Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

Uchangiaji Damu tiba katika uokoaji Uhai

Dar es Salaam

Na Edvesta Tarimo

Juni 14 kila mwaka, nchi mbalimbali Duniani huadhimisha Siku ya Wachangia Damu Duniani (World Blood Donor Day: WBDD).
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (World Health Organisation: WHO), kila mwaka watu takribani milioni 92 ni wachangiaji wa damu, asilimia 50 ya watu hao wanatoka katika nchi zinazoendelea, ambao wanafanya asilimi 15 tu ya watu wote Duniani.
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu akiwasilisha hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 mwanzoni mwa mwezi Mei mwaka 2023, katika hotuba hiyo kuimarisha upatikanaji na udhibiti wa dawa, vifaa tiba, vitendanishi, na damu salama, ni baadhi ya maeneo yaliyopewa vipaumbele katika wizara hiyo.
Shirika la Afya Duniani (World Health Organisation: WHO), linasema kuwa upatikanaji wa damu salama ni sehemu ya utekelezaji wa lengo la huduma za afya kwa wote, lakini pia ni kipengele muhimu katika utendaji kazi wa mifumo ya afya kote Duniani.
Siku ya Wachangiaji Damu Duniani huadhimishwa kwa kutambua na kuenzi siku ambayo alizaliwa mvumbuzi wa makundi ya damu A, B, na O (ABO blood group system), huko New York, Marekani mwaka 1943, ni raia wa Austria, Dk. Karl Landsteiner aliyezaliwa Vienna mwaka 1868.
Daktari huyo alikuwa ni mtafiti Vienna, Austria, na tangu mwaka 1922 alihamia katika taasisi ya Rockefeller ya Utafiti wa Matibabu huko New York, Marekani. Mwaka 1900 uhamisho wa damu ulikuwa umefanyika kwa zaidi ya karne mbili kabla, bila kufikia matokeo mazuri.
Mwaka 1901, daktari wa Austria, Karl Landsteiner alipindua Ulimwengu wa Uhamisho wa Damu kutokana na ugunduzi wa mfumo wa makundi ya damu ABO, na mwaka 1930 alipewa tuzo ya Nobel ya Dawa. Aliunganisha jina lake la ugunduzi wa makundi ya damu ABO na kipengele cha Rh na A.
Daktari Landsteiner ni mwandishi wa ripoti za tafiti mbalimbali, umuhimu msingi wa majaribio ya magonjwa, juu ya hemoglobinuria baridi, juu ya maambukizi makubwa na majaribio ya tafiti nyingine nyingi kuhusiana na damu.
Nchini Tanzania, Mpango wa Taifa wa Damu Salama Tanzania (National Blood Transfusion Service: NBTS), ulianza kuadhimishwa rasmi hapa nchini mwaka 2004, ingawa ulianza takribani katika miaka ya 1950.
Uchangiaji Damu kwa Hiari
Tanzania ni miongoni mwa nchi wanachama, hivyo kila ifikapo tarehe 14 Juni ya kila mwaka, huungana na Shirika la Afya Duniani (World Health Organization: WHO), na nchi wanachama kuwatambua, kuwashukuru, kuongeza uelewa na kuleta hamasa kwa wachangiaji, ili waendelee kuchangia damu, na wale ambao hawajawahi kuchangia damu, wajitokeze kuchangia.
Zaidi ya aslimia 70 ya idadi ya Watanzania ni vijana wa chini ya umri wa miaka 35, hii ni kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022. Kundi hili pia linatajwa kuwa nguzo muhimu katika uchangiaji damu kwa hiari.
Kijana Fredy Mavika ni mdau na balozi wa kuchangia damu, anasema kuwa ameshachangia damu zaidi ya mara 9, na ameanza tangu akiwa shule ya sekondari, mpaka sasa.
Akizungumza na mwandishi wa makala hii katika Hospitali ya Lugalo kitengo cha kuchangia damu jijini Dar es Salaam, anasema kuwa hawana elimu ya uchangiaji damu, kitu ambacho kwake anaona ipo sababu ya mtu binafsi kutambua mchakato wa uchangiaji damu.
Mavika anabainisha kuwa tangu alipoanza kuchangia damu, hajawahi kusikia utofauti wa kiafya kama ambavyo baadhi ya watu katika jamii wamejenga dhana potofu kwamba damu inaisha mwilini, na mtu hupata kizunguzungu.
