango wa Makatekesta ambao ni wasaidizi wa karibu wa Mapadre, hasa Vigangoni na Vijijini, kwa sababu Parokia moja inakuwa na vigango zaidi ya 30 ambavyo vinahudumiwa na Mapadre wawili, hivyo  Makatekesta wanasaidia sana kutoa huduma za kiroho kwa waamini wao.
Anasema kuwa hadi sasa kuna ongezeko la Parokia, kutoka 11 katika kipindi cha mwaka 2008, na sasa imefikia idadi ya Parokia 20 mwaka huu 2022, zenye Mapadre wenye makazi maalumu  katika Parokia hizo.
“Mapadri bado ni wachache kulingana na idadi ya Waamini Jimboni humu, kwani baadhi ya Parokia moja moja anaishi Padre mmoja tu, ambapo inakuwa ni kazi ngumu. Hata hivyo naamini kwamba Mungu ndiye anayeweza kutufanikishia kwa kuwategemeza katika Utume wa Kanisa licha ya uchache wao.”
Mbali na hayo, Askofu Rweyongeza amesifu ongezeko la Vyama vya Kitume Jimboni humo, ambavyo ni uhai wa Kanisa na Jimbo, na alivitaja kuwa ni Utoto Mtakatifu, WAWATA, UWAKA, VIWAWA, Lejio ya Maria, Wafransiskani na vyama vingine vya kitume, ambavyo ni chachu ya mafanikio ya kiroho Jimboni humo.
Amewasifu pia Viongozi wa Halmashauri Walei Katoliki (HAWAKA), ambao ni washiriki wenza katika shughuli za uchungaji ambao umejengwa na viongozi wanaojituma, ili kuhakikisha Jimbo linasonga mbele kiimani.
Sambamba na hayo kwa upande wa taasisi za Dini, ametaja uwepo wa Vituo vya Hija ambavyo ni ‘Zahanati za Kiroho’ zinazosaidia Waamini wengi Wakatoliki na wasio Wakatoliki kwenda kuchota neema na baraka kutoka katika vituo hivyo vya hija na maisha ya kiroho.
“Nilivizindua Vituo hivi vya hija  wakati Jimbo lilipoanza. Nikaona kwamba hili ni hitaji kubwa la kuwasaidia Waamini na jamii kuhusu masuala mbalimbali ya kiroho, kiimani na uponyaji, nikiamini kwamba Vituo hivi vya Hija ni zahanati za kiroho.”
Kalvario Kayungu ni miongoni mwa Vituo vya Hija jimboni humo, kilichozinduliwa septemba 14 mwaka 2011 kwa heshima ya Msalaba Mtakatifu. Pia, kituo kingine cha hija cha Lurd Bughene kilijengwa kwa heshima ya Bikira Maria wa Lurd  na Afya ya Wagonjwa, kikizinduliwa Februari 11, mwaka 2012.
Askofu Rweyongeza anasema kuwa familia ya Mungu Jimboni humo huwa wanafanya hija za kijimbo kila Februari 11, Kitaifa na Kimataifa huko Lurd Bughene katika kuadhimisha sikukuu ya Bikira Maria wa Lurd na Afya ya Wagonjwa. Pia, wanafanya hija za kijimbo, kitaifa na kimataifa huko Kalvario Kayungu kila ifikapo Septemba 14, kwa heshima ya kutukuka  kwa Msalaba.
Licha ya Jimbo hilo kuwa miongoni mwa majimbo machanga nchini Tanzania, limewekeza katika taasisi mbalimbali za jamii, hususan zinazogusia masuala ya Elimu kama vile shule, vituo vya afya hosptatali na zahanati, pamoja na tasisi za mazingira (CHEMA).
“Tuna taasisi muhimu sana Jimboni ijulikananyo kama CHEMA, kifupi cha Community Habitat Environment Management, kama mwitikio kwa Baba Mtakatifu kuhusu barua yake ya kitume ‘Laudato Si’ , inayohusika hasa na utunzanji wa mazingira,” alisema.
Anaeleza kwamba Taasisi ya CHEMA inashughulika na mazingira, kama vile upandaji miti na utengenezaji wa vitalu mbalimbali vya miti mbalimbali ya matunda na miti ya mbao, kivuli na biashara. Pia, ikiwemo utengenezaji wa majiko sanifu yanayotumia kuni kidogo, au majiko yanayotumia unga wa mbao kunusuru uangamizaji wa miti kwa ajili ya kujipatia kuni na mkaa, sanjari na ufugaji wa nyuki.
Wakati huo huo Askofu Rweyongeza anabainisha kwamba uharibifu wa mazingira ni moja kati ya changamoto zinazolikumba Jimbo hilo, hususani uharibifu wa vyanzo vya maji; ukataji wa miti kiholela; uchomaji moto misitu; na utumiaji wa sumu kuua magugu kwa kulima mazao ya muda.
“Jimbo langu limekumbwa na uharibifu wa mazingira, kwani mtu anakata mti wa miaka 30 ili apande mazao ya haraka kujipatia pesa ya haraka, bila kuangalia ni aina gani ya uharibifu wa mazingira anaousababisha.”
Kupitia taasisi ya CHEMA, Askofu Rweyongeza anasema kwamba anahimiza watu waoteshe miti ili kuhakikisha wanatunza uoto uliopo kwa sababu ya uharibifu wa mazingira, kwani ni hatari katika maisha ya binadamu na viumbe vyote.
“Jimbo Katoliki la Kayanga linao msitu wa mfano kuhakikisha kwamba mazingira yanatunzwa, nami namshukuru Mungu nina msitu wangu wa mfano ambao unaitwa bustani ya Edeni, ambako lengo ni kutunza miti ya asili ya matunda ambayo imeshatoweka. Nimepanda miti ya Kibiblia ambayo ni mizeituni, mitende, mitini na mizabibu, ambayo ninayo kwenye shamba langu la ekari 05”.
Itaendelea wiki ijayo.

Rate this item
(0 votes)
Last modified on Friday, 02 September 2022 08:56
Super User

Selfies labore, leggings cupidatat sunt taxidermy umami fanny pack typewriter hoodie art party voluptate. Listicle meditation paleo, drinking vinegar sint direct trade.

www.themewinter.com

Leave a comment

Make sure you enter all the required information, indicated by an asterisk (*). HTML code is not allowed.