Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

Maana ya ‘ndondo’ katika soka la mitaani

DAR ES SALAAM

Na Arone Mpanduka

Ukikatiza katika mitaa mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam, hasa muda wa jioni, utakutana na vikundi vya vijana wakicheza soka.Mara nyingi huwa wanakuwa na timu zao zenye majina yaliyobeba mitaa wanayoishi.
Pia, huenda mbali zaidi na kuanzisha ligi za mtaani ambazo hutumika kuburudisha nafsi zao na za mashabiki wao.
Wachezaji hunufaika na zawadi zinazowaniwa kwenye ligi husika kama vile mbuzi, ng’ombe, kuku pamoja na malipo ya kiasi kidogo cha fedha, huku mashabiki wakinufaika na burudani wanayopata kupitia timu za mitaa yao.
Utamaduni huo wa soka la mtaani umeibua jina maarufu la ‘Ndondo’.Jina hili limeibuka tangu miaka ya zamani, hasa kutokana na mtindo wa ligi na wachezaji wake.
Mtindo wenyewe ni namna wachezaji wanavyopatikana na kutumika katika timu za mitaani.
Neno ‘ndondo’ limeibuka kutoka kwenye wali maharage, na kama usivyofahamu, mboga ya maharage imepewa jina la ndondo, kivipi? Katika miaka ya zamani, wachezaji wengi wa mtaani malipo yao hasa yalikuwa wali na maharage, kwa maana kwamba mchezaji akitakiwa na timu fulani kwa ajili ya mechi za mtaani, atatakiwa kukusanyika na wenzake mapema kabla ya mchezo, na kinachofuatia ni kula wali na maharage, kisha mechi ikimalizika anapewa neno ‘asante’ na kuondoka.
Ikitokea viongozi husika wa timu wakijiongeza, mchezaji anapata walau nauli ya kwenda na kurudi pamoja na wali maharage.
Katika miaka ya hivi karibuni hadi sasa kumekuwa na mabadiliko kiasi, kwani licha ya mchezaji kula wali na maharage, pia hupewa posho fulani ambayo ndani yake inaweza kumsaidia kwa nauli na kununua mahitaji yake mengine madogo madogo.
Kutokana na kuwepo kwa staili hiyo, ndipo neno ‘ndondo’ likawa linatumika na kuvuma, hata wachezaji wenyewe wa mtaani wakikodiwa sehemu kwenda kuichezea timu fulani, utasikia “Ninakwenda kwenye ndondo”, akimaanisha anakwenda ‘kupiga’wali maharage na kucheza soka.
Huko kwenye soka la ‘ndondo’ masuala ya usajili yapo kama yalivyo kwenye ligi kubwa, ingawa tofauti yake ni kwamba usajili wa soka la mtaani hufanyika kulingana na mashindano maalum, na si msimu mzima wa mwaka ama miaka.
Kwenye soka la ‘ndondo’, kwa mwezi mchezaji anaweza kuchezea hata timu 10 zinazoshiriki michuano tofauti kwenye maeneo tofauti, kwa mfano, anaweza kuchezea timu A ya ligi fulani ya Ilala, na wakati huo huo akawa anachezea timu X ya ligi fulani ya mtaani huko Temeke, ilimradi tu hayo mashindano ya mtaani yawe hayana muingiliano wowote.
Kuna wakati hata wachezaji wanaocheza Ligi Kuu ama Daraja la Kwanza, nao wamekuwa wakiongeza nguvu kwenye ligi hizi za mtaani, wakiamini kwamba wanatoa mchango kwa timu za mitaa yao ambazo zimewalea na kufika walipofika.
Kwenye ligi hizo za mtaani, kama ikitokea kuna ligi ya kuwania kombe la mbuzi, basi mbuzi huyo atachinjwa na kuliwa na wali, pamoja na wachezaji wote walioshiriki kupata ubingwa.
Mbali na yote, mechi za mitaani ndizo zinazosaidia kuibua vipaji vya wachezaji ambao leo hii wanang’ara katika timu za Ligi Kuu nchini, hasa kutokana na kukosa mfumo thabiti wa kukuza vipaji vya vijana wadogo, kama ilivyo katika nchi zingine.

Rate this item
(0 votes)

Leave a comment

Make sure you enter all the required information, indicated by an asterisk (*). HTML code is not allowed.