Mavika anawasihi vijana na Watanzania kwa ujumla, kujitokeza kuchangia damu kwa hiari, kwani endapo utachangia damu zaidi ya mara tatu, ikitokea unauguliwa na mgonjwa anayehitaji kupata damu, kadi yako itatumika ili kupata huduma hiyo.
Faida za Kuchangia Damu kwa Hiari
Sadaka siyo lazima iwe fedha, hata hili la kuchangia damu ni kujisadaka kwa ajili ya wengine, ni sadaka ambayo ni hazina isiyotiwa kutu, wala kuliwa na mchwa.
Wataalamu wa afya wanasema kwamba mwanadamu pekee ndiye anayeweza kuchangia damu kwa ajili ya wahitaji wa damu, kwani haiwezekani kuunda damu katika maabara yoyote kuokoa maisha ya mwanadamu, hivyo utoaji damu kwa hiari, ndiko kutakakowezesha kuwakidhi wenye uhitaji huo.
Katika uchangiaji damu huo, baada ya kuwa mwanachama wa kuchangia damu, mwanaume anaweza kuchangia mara nne, na mwanamke mara tatu katika mwaka.
Afisa Mhamasishaji Msaidizi Kitengo cha Damu Salama,  Elizabeth Msemwa anafafanua kuwa licha ya kwamba kuchangia damu ni ishara ya upendo, pia zipo faida lukuki na chanya za kiafya ambazo mchangiaji wa damu anazipata bure pindi anapofanya tendo hilo la hiari, na la upendo kwa wengine.
Anabainisha kuwa mchangia damu anapata vipimo maalum ambapo pia katika utoaji damu inawezekana kugundua pia ugonjwa mapema unaoanza kuunyemelea mwili wake, na hivyo kuanza matibabu mapema.
Dhana potofu dhidi ya Kuchangia Damu
Waswahili walinena, “Jambo usilolijua, ni kama usiku wa giza,” “Asiyejua maana, usimwambie maana, maana atapoteza maana, kama si kuharibu kabisa,” na, “Tatizo lisikie kwa mwingine, usiombe likakufika.”
Pengine baadhi ya watu katika jamii huogopa kwenda kuchangia damu kwa kuogopa maneno ya wenzao, ama hawana elimu sahihi kuhusu kuchangia damu kwa hiari.
Siku moja alisikika mtu akisema, “Ukishachangia damu, baada ya muda fulani usipokwenda kuchangia tena, itakuletea shida.” Wengine hujisemea, “Nichangie damu ya nini wakati sipati chochote, na damu yenyewe kwanza inauzwa?”
Elizabeth anakata mzizi huo kwa kusema kuwa hizo ni dhana potofu, na kwamba mchangiaji anapofika kituoni, kwanza anapewa elimu kuhusu kuchangia damu, anafanyiwa vipimo likiwemo suala la kuangalia uzito, kiwango cha damu aliyonayo kabla ya kuanza kutolewa damu.
Anaongeza kuwa endapo mchangiaji damu anakuwa hajakidhi vigezo vinavyotakiwa, hatachangia damu. Na endapo pia atakuwa chini ya umri wa miaka 18 au ni mjamzito, hawataruhusiwa kuchangia, hata kama vigezo vingine vimekidhi.
Aidha, Afisa huyo anaongeza kuwa baadhi ya watu katika jamii wanashindwa kutambua kuwa,wanapochangia damu kwa ajili ya kuwaongezea wengine, au mgonjwa haitumii damu hiyo ambayo imetolewa muda huo, bali inachukuliwa nyingine kwenye benki ya damu, kisha ikishachakatwa, inarejeshwa kwa ajili ya wahitaji wengine.
“Labda niseme kwamba watu wanadhani damu inapotolewa, mgonjwa anawekewa muda huo huo, la hasha. Damu lazima ipitie uchakatwaji. Huwezi kutoa na ikatiliwa mwingine hivi hivi tu,” anasema Afisa Elizabeth.
Elimu ya Kuchangia Damu kwa Hiari
Judith Charle, Msimamizi wa huduma za wachangiaji damu kutoka Mpango wa Taifa wa Damu Salama Makao Makuu, anasema kuwa timu za ukusanyaji damu huelimisha jamii kuhusu suala la kuchangia damu kupitia vyombo mbalimbali vya habari.
Anaongeza kwa kusema kuwa wanaendesha kampeni ya uchangiaji damu katika sehemu mbalimbali, mathalan kwenye Vituo vya Kanda, Vituo vya Damu Salama vya Hospitali za Rufaa za Kanda, Hospitali za Rufaa za Mikoa, na Hospitali za Wilaya zote nchini, ili kuleta mwamko kwa jamii kuhusu uhitaji wa zao hilo.
