Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

Adolf Mbinga anapotuachia Nyimbo zenye Mikasa ya kweli

DAR ES SALAAM

Na Arone Mpanduka

Tayari mwili wake umelala katika makaburi ya Kijiji cha Mpute huko mkoani Lindi, huku akiacha mabaki ya mtekenyo wa ala tamu za gitaa kwenye masikio ya mashabiki wake wa muziki wa dansi.
Ni ala za tamu na chungu,kwani kila shabiki anayekumbuka jinsi gitaa lilivyotekenywa kwenye wimbo maarufu wa ‘Kisa cha Mpemba’, ama ‘Bwana Kijiko’, anabaki kuwa na huzuni.Mtu huyu si mwingine bali ni marehemu Adolf Mbinga, mtaalamu wa kucharaza gitaa la solo na rhythm.
Mbinga ambaye alizaliwa mwaka 1967, alianza kuupenda muziki tangu akiwa kijijini kwao Mpute ambako mara kadhaa alikuwa akitumika kama miongoni mwa washereheshaji kwenye shughuli za jando, mwanzoni mwa miaka ya 1980.
Alikuwa akitumia sana gitaa la asili lililofungwa na kamba na nyaya katika shughuli hizo za jando.
Baadaye mwaka 1988 akajiongeza na kujiunga na Bendi ya Mondomondo huko Nachingwea.Mwaka 1989 akatua Dar es salaam akitokea ‘bush’ na kujiunga na Bendi ya Biko Stars na hakudumu, kwani mwaka 1992 akatimkia Bendi ya Carnival, na kupewa gitaa la rhythm.
Baadaye akapita bendi zingine nyingi, ikiwemo Diamond Sound, Twanga Pepeta, Mchinga Sound, na nyingine nyingi, ikiwemo Sikinde.
NEEMA
Huu ni wimbo wa kwanza kwa Mbinga kutunga katika maisha yake ya muziki akiwa na bendi ya Diamond Sound. Hiki pia ni kisa cha kweli ambacho kilimtokea mwenyewe wakati akiishi geto pale Kinondoni. Alimpata msichana kwa lengo la kuishi naye, lakini alimkimbia kwa sababu hakuwa na pesa.
Wimbo huo aliutunga mwaka 1996 akiwa na Diamond Sound, maarufu kama wana Kibinda Nkoi, ambao miaka hiyo ndiyo walioanza kuichangamsha nchi kwa miziki ya dansi la kizazi kipya.
KISA CHA MPEMBA
‘Kisa cha Mpemba’ ni miongoni kwa nyimbo maarufu kutunga akiwa Twanga Pepeta, na uliompa umaarufu. Wimbo huu ulitengenezwa mwaka 1998 katika studio za MJ Records (Master J). Hiki ni kisa cha kweli kabisa ambacho kilitokea Tabata ambapo Mbinga alishuhudia purukushani ya muuza duka mmoja (Mpemba) aliyepata sekeseke kutoka kwa jamaa ambaye mkewe alikuwa anapewa vyakula vingi kutoka duka la Mpemba huyo, kuliko thamani ya pesa aliyoacha.
Mbinga akatumia kisa hicho na kutengeneza wimbo ambao ndani yake aliongeza vionjo.
MTUHUMIWA
Mtuhumiwa si wimbo bali ni jina la utani alilopewa na wenzake mara baada ya kuiasi bendi ya Mchinga Sound.
Ikumbukwe kwamba mwaka 2000, Mbinga aliondoka ghafla katika bendi ya The African Stars ‘Twanga Pepeta’ na kwenda kumshawishi Mheshimiwa Mudhihiri Mudhihiri ambaye alikuwa Waziri kwa wakati huo, aanzishe bendi yake ambaye naye alikubali na kununua vifaa vya muziki.
Baada ya ushawishi huo kukubalika, ndipo wakaunda bendi ya Mchinga Sound ambayo ndani yake alikuwemo Mbinga mwenyewe, Mwinjuma Muumini, Deo Mwanambilimbi, Roshi Mselela, Rogart Hega Katapila, na wengine wengi.
Mbinga alitoka na tungo iitwayo ‘Kidomodomo’ambayo aliitunga akiwa Twanga Pepeta na kwenda kuirekodi Mchinga, na kufuatiwa na nyimbo zingine nzuri kama Kisiki cha Mpingo, na Fadhila kwa Wazazi.
Nyimbo zote za Mchinga Sound, kazi za kurekodi gitaa la solo na rhythm zilifanywa studio na Mbinga mwenyewe.
Wakati Mchinga Sound ilipokolea na kuwa maarufu nchini, ghafla Mbinga ambaye alikuwa kiongozi mkuu, aliondoka kwenye bendi hiyo na kurudi Twanga Pepeta. Kwa tafsiri nyingine ni kama alimuacha kwenye mataa Mheshimiwa Mudhihiri asijue nini cha kufanya, hasa ikizingatiwa alikuwa hajui lolote kuhusu masuala ya muziki, ikiwemo kuongoza bendi.
Hicho ndicho kikawa chanzo cha bendi hiyo kuvunjika na kusambaratika, kwani wanamuziki wengine wote waliondoka na kwenda kwenye bendi zingine.
Aliporudi Twanga Pepeta, wanamuziki wenzake walimpa Mbinga jina la mtuhumiwa wakiamini kwamba Mheshimiwa Mudhihiri alimtuhumu kwa usaliti wa bendi ya Mchinga Sound.
Hivyo, Mbinga ameondoka duniani akiwa ameacha majina ya utani ya ‘Mtuhumiwa’ na ‘Chinga One’.Jina la Chinga One lilitokana na kabila lake la Kimakonde.
KIFO CHAKE
Mwanzoni mwa mwaka huu, Mbinga aligundulika kwamba anaumwa mara baada ya ndugu, jamaa na marafiki kubaini kutetereka kwa afya yake.
Inaelezwa kwamba alikuwa akiumwa kwa muda mrefu ugonjwa ambao mwenywe hakutaka kuuweka hadharani, lakini aliwaficha hata ndugu na jamaa hadi kufikia katika hali mbaya.Jambo baya zaidi, alikuwa hataki kutumia dawa alizokuwa anapewa hospitalini.
Kufuatia hali yake kuwa mbaya zaidi, ilifikia hatua ikabidi asafirishwe kurudishwa kijijini kwao Mpute, ambako usiku wa Juni 15 mwaka huu, alifariki dunia na kuzikwa Juni 17.

Rate this item
(0 votes)

Leave a comment

Make sure you enter all the required information, indicated by an asterisk (*). HTML code is not allowed.