Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

Juma Kaseja kurejea Ligi Kuu?

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Kocha mkuu wa timu ya KMC ya Kinondoni Jamhuri Kihwelo amesema anataka kufanya mpango wa kumshawishi golikipa mstaafu Juma Kaseja, ili msimu ujao arejee langoni kuitumikia tena timu hiyo.
Kaseja alitangaza kustaafu soka mwishoni mwa msimu wa 2021/2022 akiwa na timu ya KMC na kuhamia kwenye jukumu lingine la kuwa kocha wa magolikipa wa timu za taifa.
Kihwelo, maarufu kama Julio, hivi karibuni alivutiwa na kiwango kilichoonyeshwa na nyanda huyo wa zamani wa Moro United, Simba SC, Yanga na Taifa Stars, wakati alipoichezea timu ya Ali Kiba katika mechi ya hisani dhidi ya timu ya Mbwana Samatta.
Katika mechi hiyo ya tamasha la SamaKiba, Kaseja alionyesha kwamba bado ana kitu anaposimama langoni, licha ya timu yake kufungwa mabao 4-2 na timu ya Samatta kwenye uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es salaam.
“Kaseja bado ni kipa mzuri sana licha ya kustaafu.Nikiwa kama kocha wa KMC, nitamshawishi ili aweze kurudi na kuitumikia timu hii msimu ujao,”alisema Julio.
Alisema kwamba Mungu akipenda atamchukua kipa huyo na kumrejesha ndani ya KMC kwa sababu ni mtu anayejitambua kwa kujali mazoezi, na bado uwezo wa kudaka anao.
Hadi gazeti linaingia mtamboni, juhudi za kumpata Kaseja mwenyewe ziligonga mwamba kufuatia simu yake kuita bila kupokelewa, ingawa mara ya mwisho wakati ametangaza kustaafu soka, alidai kuwa amefanya hivyo ili kuwapa nafasi vijana wanaochipukia kwa sasa.
Mbali na hilo, inaelezwa kwamba alichoshwa na maneno ya watu waliokuwa wakimzodoa kwa madai kwamba anaziba nafasi za vijana, wakati yeye tayari umri wake umekwenda.
Kaseja alianza kuonekana kwenye medani ya soka la ushindani mwaka 2000 akiichezea Moro United aliyojiunga nayo ikiwa Ligi Kuu, akitokea Shule ya Sekondari ya Makongo, na kucheza kwa msimu mmoja.
Mwaka uliofuata alijiunga na Simba aliyoichezea kwa mafanikio kwa zaidi ya miaka 10 kwa misimu tofauti.
Pia, Kaseja aliichezea Yanga katika vipindi viwili kama ilivyo kwa Simba, na baadaye alijiunga na Kagera Sugar, kisha kutimkia Mbeya City, na kumalizia KMC.

Rate this item
(0 votes)

Leave a comment

Make sure you enter all the required information, indicated by an asterisk (*). HTML code is not allowed.