Anaongeza pia kuwa wanatumia Siku ya Wachangiaji Damu Duniani, Juni 14, kuwashukuru, kuongeza uelewa, na kuleta hamasa kwa wachangiaji ili waendelee kuchangia damu, na wale ambao hawajawahi kuchangia damu, wajitokeza kuchangia.
Uchangiaji damu umeendelea kuongezeka, kwani mwamko ni mkubwa, na uelewa pia unaongezeka, kwa sababu mwitikio wa uchangiaji damu kwa hiari kadri miaka inavyokwenda, ndivyo unavyozidi kuongezeka, na dhana nzima ya uchangiaji damu pia inaongezeka.
Uhitaji wa Damu Nchini Tanzania
Dokta Judith Charle aliliambia Tumaini Letu kuwa kulingana na Shirika la Afya Duniani, (World Health Organization: WHO), mahitaji ya damu ya nchi husika ni aslimia 1 ya wingi wa watu.
Anasema kuwa mahitaji ya damu salama ni takribani chupa laki 5 na elfu 90 (590,000) kwa mwaka kulingana na Shirika la Afya Duniani.
Aidha, anaongeza kuwa kwa sasa hawajaweza kufikia mahitaji kwa sababu ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, na kwamba kabla ya hapo Watanzania walikuwa takribani milioni 50 hadi 55, kwa hiyo mahitaji ya damu walilenga kukusanya chupa laki 5 hadi 5 na nusu (500,000 hadi 550,000) za damu salama.
Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi iliyofanyika mwaka 2022, Tanzania ina watu 61,741,120, huku Bara ikiwa na watu 59,851,357, na Zanzibar watu 1,886,773.
Dokta Charle anasema kuwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2023/2024 na Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, wameweka malengo ya kukusanya chupa laki 5 hadi 5 na nusu za damu salama.
Wito kwa Jamii wa Kuchangia Damu kwa Hiari
Dk. Judith Charle anaiasa jamii kuona umuhimu wa kuchangia damu kwa hiari, ili kuweza kuwasaidia Watanzania ambao wanahitaji huduma ya damu katika hospitali mbalimbali.
Aliwasihi kutembelea Vituo vya Mpango wa Taifa wa Damu Salama ambavyo vipo katika ngazi ya Kanda, Mkoa, Hospitali za Rufaa za Kanda, Hospitali za Taifa, na Hospitali zote za Halmashauri nchini, ambapo Vituo vya Uchangiaji Damu vinapatikana.
Hakuna mbadala wa damu, mgonjwa anapohitaji huduma ya damu anahitaji damu ya kutoka kwa binadamu mwenzake ili kuweza kumwongezea, na damu lazima iandaliwe ili pale dharura ya kumwongezea mgonjwa damu inapotokea, damu hiyo iwe tayari ili kuweza kuokoa vifo vinavyotokana na upungufu wa damu katika hospitali mbalimbali nchini.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Kila Wiki ya Ugavi wa Damu wa Kundi O ya AABB (Association for the Advancement of Blood and Biotherapies), ambayo ni Chama cha Kuendeleza Damu na Tiba Viumbe iliyotolewa mwishoni mwa mwezi Mei mwaka 2023, inasema kuwa uchangiaji wa damu unahitajika ili kuhakikisha upatikanaji wa damu.
Chama cha kuendeleza Damu na Tiba viumbe (Association for the Advancement of Blood and Biotherapies: AABB) inawahimiza wale wanaostahili kuchangia damu mara kwa mara, ili kuhakikisha kwamba nyenzo hiyo muhimu ya kuokoa uhai, inapatikana kwa wagonjwa wanaohitaji.
Kaulimbiu ya Kimataifa ya Siku ya Wachangia Damu Duniani, hubadilika kila mwaka kwa kutambua watu waliojitoa kuchangia damu yao kwa watu wengine wasiowafahamu.
Kwa maana hiyo, tuunganishe nguvu zetu pamoja kwa ajili ya kujitokeza kuunga mkono suala la uchangiaji damu kwa hiari, ili kuokoa maisha ya watu.
Karibu katika ‘group’ la WhatsApp la kuchangia damu kwa hiari la Marafiki wa Vijana Club, kipindi kinachoruka kupitia Tumaini Televisheni. Changia damu, okoa maisha, wasiliana na ‘group’ la WhatsApp +255 713 062 953.

Rate this item
(0 votes)

Leave a comment

Make sure you enter all the required information, indicated by an asterisk (*). HTML code is not allowed.